LEO ni siku ya pili katika mwaka mpya wa 2025. Ninawatakia wasomaji wa safu hii kheria ya mwaka mpya wa 2025. Ni maombi yangu kwamba tutaendelea kukutana kwenye safu hii kila wiki kuchambua mambo makubwa ya kitaifa kwa nia ya kukuza na kusukuma mbele moto wa utawala bora na uwajibikaji katika taifa letu.
Wiki iliyopita katika safu hii nilieleza mambo mbalimbali ya maana na ovyo yaliyotawala mwaka 2024 ambao tuliupa kisogo juzi. Kikubwa ni changamoto ambazo zilishuhudiwa katika chaguzi za nchi mbalimbali duniani. Tuliona jinsi sanduku la kura lilivyowatia adabu watawala huko Japan chama tawala kikipoteza wabunge wengi; tukaona pia jinsi takribani muongo mmoja na ushei wa utawala wa chama cha kihafidhina nchini Uingereza, Conservative, kilivyopoteza mvuto.
Mshangao mkubwa ulikuwa nchini Botswana ambako chama kilicholeta uhuru, Botswana Democratic Party (BDP) kilipoteza madaraka ambayo kimekuwa nayo kwa takribani miongo sita. Kwa majirani wake, Afrika Kusini, Chama tawala ANC nacho kilionjeshwa shubiri kwa kukutana na nguvu ya sanduku la kura kwa kupoteza wingi wa viti bungeni, hivyo kulazimika kuingia katika mfumo wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa kualika vyama vingine kuunda serikali.
Kwa kifupi mwaka 2024 ulikuwa na mafundisho mengi sana katika uwanja wa utawala bora na demokrasia, hasa kwenye sanduku la kura. Kwetu Tanzania, yapo tuliyoshuhudia juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 ulivyoendeshwa. Bado vumbi la uchaguzi huo halijatulia na bado watu wanajiuliza ni nini hasa kilitokea na kwa nini?
Pamoja na hayo, mambo mengine yaliyopamba mwaka 2024 ni matukio ya kutekwa, kupoteza, kuteswa na kuuawa kwa watu mbalimbali nchini. Inawezekana mambo haya ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine, na kwa maana hiyo kuhitaji kushughulikiwa tu kwa mfumo wa kipolisi. Pamoja na hoja hiyo, kuna mahali akili ya kawaida inagoma kukubaliana na dhana kwamba vitendo hivi ni uhalifu kama ulivyo uhalifu wa kawaida tu. Sababu kubwa ni kwamba walengwa wakuu wa vitendo hivi ni wale wenye nasaba na masuala ya kisiasa. Ipo orodha ya takribani watu 80 iliyowekwa hadharani kitambo sasa na Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS), lakini pia orodha hiyo kadri siku zilivyosonga, nayo ilizidi kuongezeka. Walengwa wakiwa ni watu wa aina ile ile. Wenye nasaba au wanaoshiriki shughuli za kisiasa ama kama viongozi wa vyama vya siasa, au kama wanaharakati.
Kinachosumbua katika kadhia hii ya watu kutekwa, kuteswa, kuumizwa na hata kuuawa, ni kukosekana kwa taarifa za kina za uchunguzi za vyombo vyenye dhima ya kulinda uhai wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi, kwamba ni akina nani wako nyuma ya vitendo hivi ambavyo vinalenga kundi mahususi katika jamii? Na je, nani hasa anawatuma watu hawa au wanalindwa na nani?
Mambo haya yanatokea katika taifa letu ambako kuna wizara nzima ya Mambo ya Ndani ambayo ina wajibu wa kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa usalama, amani na uhuru katika nchi yao. Wanafanya shughuli zao halali za kisiasa, kijamii na kiuchumi bila kuhofia kwamba watalengwa na makundi ya kihalifu ambayo kwa kweli yanazidi kuzua taharuki ndani ya jamii.
Zipo taarifa za uhakika kwamba katika mkumbo huu wa kuibuka kwa makundi yanayojiendeshea mambo yake watakavyo, pia wapo wanaotumia mwanya huo kukamata, kutisha, kutesa raia wakiwasingizia tuhuma mbalimbali za kodi kwa nia ya kutaka kujipatia fedha nyingi. Matendo haya kwa hakika ni kama yale ambayo tulipata kuyashuhudia katika pwani ya Somalia miaka ya 2000 hadi 2010 ambako utekaji wa meli kwa ajili ya kudai malipo (ransom) yalikuwa ni matukio ya kawaida. Tunakumbuka tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 2021 alipiga marufuku vikosi kazi na kutaka kila taasisi ya serikali yenye wajibu wa kushughulika na mambo ya kodi na usalama itekeleze wajibu wake kulingana na sheria za kuanzishwa kwake.
Umma uliamini alichosema Rais SSH. Uliona ni kweli kauli yake ilikuwa ni ya kufikisha mwisho makundi na vikosi kazi vilivyokuwa vinatikisa nchi kama yale makundi ya watekaji meli pwani ya Somalia miaka ile ya 2000. Hofu ilitanda nchini. Kwa sasa kuna kila dalili vikosi kazi viko kazini tena. Wapo watu wameumizwa sana na vikosi hivi.
Katika mazingira haya tunapoanza mwaka 2025 yafaa kutafakari kama uwepo wa Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inakuwa na manufaa gani kwa taifa, kama madhila haya bado yapo. Bado wapo watu wenye jeuri ya kuwakamata raia, kuwashikilia kinyume cha sheria kwa miezi na miezi bila kuwaandikisha kokote, bila kuwafungulia mashitaka yoyote huku wakiwatisha, wakiwatesa na kuwataka kulipa malipo ambayo hayana uhalali wowote wa kisheria.
Bado watu waliodaiwa kukamatwa na wanaodaiwa ni askari hawajapatikana. Polisi hawaonyeshi ama kujua waliko au hawataki kabisa kushughulika na matukio hayo ili raia wapate majawabu ya maswali yanayowasumbua kwamba ni akina nani wanaoendesha uhalifu huu dhidi ya jamii. Kwamba je, nchi yetu kidogo kidogo inapoteza sifa yake ya kuwa taifa linaloongozwa na serikali iliyochaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura na inayoogozwa na utawala wa sheria na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi? Kwamba suala la utawala bora linazidi kusiginwa na wenye maslahi yao binafsi, kama wale Wasomali wa pwani ya Somalia miaka ya 2000?
Ni katika kutafakari mambo haya ambayo yalitikisa jamii nchini Tanzania kwa mwaka 2024 ambayo hakika hayajapata suluhu, tunapaswa kujiuliza kama taifa kwamba mwaka mpya wa 2025 unakwenda kuwa mwaka wa namna gani kama shida hizi bado zingalipo? Je, 2025 unakwenda kuwa ni mwaka wenye nafuu katika uga wa utawala bora au ni wa kuzidi kujiimarisha kwa magenge ya utekaji na utesaji?
Inawezekana kwamba madhila haya ambayo yalitamalaki ndani ya jamii mwaka 2024 kwa baadhi ya watu yakadhaniwa ni mambo mepesi. Pia, inawezekana kudhaniwa kwamba wanaokumbwa na madhila haya ni wale wenye ‘mdomo mrefu’ dhidi ya watawala. Kadhalika, hoja inaweza kujengwa kwamba walioko madarakani wako salama kwa kuwa wanaotaabika sasa ni wale wa upande wa pili.
Kwa vyovyote itakavyochukuliwa, madhila haya ya mwaka 2024 hayawezi kuchukuliwa kwa wepesi kwamba ni adha ya watu fulani. Kama kwa pamoja Watanzania hawatasimama na kukataa na kulaani kuzidi kujengeka kwa utamaduni huu wa ovyo wa kuteka, kutesa, kuumiza, kujeruhi na hata kuuawa, hawaitakii mema nchi yao na hawajengi kesho yao iliyo njema zaidi. Tukumbuke tu ile kuimba Tanzania ni nchi ya amani, siyo kitu kilichoibuka kama uyoga au kushuka kama mana kutoka mbinguni. Ni matokeo ya kazi nzito iliyofanywa na waasisi wa taifa hili, ni kazi ya kupigania haki ya kila raia na usawa wa watu wote mbele ya sheria. Tukiendelea kuendekeza magenge ya wahalifu hata kama yatapewa majina gani kuyahalalisha, hutuitakii mema nchi yetu. Tukatae magenge haya sasa kwa nguvu zetu zote