Nimemsikiliza Gachagua, nikatamani Lowassa 2008 angelipambana vivyo

KWA zaidi ya wiki mbili sasa majirani zetu, Kenya, kumekuwa na siasa za moto. Mzozo unaochemka huko ni wa kutaka kumuondoa madarakani Naibu Rais Geoffrey Rigathi Gachagua. Naibu Rais huyo alimaarufu kama Riggy, anatuhumiwa kwa makosa 11. Miongoni mwake ni uvunjaji wa katiba ya Kenya kwa njia mbalimbali ikiwamo kueneza siasa za ukabila, kuingilia kazi za ukandarasi za serikali ili kujinufaisha binafsi, kumdharau na kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya Kenya, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu hadi kufikia ukwasi wa KSh. bilioni 5.2 kwa miaka miwili pekee na tuhuma nyingine kadhaa.

Kutokana na tuhuma hizo Bunge la Kenya Jumanne wiki iliyopita lilijadili hoja ya kumng’oa madarakani kiongozi huyo namba mbili kwa ukubwa katika taifa hili. Kwa mara ya kwanza hoja hiyo ambayo Riggy amekanusha tuhuma zote, iliwasilishwa bungeni Septemba 26 na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.

Kuwasilishwa bungeni kwa hoja ya kumng’oa Naibu Rais ni kielelezo cha dhahiri cha kufikia tamati kwa ndoa ya kisiasa kati ya Riggy na bosi wake, Rais William Ruto. Ruto na Riggy waliingia madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2022.

Uongozi wa Ruto umekuwa na changamoto nyingi. Kubwa ya yote ni kuweka pamoja muungano wa Kenya Kwanza unaoundwa na vyama zaidi ya 20. Ingawa hakuna mdau wa muungano huo amekuwa na uasi wa kiwango cha Riggy, hatua ya sasa inaongeza maumivu kwenye serikali ya Rais Ruto ambayo tayari imepita katika tanuru la moto ndani ya kipindi kifupi sana cha uongozi wake wa miaka miwili tu.

Itakumbukwa kwamba katikati ya mwaka huu Rais Ruto alikuwa katika kikaango cha moto baada ya wananchi wa Kenya wakiongozwa na waandamanaji vijana almaarufu kama GenZ, wakipinga muswada wa fedha wa mwaka 2024. Hali hiyo ya maandamano ilichochewa na wabunge kupitisha muswada huo ambao wananchi wa Kenya walikuwa wameulalamikia kuwa unakwenda kuongeza machungu juu ya hali ngumu ya maisha ambayo tayari ilikuwa ikiwakabili.

Ni kutokana na sekeseke la Gen Z la kupinga muswada huo walimwagika katika mitaa ya miji mikubwa ya Kenya kama Nairobi, Kisumu, Mombasa, Eldoret kwa maelfu, hatimaye lilimlazimisha Rais Ruto kuacha kuutia saini, ili walau kuutuliza moto wa maandamano uliokuwa unawaka kila kona ya nchi.

Machungu dhidi ya serikali ya Ruto hayakuishia hapo tu, kwani katika kutuliza hasira za Gen Z aliamua kuvunja baraza la mawaziri, huku akiomba wakubali kukutana nao kwa majadiliano. Hatua hizo, kukataa kuridhia muswada wa fedha wa mwaka 2024 na kuvunja baraza la mawaziri, kwa kiasi fulani vilituliza hasira za Gen Z, ingawa hali ya kuaminiana baina ya makundi hayo ya vijana na serikali ya Ruto siyo ya kuwekewa dhamana hadi sasa.

Moto huu unaobabua serikali ya Ruto ulianza kwa maandamano ya Machi mwaka jana ambayo yaliitishwa na Raila Odinga aliyekuwa amegombea urais kwa mwavuli wa Azimio la Umoja One Kenya wakipinga ushindi na serikali ya Rais Ruto.

Mlolongo huu wa matukio dhidi ya serikali ya Ruto unafungua utawala wake katika sura mpya, safari hii mashambulizi yakiwa yametoka kwa mwandani wake. Mashambulizi dhidi ya Ruto na serikali yake ambayo Jumanne wiki hii yaliwafanya wabunge kuamua kumtosa Riggy katika mjadada wa hoja ya kumng’oa madarakani, yanaicha serikali ya Ruto katika safari mpya ya kutafuta kuungwa mkono na wananchi wa Kenya.

Kwa hali ya mjadala ilivyokuwa bungeni na hata baada Riggy kujitetea, ni dhahiri Riggy hatavuka kihunzi siyo cha Bunge tu, bali hata cha Senate. Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya Jumatatu usiku wiki iliyopita, ulikuwa ni mahususi kuivua nguo serikali ya Ruto. Kwa mara ya kwanza Riggy amemwaga hadharani makubaliano baina ya vyama vya siasa vinavyounda Kenya Kwanza, kwamba walipoungana walikuwa wanatafuta nini. Kwamba ulikuwa ni muungano wa nini? Kuwatumikia wananchi au wakubwa kugawana keki miongoni mwao.

Riggy anaondoka na kuna kila dalili bado ngome yake haiko salama kwa kuwa anaweza kuanza kuandamwa na kesi mbalimbali za jinai, ikiwamo ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Bado Riggy hatakuwa huru hata atakapokuwa amekwisha kuvuliwa wadhifa wa Naibu Rais, bado ana vita kubwa mbele yake. Jambo la muhimu la kujiuliza ni hili, je, akishang’oka serikali ya Ruto itakuwa na utulivu? Je, siri za kugawana keki ya Kenya kama ambavyo Riggy mwenyewe alisema ni kama waligawana hisa za kampuni, zinakwenda kuiweka wapi serikali ya Ruto?

Ukisikiliza kwa makini sauti za wabunge kama Naibu Spika Glady Shollei kwamba Riggy amevujisha siri za watu waliounda Kenya Kwanza bila kupata idhini yao, ni kielelezo kwamba makubaliano baina ya umoja wa Kenya Kwanza yalipaswa kuwa siri kubwa miongoni mwa wahusika. Kwamba hata wananchi wa Kenya walioichagua serikali ya Ruto, ambao kwa mujibu wa katiba ya Kenya ndiyo wenye mamlaka ya mwisho ya kuamua nani awe mtawala wao, hawaijui. Huu ni mlango mwingine wa mapambano ambao Riggy ameuacha wazi utakaohitaji nguvu kubwa kuufunga ili wananchi wawe na imani na serikali yao kwamba ipo kwa ajili ya wote na siyo kwa ajili ya maslahi ya kikundi cha watu fulani.

Jumanne jioni wiki iliyopita Riggy alifika mbele ya Bunge, alijijteta kwa ushahidi dhabiti. Alitoa vielelezo vyake kupinga vile vya mtoa hoja, Mwengi Mutuse. Alijibu hoja moja baada ya nyingine, kwa yeyote aliyekuwa anafuatilia mjadala wa Bunge la Kenya katika hoja ya kumng’oa Riggy, alipata fursa ya kujua ukweli. Kujua ukweli wa wanasiasa wanapotaka kushughulikiana. Ni dhahiri, suala la kumng’oa Riggy lina mambo mengi. Mapambano ya kutaka madaraka.

Bunge la Kenya pamoja na mapungufu yoyote ambayo yanaweza kutajwa, limeonyesha kitu kimoja cha umuhimu wa kipekee kwamba lina uwezo wa kufuata katiba ya Jamhuri ya Kenya hata pale linapotaka kunyoa mtu yeyote. Hakuna ubishi kwamba Riggy ameshughulikiwa. Na ni kweli amefikishwa kwenye kona ngumu, amepigana kujitetea. Amejiandaa kuendelea na mapambano.

Ninapomwangalia Riggy ninakumbuka jinsi Bunge la Tanzania lililoongozwa na Spika Samuel Sitta mwaka 2008, lilivyoamua kushughulika na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, juu ya tuhuma za mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond.  Nimetafakari na kujiweka kwenye mzani wa kilichotokea Kenya na kile kilichotokea mwaka 2008, nimejikuta katika himisho kwamba huenda wenzetu wa Kenya wanapiga hatua za haraka zaidi kutumia katiba yao na kujenga demokrasia katika jamii yao.

Tunapotazama nyuma leo, mtu anaweza kusema yawezekana kama Spika Sitta (sasa marehemu) ambaye alikuwa mwanasheria, angejipa muda wa kusoma ripoti ya kamati ya Bunge ya kuchunguza suala la Richmond ambayo iliongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, ni hakika angegundua kwamba haikutimiza matakwa ya haki ya asili (natural justice), hivyo mjadala wa Richmond na Lowassa ungeliweza kutupa fursa ya kupiga hatua za maana zaidi za kidemokrasia.

Wakenya wanakwenda kumuhumu Riggy, iwe wamemuonea au la, wamempa muda wa kusililizwa, Sitta na Mwakyembe wake walifayanya yao mwaka 2008 kumsulubu Lowassa bila kumsikiliza. Kwa bahati mbaya, Ruto amejikalia kimya kana kwamba hajui kinachomkuta Naibu wake, kama vile vile Rais Jakaya Kikwete alivyokaa kimya, kana kwamba alikuwa hajui kilichokuwa kinakwenda kumtokea Lowassa 2008.  Bunge lilipiga kura ambazo wabunge 281 waliridhia kumng’oa madarakani, 44 wakipinga na mmoja akijizuia kuonyesha upande.

Kenya wametupa funzo jingine kubwa Jumanne wiki hii kwamba wanao uwezo wa kuendesha mambo yao kwa kuzingatia sheria na katiba yao. Pamoja na udhaifu wowote unaoweza kutajwa kuhusiana na mchakato wa kumng’oa Riggy, wamepiga hatua kubwa ya kisiasa.

spot_img

Latest articles

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

Urathi wa Mwalimu Nyerere usaidie kukubali kukosolewa

JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki...

Kukataa mgombea binafsi ni kukumbatia utumwa

HISTORIA inashuhudia kwamba wapo watumwa walikataa kuwa huru kwa sababu waliamini kwamba pamoja na...

Zanzibar kuanza uboreshaji Daktari la wapiga kura

Na Mwandishi Wetu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar, unatarajiwa kufanyika...

More like this

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

Urathi wa Mwalimu Nyerere usaidie kukubali kukosolewa

JUMATATU wiki hii Watanzania walikumbuka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki...

Kukataa mgombea binafsi ni kukumbatia utumwa

HISTORIA inashuhudia kwamba wapo watumwa walikataa kuwa huru kwa sababu waliamini kwamba pamoja na...