Kukomesha bidhaa feki vita ngumu

VITA ya kukomesha bidhaa bandia nchini inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na biashara hiyo kuhusisha makundi mengi yenye maslahi kinzani, kukosekana kwa elimu miongoni mwa watumiaji wa bidhaa na udhaifu wa kisera na kisheria ambao unasababisha mgongano wa kiutendaji baina ya mamlaka za kiserikali ambazo zinahusika moja kwa moja na suala hilo.

Kati ya sababu hizo, uchunguzi wetu unaonyesha kwamba mgongano wa kimaslahi baina ya baadhi ya taasisi za umma, ni kikwazo kikubwa katika kudhibiti bidhaa bandia. Ingawa vipo vyombo kadhaa vya kiserikali ambavyo vingeliweza kudhibiti kabisa bidhaa feki nchini kama Tume ya Ushindani (FCC), pamoja na mamlaka nyingine zinazoshughulika na bidhaa nchini kama Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na hata vyama vya walaji (Consumer Councils), kwa ujumla wao vinakabiliwa na mtihani mkubwa wa kudhibiti bidhaa bandia ambazo kila uchao zinazidi kuzagaa nchini.

Mgongano mkubwa wa maslahi unajidhihirisha kupitia FCC, yenye dhamana ya kudhibiti bidhaa bandia nchini kwa upande mmoja na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa upande mwingine. FCC, ambao ndiyo mamlaka yenye wajibu namba moja wa kudhibiti bidhaa bandia, wanakabiliwa na changamoto za kutosha kutokana na bidhaa hizo kuwa chanzo cha mapato siyo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu tu, bali hata TRA ambao kimsingi kazi yao kuu ni kukusanya mapato. Katika kutekeleza wajibu wa kukusanya mapato, TRA hawajisumbui kabisa na ubora au uhalali wa bidhaa yoyote ama inayoingizwa nchini au inayotengenezwa nchini, mbali ya kukusanya kodi halali za serikali kwa mujibu wa sheria.

Ndio maana, TRA walipoulizwa iwapo wana takwimu zozote na taarifa kuhusiana na bidhaa bandia na zile zisizo na ubora, maofisa wake walikiri kuwa wao hawana taarifa hizo kwani hawahusiki kuangalia ubora wa bidhaa na kumshauri mwandishi wetu kuwasiliana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupata tarifa hizo.

Katika mazingira hayo, FCC ambao wanapambana kulinda haki za walaji, kukuza ushindani wa kibiashara kwa kuzuia vitendo vyovyote vinavyofubaza ushindani na kuzuia aina zote za udanganyifu wa kibiashara kama uuzaji wa bidhaa feki, katika kutimiza malengo yao, wanakutana na vyombo vingine vyenye malengo ya kuongeza mapato ya serikali ambavyo, kwao suala la ama ubora au uhalali wa bidhaa siyo jambo la msingi ilamradi wafanyabiashara wamezingatia taratibu za kiforodha za kuagiza bidhaa kutoka nje na kulipa kodi stahiki za serikali.

Chanzo chetu cha habari kutoka moja ya mamlaka za serikali kilisema: “Ni kweli FCC wana wajibu wa kudhibiti bidhaa feki, lakini kumbuka TRA nao wana malengo yao ya kukusanya mapato. Kuna nyakati juhudi za FCC zinaweza kuonekana kama kikwazo kwa TRA kufikia malengo. TRA wanataka kuongeza makusanyo, hawashughuliki na ama ubora au uhalisia wa bidhaa.”

Katika mazingira hayo kunakuwako na mvutano usio rasmi wa kitaasisi wa ndani kwa ndani ambao siyo rahisi kueleweka kwa wananchi.

Chanzo hicho kilieleza kwamba kutokana na soko huria, wafanyabiashara wengi wanasafiri kwenda nchi mbalimbali duniani kufungasha bidhaa. Kila mmoja anakuwa na uwezo wake kimtaji, wapo watakaoleta bidhaa duni, wengine bora na hata wengine bandia, wote wanaziingiza nchini.

Bidhaa hizo zikifika nchini wapo wafanyabiashara wa ndani wanaonunua kwa wauza bidhaa za jumla kutoka nje. Wengi hawajui bidhaa ipi ni halali na ipi ni bandia, kiasi kuwa ukipita msako huko mitaani kama FCC inavyofanya mara kwa mara, wapo wafanyabiashara wanaofunga maduka kukwepa kukamatwa kwa bidhaa zao kwa sababu ya hofu kwani hata wenyewe hawajui hadhi ya bidhaa zao kama ni halisi au bandia.

Chanzo chetu kilisema kuwa katika mazingira hayo, maduka mengi yakifungwa kwa sababu ya operesheni ya bidhaa feki, iwe ni Dar es Salaam kama eneo maarufu la soko la Kimataifa la Kariakoo, au hata kwenye miji mingine mikubwa nchini, makusanyo ya TRA kwa siku hiyo yanaporomoka na kuibua malalamiko kutoka TRA kuwa wanakwamishwa kukusanya mapato.

Hata hivyo, kulingana na sheria ya FCC namba 8 ya mwaka 2003 kabla ya kufanyiwa marekebisho makubwa mwaka jana, 2024, ulazima wa kuwako kwa mlalamikaji mwenye bidhaa yake halisi iliyoghushiwa na ziliko hizo bidhaa feki, ilikuwa ni mojawapo ya changamoto ya mamlaka hiyo kudhibiti bidhaa hizo nchini. Mabadiliko ya sheria ya FCC ya mwaka 2024 yamepanua mamlaka na wigo wa kufanya kazi katika udhibiti wa bidhaa feki na vitendo vinavyokwaza ushindani wa haki wa kibiashara nchini.

Makubaliano baina ya mahasimu

Hata hivyo, katika sura nyingine inayoleta changamoto kubwa ya udhibiti wa bidhaa bandia ni pale mlalamikaji mwenye haki ya bidhaa halali anapokubaliana na aliyeingiza bidhaa ambazo hazina kibali chake au bandia kwa kulipana gharama za kibiashara.

Miongoni mwa matukio ya kuelewana wenye bidhaa halisi na wale walioingiza bidhaa bila ridhaa ya mwenye nembo yake, ni tukio la miaka ya hivi karibuni lililotikisa nchini la jezi za klabu za Simba, Yanga, Azam na Taifa Stars. Taarifa zinasema kwamba ingawa FCC walihusika katika kamatakamata hiyo, baadaye wenye mzigo kwanza walilipa kodi TRA na kisha kuelewana na wenye nembo zao (Yanga, Simba na Taifa Stars). Ni Azam pekee walikataa kuingia makubaliano hivyo jezi hizo zikateketezwa.

FCC wamekuwa wakiteketeza bidhaa nyingi feki zinazokamatwa mitaani, lakini kasi na mawanda ya kuzagaa kwa bidhaa bandia ni kubwa mno kiasi kwamba nguvu na juhudi za FCC ni sawa na tone la maji ya sukari kubadili ladha ya maji ya bahari.

FCC imegawa bidhaa nchini katika makundi makuu manne, bidhaa jamii ya nguo na viatu; vifaa vya ujenzi; vifaa vya kieletroniki na bidhaa za anasa (luxurious). Ingawa FCC hawakuweza kutoa takwimu kamili kwa kila kundi juu ya kuzagaa kwa bidhaa hizo, hakuna lenye unafuu.

Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa bidhaa bandia zozote ambazo haziangukii kwenye vyakula zina uwezekano mkubwa sana wa kufumbiwa macho kuendelea kuuzwa nchini hata kama inajulikana wazi kwamba ni bandia na hata viwango vyake vya ubora ni vya chini mno.

Hali hii ya ubora duni ni mkubwa kwa bidhaa kama vipuri vya magari – break pads na discs, bush, shock-absorber, filter nk; nguo- mashati, soksi, magauni, vitenge, kanga, suruali za aina zote, mashuka, vitambaa nk; viatu vya aina zote;  vifaa vya ujenzi kama mabomba na viunganishi vyake, mabati nk; vifaa vya umeme kama nyaya, taa za umeme, viyoyozi, vifaa vya nyumbani vya kieletroniki kama majokofu, feni, blenders, birika, runinga, pasi, hita na kila kifaa kitumiacho umeme kinachotumika majumbani.

Kwa takribani mwezi mmoja sasa FCC wamekuwa wakitupiga danadana kujibu maswali tuliyowapelekea kuhusu janga la bidhaa bandia nchini, ambayo pia yalilenga kupata taarifa za kitakwimu jinsi ukubwa wa tatizo lilivyo kwa sasa.

Wakati FCC wakipambana na hali hii, TBS ambao kimsingi wanashughulika na udhibiti wa bidhaa za elektroniki, chakula, vifaa vya umeme, magari yanayoingia kutoka nje ya nchi na vifaa vya ujenzi nao wanakabiliwa na kibarua kikubwa katika udhibiti ubora wa bidhaa hizo.

TBS wanasema kuwa wanafanya ukaguzi na upimaji wa bidhaa mbali mbali ikiwemo bidhaa kama za chakula, za ujenzi na za kielekroniki kwa lengo la kuhakikisha kama zinakidhi matakwa ya kiwango husika kabla ya kuingia katika soko. Kwa mfano, mwaka wa fedha wa 2022/23 mpaka Aprili 2024, walifanikiwa kuondoa sokoni bidhaa mbalimbali ambazo zilibainika kuwa chini ya kiwango kiasi Kg 10,139,189 (Tani 10,139.19) zenye thamani ya Sh. 12,718,367,100 (Bilioni 12.718).

Katika majibu ya maswali yetu tuliyowapelekea kwa maandishi nao wakajibu kwa maandishi, TBS wanasema kuwa wana utaratibu wa kufanya kaguzi za mara kwa mara na za kushtukiza katika soko. Hali hiyo ni sehemu ya kuhakiki kama bidhaa zilizoko sokoni zinakidhi matakwa ya viwango husika. Aidha, wanasema kuwa hakuna eneo lililothibitishwa kuwa na idadi kubwa ya bidhaa zisizo na ubora.

Wakati TBS wakitoa utetezi huo, ni jambo lililodhahiri kwamba bidhaa za jamii ya nguo zinazouzwa katika masoko ya ndani ni za kiwango duni sana. Kwa mfano, ukichukulia jezi za timu kubwa za soka hapa nchini na hata huko nje, bei yake inadhihirisha wazi kwamba ni za kiwango cha chini.

Kwa mfano, jezi halisi ya timu kubwa za soka za Ulaya kama Arsenal, Manchester United, Barcelona na Real Madrid ni zaidi ya Dola za Marekani 100 kwa t-shirt tu, wakati jezi hizo hapa nchini zinauzwa kati ya Sh. 28,000 mpaka 35,000/- tu.

Tofauti ya kimsingi inayojidhirisha ni ubora wa jezi hizo, zilizozagaa mitaani nchini, ikifuliwa mara chache tu, inachuja rangi na maandishi yake kubanduka. Aidha jezi za klabu kubwa za Yanga, Simba na Azam, kwa wale mawakala waliopitishwa na klabu hizo kuuza jezi zao bei yake inaanzia Sh. 35,000 hadi 70,000/- kulingana na klabu, lakini pia zipo zinazouzwa kwa bei ya kati ya Sh. 15,000 hadi 20,000/- lakini nazo ni ‘tiamajitiamaji’.

TBS haikutaka kujibu kwa undani swali letu juu ya idadi ya watu waliokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwa kujihusisha na biashara (kuingiza nchini, kusambaza au kuuza) bidhaa zisizo na ubora. Na pia walichukua hatua gani za kisheria dhidi ya watu hao? Pia adhabu gani hutolewa kwa wale wanaopatikana na makosa hayo? Mbali tu ya kueleza kuwa kupitia kaguzi mbalimbali zinazofanyika mara kwa mara katika masoko, viwandani na vituo vya forodha walibaini baadhi ya wafanyabiashara wakiwa na bidhaa zisizo na ubora. Hakuna takwimu zilizotolewa.

Aidha, TBS wanasema wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Sura 130 na Kanuni zake ambayo inahusisha kuondoa bidhaa duni katika soko, kuziteketeza kwa gharama za mkosaji, kurudisha nchi zinapotoka kwa gharama za mkosaji, kuwatoza faini na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Kanuni za mwaka 2021 za TBS kanuni ya 15 juu ya adhabu ya jumla: “Mtu atakayefanya kosa chini ya kanuni hizi, lakini adhabu maalum hazijaelezwa, atakuwa amefanya kosa na akipatikana na hatia atahukumiwa kulipa faini isiyopungua Sh. milioni tano na isiyozidi Sh. milioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano au vyote viwili.”

TBS wanasema ili kudhibiti bidhaa hatarishi kuingia katika soko, wanafanya udhibiti wa usalama na ubora wa bidhaa mbali mbali, viwandani, katika soko na kwenye vituo vya forodha. Hatua hizo ni pamoja na kutumia mifumo ya udhibiti inayohusisha ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara, tathmini ya viambato, taarifa za lebo na vifungashio na usajili wa bidhaa (registration).

Vile vile, bidhaa zinazoingia nchini hukaguliwa na kuhakikiwa ubora na usalama wake kabla ya kuruhusiwa kuingia na kutumika hapa nchini. Pamoja na kufanya ukaguzi viwandani na mipakani. Pia wana utaratibu wa kufanya ukaguzi mara kwa mara katika soko na kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kuhakikisha bidhaa zilizopo sokoni hazileti madhara kwa mazingira na afya ya mlaji.

TBS wanaeleza kuwa kwa kutumia mfumo wa alama ya ubora wamepata mafanikio makubwa kudhibiti ubora wa bidhaa, kwani kupitia mfumo huo bidhaa hufanyiwa uchunguzi zaidi ya mara nne kwa mwaka katika soko, hivyo kurahisisha katika ufuatiliaji wa bidhaa ambazo zinakidhi matakwa katika soko.

Tathmini ya TBS inaonyesha kuwa kiwango cha bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi hasa kwa bidhaa za chakula na vipodozi kimepungua. Hali hiyo inathibitishwa kwa idadi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zilizopo kwenye maduka makubwa (supermarket). Kwa maana hiyo, TBS wanasema kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini zina ubora na unaoshindana sawa na bidhaa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo, TBS wanakiri kukabiliwa na changamoto katika kudhibiti ubora wa bidhaa kutokana na uwepo wa mipaka isiyo rasmi; uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanazalisha/wanaingiza kupitia mipaka isiyo rasmi au njia za panya bidhaa ambazo hazijakidhi viwango. Pia uelewa duni kwa wazalishaji, waagizaji, wasambazaji na watumiaji kuhusu masuala ya ubora, usalama na viwango.

Dawa, vinywaji nako hali mbaya

Utafiti wetu unathibitisha kuwa katika eneo la dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na vinywaji nako hakuko salama kwani Watanzania wameendelea kuuziwa dawa, vifaa tiba na vinywaji visivyo na ubora au bandia.

TMDA inathibitisha hili kupitia ripoti yake ya mwaka 2022/23 ikibainisha kuwa katika kipindi hicho jumla ya tani 191.7 za dawa za binadamu na vifaa tiba vyenye thamani ya jumla ya Sh. 713,041,353.64 visivyo na ubora ziligunduliwa na kuondolewa sokoni.

Kwa upane mwingine, mmoja wa wauzaji wa jumla wa vinywaji amesema kuwa ukiacha bia zinazotengenezwa nchini, aina nyingine ya vilevi, hasa pombe kali zilizopo sokoni, nyingi ni bandia.

“Huku kwenye vinywaji hali ni mbaya sana hasa kwenye pombe kali kwa sababu ni rahisi sana kuzitengeneza. Kwa kiasi kikubwa pombe kali zinazouzwa mitaani, zikiwemo pombe maarufu zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazoagizwa kutoka nje, hasa zile zenye ujazo mdogo, ni bandia,” anasema.

Anabainisha kuwa baadhi ya vinywaji hivyo bandia vingi hutengenezwa katika viwanda bubu vilivyo mitaani katika makazi ya watu, kisha kuingizwa sokoni kinyemela kupitia maajenti wadogo wanaojihusisha na uuzaji wa jumla wa vilevi.

Anasema shughuli hiyo hufanywa na mtandao wa wahalifu ambao ‘wana nguvu sana’ kiasi kuwa ni vigumu kuwadhibiti.

TCRA CCC yatahadharisha

Kwa upande wake, Baraza la Ushauri wa Kuwalinda watumiaji wa bidhaa za Kielektroniki lililo chini ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA-CCC) limewatahadharisha watumiaji wa vifaa vya kielektroniki kuwa makini wanaponunua vifaa hivyo, wavikague kwa makini na kupatiwa risiti na kadi ya waranti wanaponunua.

Katibu Mtendaji wa TCRA-CCC, Mary Msuya amesema kuwa iwapo wateja watakuwa makini kwenye ununuzi wa bidhaa, basi upo uwezekano mkubwa wa bidhaa bandia na zisizo na ubora zikaondoka sokoni.

“Kama wateja wakianza kununua bidhaa halisi na zenye ubora pekee na kukataa bidhaa bandia hakuna mfanyabiashara ambaye ataleta au kutengeneza bidhaa hizo kwa sababu hatakuwa na soko. Tatizo ni kuwa bidhaa hizo bandia na zisizo na ubora huuzwa kwa bei ya chini na hivyo kuwavutia watu,” anasema Msuya.

Akisitiza umuhimu wa watumiaji bidhaa kushiriki kwenye vita ya bidhaa bandia na zisizo na ubora, Msuya anasema kuwa bidhaa hizo haziwaathiri tu wateja wanaozinunua na kuzitumia bali pia huua uchumi wa nchi kwani nyingi huingizwa nchini kupitia njia za panya hivyo kuikosesha serikali mapato.

“Pia bidhaa hizi ni chanzo cha wafanyabiashara wa bidhaa halali kufilisika kwani wanakosa wateja sokoni, wateja ambao hukimbilia bidhaa bandia kwa sababu zinazuzwa kwa bei ya chini,” anasisitiza.

Hali ya bidhaa feki duniani ni janga kubwa kama ambavyo kampuni ya kulinda nembo za kibiashara ya Corsearch imethibitisha. Ilibaini kwamba biashara ya dunia ya bidhaa feki kwa mwaka 2023 ilifikia thamani ya Dola za Marekani trilioni 1.1 sawa na asilimia 3.3 ya biashara yote duniani kwa mwaka 2023. Aidha, biashara hiyo ilisababisha watu milioni 5.4 kupoteza kazi.

Corsearch wanaonya kuwa kama hali ya bidhaa feki duniani haitadhibitiwa vilivyo, madhara yake yatazidi kuongezeka zaidi na kufanya pato linalotokana na shughuli hizo kufikia Dola za Marekani trilioni 1.79 ifikapo mwaka 2030, likiwa ni ongezeko la asilimia 75 ya hali ilivyokuwa mwaka 2023.

spot_img

Latest articles

Baraza la saba la Wafanyakazi Wizara ya Nishati lakutana Dodoma

📌 Dkt. Kazungu asema Wizara itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Kimkakati 📌 Baraza lapitisha rasimu...

Wizara ya Nishati yataja mafanikio utekelezaji majukumu 2024/25

📌 Uzalishaji umeme waongezeka kwa asilimia 59.9 📌 Misheni 300 kuongeza upatikanaji umeme...

Gavana Tutuba: Hali ya uchumi wa Tanzania inaendelea kuimarika

Na Tatu Mohamed GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa, hali...

Dkt. Biteko: Ufundi Stadi umepewa kipaumbele na serikali

📌 Asisitiza kuwa, Rais Samia anajenga vyuo kila wilaya nchini 📌 Apongeza utoaji wa mafunzo...

More like this

Baraza la saba la Wafanyakazi Wizara ya Nishati lakutana Dodoma

📌 Dkt. Kazungu asema Wizara itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Kimkakati 📌 Baraza lapitisha rasimu...

Wizara ya Nishati yataja mafanikio utekelezaji majukumu 2024/25

📌 Uzalishaji umeme waongezeka kwa asilimia 59.9 📌 Misheni 300 kuongeza upatikanaji umeme...

Gavana Tutuba: Hali ya uchumi wa Tanzania inaendelea kuimarika

Na Tatu Mohamed GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa, hali...