Madini ya Tanzanite kuuzwa kwenye masoko ya ndani, nje ya Mirerani

📍Ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Chumvi Nangurukuru – Kilwa Waendelea

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa katika kuimarisha thamani ya madini ya Tanzanite, Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2019 ili kuwezesha biashara ya madini hayo kufanyika katika masoko mengine ya ndani, nje ya Mirerani kwa utaratibu maalum ikiwemo kwenye Masoko ya Madini kama ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na Zanzibar.

Amesema hayo, leo Februari 10, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alieyetaka kujua ni lini Serikali itaruhusu kuuzwa kwa Madini ya Tanzanite kwenye Masoko ya Madini ya ndani kama Arusha, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na Zanzibar,

Katika majibu yake, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, kwa kuzingatia umuhimu wa biashara ya madini ya Tanzanite katika maeneo mbalimbali nchini, Mwaka 2024 Wizara ya Madini ilifanya marekebisho ya Kanuni ya 22 ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2019 ambapo kwa sasa umewekwa utaratibu bora zaidi wa biashara ya madini ya Tanzanite kupitia kituo cha uuzwaji wa pamoja wa madini ya tanzanite (Tanzanite Exchange Centre – TEC).

”Mhe. Spika, Utaratibu huo unatoa nafasi ya kufanya biashara ya Tanzanite nje ya Mirerani kwa utaratibu ufuatao, kwanza ni Biashara ya Tanzanite ghafi (rough tanzanite) itaruhusiwa kufanyika nje ya Mirerani endapo mmiliki wa madini husika atakuwa na leseni kubwa ya ukataji wa Madini (large lapidary licence); na pili biashara ya tanzanite iliyokatwa na kung’arishwa (cut and polished) itaruhusiwa kufanyika nje ya Mirerani endapo mhusika wa madini husika atakuwa na leseni yeyote ya biashara au ukataji wa madini,” amesema.

Dkt. Kiruswa amebainisha kuwa, katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara imepanga kufanya minada na maonesho ya madini ya vito ikiwemo Tanzanite katika maeneo ya Arusha, Mirerani, Mahenge, Dar es Salaam na Zanzibar. Tayari mnada wa kwanza wa madini ya vito umefanyika Desemba 14, 2024 huko Mirerani mkoani Manyara.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa Kiwanda cha kusafisha chumvi (Salt Refinery Plant) katika eneo la Lingaula, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi kwa kutambua umuhimu wa kutatua changamoto ya wazalishaji wa chumvi hususani Mikoa ya Kusini.

Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Mohamed Kassinge aliyetaka kujua, Serikali imefikia hatua gani katika mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha chumvi eneo la Nangurukuru – Kilwa.

Akielezea maendeleo ya Mradi huo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, eneo la Mradi huo, limekwisha pimwa, hati ya umiliki imepatikana, na tayari imekabidhiwa kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

“Mhe. Spika, STAMICO imenunua mtambo wa kusafisha chumvi kwa ajili ya mradi huo ambao awamu ya kwanza ya mtambo imewasili nchini na taratibu za kutoa bandarini na kusafirisha kwenda eneo la mradi zinaendelea. Aidha, shughuli za ujenzi wa jengo utakaposimikwa mtambo huo zinaendelea. Ujenzi wa mtambo huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025.”

Hatua hizo zinaonesha juhudi za Serikali katika kuboresha Sekta ya Madini na kuongeza thamani ya rasilimali za taifa kwa kukuza biashara ya Tanzanite na kuongeza uzalishaji wa chumvi nchini.

spot_img

Latest articles

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

Gari, Pikipiki, dhahabu, simu janja zaongeza msisimko katika mnada wa Piku

Na Mwandishi Wetu JUKWAA la kidigitali la PIKU linalojulikana kwa kuendesha minada ya kipekee...

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...

More like this

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

Gari, Pikipiki, dhahabu, simu janja zaongeza msisimko katika mnada wa Piku

Na Mwandishi Wetu JUKWAA la kidigitali la PIKU linalojulikana kwa kuendesha minada ya kipekee...