KWA miaka mingi sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa na utaratibu ambao unajulikana wazi kwamba katika mikutano yake mikuu ni nini kinakwenda kutokea. Katika mkutano mkuu maalum wa CCM uliofanyika Dodoma kati ya Januari 18 -19, 2025 ulikuwa na ajenda kuu tatu; mosi, kujaza nafasi ya makamu mwenyekiti wa CCM Bara; pili, kupokea taarifa ya kazi za chama kuanzia mwaka 2022 hadi 2025; tatu, kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Kwa utamaduni wa CCM, ilijulikana kwamba wajumbe wa mkutano mkuu maalum wanakwenda kutekeleza majukumu yao juu ya ajenda hizo tatu. Hata wale watu wanaoaminiwa kuwa ni wajuzi wa kunusa na kudukua mambo ya ndani ya CCM, hawakuweza kuibua habari yoyote kwamba kutakuwa na ajenda nyingine yoyote kubwa ndani ya mkutano mkuu wa CCM itakayojadiliwa na kuamuliwa.
Kama ilivyotarajiwa, mkutano ulianza na ajenda ziliwasilishwa, zikajadiliwa na mwisho wajumbe wakawa wamemaliza kazi yao. Wakati mkutano ukiwa unaendelea siku ya kwanza, yaani Januari 18, 2025, ikaanza kusikika minong’ono kwamba ‘kwa nini tusimalize kila kitu katika mkutano huu?’ Kumaliza kila kitu ulikuwa ni ujumbe wa kutaka kumpitisha mgombea urais wa CCM kwa mwaka 2025.
Kwa wale wanaokifahamu Chama Cha Mapinduzi waliamini kabisa kwamba kiutaratibu minong’ono hiyo ya tumalize kila kitu isingeliwezekana. Sababu kubwa ya kutokuwezekana ni kwamba mchakato wa kutafuta mgombea urais kupitia CCM ni shughuli kubwa, ni shughuli pevu na maandalizi yake huwa ya wazi. Wajumbe hupata taarifa mapema juu ya mkutano wa kumchagua mgombea urais kupitia chama hicho.
Hata hivyo, mwaka huu utamaduni wa CCM umebadilika. Kisa na sababu za kubadilika kwa utaratibu mpaka sasa ni hisia tu. Kwamba ni nini hasa kilisukuma hoja za baadhi ya wajumbe kama Livingstone Lusinde (Kibajaji), Adam Kimbisa na Ng’wasi Kamani kuibuka ghafla ukumbini na kupendekeza mkutano mkuu maalum kuwa uwapitishe wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Zanzibar, bado ni utabiri tu.
Kwa kitambo sasa kumekuwa na hoja zinazosukumwa ndani ya CCM kwamba, mgombea urais wao huchaguliwa na mkutano mkuu wa chama, lakini baada kupitia mchakato wa kuchukuwa fomu, kupitishwa na Kamati Kuu, kisha Halmashauri Kuu ya CCM ambako kote kura ndizo huamua miongoni mwa wagombea waliojitokeza. Kwa maana hiyo, kwamba Rais aliyeko madarakani anakuwa amechaguliwa na wanachama katika vikao halali vya chama, katika mazingira hayo, Rais aliyetokana na CCM akishatumikia muhula wa kwanza madarakani anakuwa na haki ya kupitishwa bila kupingwa kuwania kipindi cha pili.
Sasa katika mazingira ya sasa, Rais Samia Suluhu Hassan anamaliza kipindi chake cha kwanza kama Rais mwishoni mwa mwaka huu wa 2025. Rais Samia aliingia madarakani kurithi kiti cha urais baada ya kifo cha Rais John Magufuli Machi 2021. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya “40 (4) Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu.” Sharti hili ndilo linampa Rais Samia sifa ya kuwania urais mwaka huu, kwani ametumikia kiti hicho kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu, na kwa maana hiyo ana haki ya kuomba kipindi cha pili.
Tetesi zinasema kwamba wapo ‘wahafidhina’ waliojipanga kwa nguvu zote wakisukuma hoja, kwamba ni kweli Rais SSH ana sifa na haki ya kuwania urais mwaka 2025, lakini ni lazima apitie kwenye mchakato wa kuchukua fomu, ashindanishwe na wanachama wengine, ili awashinde. Wanaosukuma hoja hiyo wanadaiwa kujenga ushawishi wao kwenye ‘dhana’ kwamba Rais SSH hajawahi kushindana au kushindanishwa ndani ya chama, hivyo ni haki yake kuwania kiti hicho, lakini kwa kushindana na wengine. Dhana hii ilikuwa inapingana na ile ya kutolewa kwa fomu moja tu ya mwanachama wa CCM atakayeomba urais mwaka 2025.
Hoja hiyo pia ilikuwa inatiliwa nguvu na ushawishi mwingine kuwa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM ndiyo mchakato pia wa kumpata mwenyekiti wa taifa wa chama hicho. Hoja hiyo inajengwa kwenye msingi kwamba siyo utamaduni wa kiti cha mwanyekiti wa CCM kugombewa na mtu zaidi ya mmoja. Umekuwa ni utamaduni wa CCM miaka yote nafasi ya mwenyekiti wa CCM jina lake kupendekezwa na vikao vya juu vya CCM, Kamati Kuu na kisha Halmashauri Kuu. Mkutano mkuu hupiga kura ya ndiyo na hapana. Huu ni utaratibu wa miaka yote. Utaratibu huu unasimamiwa na watoa hoja ya Rais SSH kuingia kwenye mchakato wa kuomba kuteuliwa na chama hicho kwa kushindana na wenzake, ili kupata kile wanachodai ‘uhalali.’
Ingawa hoja za kundi hili ndani ya CCM ilionekana ya ovyo, katika siku za hivi karibuni inadaiwa kuwa kulikuwa na msukumo mkubwa zaidi wa kutaka hilo litokee. Wapo wanaodai kuwa kuna watu walikuwa wamejipanga kwa nguvu kubwa ya fedha, kwamba wakati sasa ukifika wa ratiba ya kutafuta wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na mwishowe urais, wasukume kwa nguvu zote msimamo huo kwamba nafasi ya kupata mgombea urais mwaka huu uwe wa ushindani ndani ya chama kana kwamba ndiyo kwanza Rais SSH anatafuta nafasi hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika mazingira ya namna hiyo, wajuzi wa siasa za CCM wakajua kinachotengenezwa, wakajua na kiwango cha fedha kilichotengwa na ambacho kinaendelea kutengwa ili kufanikisha mkakati huo. Watetezi wa uwanja huru na wazi kuwania urais wangali wakiangalia mbele kwamba mkutano mkuu wa CCM ujao ndiyo utakaoamua kuhusu mgombea urais, juzi Jumapili Januari 19, 2025 wakapigwa ‘shoti ya umeme mkubwa’.
Hakuwa mwingine bali Rais mstaafu na mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete aliyetoboa meli ya ‘wataka uwanja wazi wa kutafuta kura ya kuwania urais CCM’ kwa kuwakumbusha wajumbe wa mkutano mkuu maalum kwamba wanayo mamlaka ya kikatiba kuteua mgombea urais kupitia chama hicho kwa mujibu wa ibara ya 101 (5) (b). Kikwete baada ya kutoa kauli hiyo, aliwataka wajumbe wapitishe azimio la kufanya hivyo. Pendekezo hilo liliilazimu Halmashauri Kuu ya CCM kukaa kwa dharura na kisha kuja na azimio ambalo lilipendekeza kupitishwa kwa Rais SSH kwa nafasi hiyo mwaka huu, na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi naye kuwania nafasi hiyo, upande wa Zanzibar. Kura zote za wajumbe 1,924 zilisema ndiyo, Rais SSH ndiye mgombea urais kupitia CCM mwaka 2025. Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa CCM akapitishwa kuwa mgombea mweza wa Rais SSH.
Katika kufikiwa kwa maamuzi hayo, ni vigumu kuamini kwamba eti ajenda ya ‘‘kwa nini tusimalize kila kitu katika mkutano huu?’ ilianzia Dodoma kati ya Januari 18 na 19, 2025 wakati wa mkutano mkuu maalum. Kwa jinsi ilivyowasilishwa, ikajadiliwa na kuamuliwa, ni hakika ilikuwa ni ajenda kuu kuliko hata ya kufikiri ni nani angelikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, nafasi ambayo mkongwe Stephen Wassira ameichukua. Ni mkakati uliopangwa kwa ustadi mkubwa, kwa mbinu kubwa za kutokutoa siri na mwishowe kuwaacha njia panda wasukuma hoja kwamba nafasi ya kuwania urais kupitia CCM mwaka huu ingelikuwa wazi kwa kila mwanachama mwenye kutaka nafasi hiyo. Hili ni pigo kubwa la kisiasa kwa baadhi ya watu.
Ni pigo kwa sababu mkakati huo ulionekana kama uasi, ulionekana ukisukumwa na baadhi ya watu ‘waliotofautiana’ na waliokalia viti kwa sasa. Kazi ngumu na kubwa iliyoko mbele ya wafuasi wa hoja hiyo ni hii; je, wanakwenda kubaki salama ndani ya CCM hasa baada ya mbinu zao kujulikana na kushughulikiwa kwa njia ya ‘ambush’? Watasalimika? Wataeleweka na mbaya zaidi wataaminika tena? Maswali yote haya yanahitaji muda kupata majawabu yake. Kwa sasa itoshe kusema tu CCM imefanya mapinduzi Dodoma.