DC Bariadi akemea vitendo vya kuchungia mifugo ndani ya Hifadhi

Na Mwandishi wetu, Bariadi

MKUU wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga amekemea vitendo vya baadhi ya wafugaji wilayani humo kuchungia mifugo ndani ya Hifadhi hususani Pori la Akiba Maswa huku akisisitiza kuwa wilaya hiyo sio sehemu salama kwa watu wanaofanya ujangili na wanaovunja sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi.

Akizungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari wilayani humo, Simalenga amesema vitendo hivyo vimekuwa vikileta athari kubwa kwa mazingira ya hifadhi, na pia kuhatarisha usalama wa wafugaji wanaoingia ndani ya hifadhi dhidi ya wanyamapori wakali pamoja na kuharibu mfumo ikolojia wa maeneo hayo.

“Niwasihi sana wananchi wote walio ndani ya wilaya ya Bariadi, maeneo ya Pori la Akiba Maswa, maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti Kwa kipande kinachoingia wilaya ya Bariadi Kata ya matongo sio maeneo ya kwenda kuchunga mifugo wala haifai kwenda kuingiza mifugo kwenye hayo maeneo” amesema Simalenga.

Katika hatua nyingine, Afisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Beatus Maganja akiongea na wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani humo wakati wa programu ya utoaji elimu amebainisha athari mbalimbali zinazoweza kusababishwa na vitendo vya kuchungia mifugo ndani ya hifadhi kuwa ni pamoja na ushindani wa malisho unaotokana na mwingiliano kati ya wanyamapori na wanyama wafugwao ambao unaweza kupelekea wanyamapori kupoteza maeneo yao ya asili ya kulisha au maji.

Maganja amebainisha kuwa wanyamapori wanapohisi tishio la upungufu wa malisho yao ya asili wakati mwingine huhama katika maeneo hayo na kuelekea maeneo mengine ikiwemo makazi ya watu na hivyo kupelekea migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Naye CI Lusato Masinde Afisa Uelimishaji kutoka Kanda ya ziwa ya TAWA amesema katika kuhakikisha usalama wa wananchi wa vijiji 32 vinavyozunguka hifadhi hiyo TAWA kupitia Pori la Akiba Maswa wamekuwa wakitoa elimu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi hao ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 mpaka Januari 2025 wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya elfu arobaini na tano (45,000) wakiwemo wanafunzi wa shule mbalimbali.

Aidha, Masinde amesema TAWA imekuwa ikiwadhibiti wanyamapori hao kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo mabomu baridi waliyopokea kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na hivyo matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu yameendelea kupungua siku hadi hadi siku.

Wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani Bariadi wamepongeza jitihada zinazofanywa na TAWA katika kuwaelimisha masuala mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo athari za kuchungia mifugo ndani ya hifadhi na kukiri kuachana na shughuli hizo kwani zimechangia kupata umasikini hasa pale wanapolazimika kulipia faini mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi.

“Mimi nilikuwa na ng’ombe 30 ambazo nilikuwa nazichungia ndani ya hifadhi ya Maswa, nikakamatwa na kulazimika kuuza ng’ombe 5 ili kulipa faini kuwakomboa ng’ombe waliobaki nikabaki na 25, kwahiyo niliwapoteza ng’ombe watano Kwa ajili ya kuchungia hifadhini” amesema Ngomanzito Lenhya Mkazi wa Kijiji cha Halawa na kuongeza:

“Tangu siku hiyo sitaki tena kuchungia hifadhini bora nitunze ng’ombe wangu 25 hao angalau na nyumba nijenge familia yangu ilale pazuri,”.

spot_img

Latest articles

Hatuna pa kujificha, tuwajibike tu yaishe

TAIFA la Tanzania ni nchi huru iliyojitawala kwa takribani miaka 65 sasa, tangu bendera...

MD TWANGE ATOA RAI KWA MAMENEJA TANESCO KUONGEZA KASI YA KUPAMBANA NA WIZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME

📌Afungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, Dodoma 📌Asisitiza umuhimu wa...

Yanga yakomaa kileleni, Simba yavizia ikitafuna  miwa Morogoro

Na Mwandishi Wetu WANANCHI Yanga wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu...

WIZARA YA NISHATI YAENDELEA KUTUMIA NISHATI SAFI EXPO KUTOA ELIMU KWA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Nishati inaendelea kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia...

More like this

Hatuna pa kujificha, tuwajibike tu yaishe

TAIFA la Tanzania ni nchi huru iliyojitawala kwa takribani miaka 65 sasa, tangu bendera...

MD TWANGE ATOA RAI KWA MAMENEJA TANESCO KUONGEZA KASI YA KUPAMBANA NA WIZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME

📌Afungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, Dodoma 📌Asisitiza umuhimu wa...

Yanga yakomaa kileleni, Simba yavizia ikitafuna  miwa Morogoro

Na Mwandishi Wetu WANANCHI Yanga wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu...