KWA mtu yeyote anayefuatilia hali ya amani katika nchi za Afrika kwa zaidi ya miongo sita sasa, atathibitisha kwamba ni vigumu kupita wiki bila kusikia habari za mauaji ya raia wasiokuwa na hatia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). DRC au Zaire kama ilivyokuwa inajulikana zama za Rais Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa za Banga, haijawahi kuonja amani, hasa eneo la mashariki la nchi hiyo.
Utawala wa zaidi miongo mitatu wa Rais Mobutu ambaye alifurushwa madarakani na majeshi ya waasi dhidi ya utawala wake wakiongozwa na Laurent Disire Kabila mwaka 1997, bado hakujakuwa na nafuu yoyote ya maana kwa ustawi wa maisha ya watu wa mashariki ya DRC kama ilivyo leo. Mauji, vita vya wenyewe kwa wenyewe na mara nyingi kutumika kwa mamluki, umekuwa ni utambulisho wa nchi hiyo mbele ya jamii ya kimataifa.

Umoja wa mataifa unasema kuwa kiasi cha watu milioni saba wanadaiwa kuyakimbia makazi yao ndani ya DRC eneo la mashariki ambalo limekuwa kitovu cha vita vya vikundi mbalimbali vyenye silaha na majeshi kutoka nchi jirani. Kikundi cha waasi cha MK23 peke yake kinadaiwa kuwa chanzo cha watu milioni moja mashariki mwa nchi hiyo kuyakimbia makazi yao.
Vita vya ndani ya DRC vinaelezwa kusababisha vifo vya watu milioni 5.4 tangu mwaka 1998 hadi sasa, hii maana yake ni kwamba tangu kufurushwa kwa Mobutu mwaka 1997 DRC hajaonja chembe ya amani, hasa eneo la mashariki lenye utajiri wa rasilimali nyingi- madini ya kila aina, misitu minene na wanyama pori. Vifo hivi ni sawa na kusema ni kufuta kabisa katika uso wa dunia moja kati ya nchi 22 za Ulaya ambazo zina idadi ya watu sawa au chini ya milioni 5.4, hizi ni kama Norway milioni 5.47, Ireland milioni 5.0, Croatia milioni 4.0, Moldova milioni 3.4 na nyinginezo. ambazo idadi ya watu wake ni chini ya milioni 5.4.
Wakati damu isiyo na hatia inayomwagwa kila uchao ikiendelea kulia kutoka ardhi ya DRC, nako Sudan kwa sasa hali siyo salama kabisa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji (IOM) hivi karibuni lilitoa taarifa kwamba kiasi cha watu milioni 7.6 wameyakimbia makazi yao ndani ya Sudan tangu Aprili 2023 mpaka sasa mapigano baina mahasimu wawili yaanze nchini katika mjini mkuu wa Khartoum na kusambaa maeneo mengine. Mapigano hayo ni kati ya upande wa Majeshi ya Jeshi la Sudan (SAF) chini ya Jenerali Abdiel Fattah al-Burhan na hasimu wake wa kikosi cha wanamgambo wa msaada wa haraka- Rapid Support Forces (RSF), Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo. Hadi sasa watu 14,600 wanadaiwa kufa katika mapigano hayo, wengi wakiwa ni raia wasio na hatia.
Ukiangalia kwa undani takwimu hizi za watu kuyakimbia makazi yao, ni sawa na kusema takribani nchi 27 za Ulaya zenye wakazi sawa au chini ya milioni 7 wamekimbia wote. Ama ni sawa na kusema kuwa nchi za Afrika kama Libya yenye watu milioni 6.8, Jamhuri ya Congo (Brazzaville) yenye watu milioni 6.1 au Jamhuri ya Afrika ya Kati yenye watu milioni 5.7 na nchi nyingi takribani 17 za Bara la Afrika zenye idadi ya watu chini milioni saba, kukimbiwa na wakazi wake wote. Kwa maneno mengine, tunapotafakari hali hii ya migogoro ya DRC au Sudan, dunia ingetarajiwa kuona nguvu kubwa ikielekezwa kutatua shida za nchi hizi.
Tatatizo kubwa zaidi ni kuona jinsi mataifa ya Afrika yasivyochulia kwa umakini mizozo hii. Kwa mfano, vikosi vingi ama vya mwavuli wa Umoja wa Mataifa au Umoja wa Afrika, au Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivi sasa kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hazionyeshi zikifua dafu kwenye mgogoro wa DRC. Mauaji yanaongezeka kila siku, wananchi wengi zaidi wanayakimbia makazi yao, lakini kibaya zaidi vikundi vya uasi vinazidi kuongezeka nchini humo huku nchi jirani kama Rwanda na Uganda zikitajwa kuhusika na ama kuunda au kusaidia vikundi hivyo.
Rais Yoweri Museveni (78) wa Uganda amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, ni kiongozi wa nne kwa kukaa madarakani kwa muda mrefu zaidi miongoni mwa marais wa Afrika amekalia kiti cha urais kwa miaka 38 sasa. Anayeongoza kwa kukaa muda mrefu zaidi ni wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Mbasogo (80) amakaa ikulu kwa miaka 45; Rais wa Cameroon, Paul Biya (89) amedumu kwa miaka 41; na Rais wa Jamhuri ya Congo, Denis Sassou Nguesso (78) amakaa madarakani kwa miaka 40 sasa. Wakongwe hawa siyo tu hawajawa na msaada wa maana katika kutatua mizozo ya Afrika, bali wanatajwa kuhusika kama ilivyo kwa Museveni.
Wiki iliyopita Paul Kagame alishinda kiti cha urais nchini kwake kwa zaidi asilimia 99. Kagame amekuwako madarakani kama Rais tangu mwaka 2000, hata hivyo kiuhalisia ndiye alikuwa na madaraka akiwa Makamu wa Rais chini ya Rais Pascal Bizimungu, kuanzia mwaka 1994 Rwanda Patriotic Front walipomg’aoa madarakani Rais Juvenal Habyarimana kufuatia kutunguliwa kwa ndege yake na kusababisha kifo chake akiwa na mwenzake wa Burundi, Rais Cyprian Ntaryamira. Hali ya uchunguzi wa amani eneo la mashariki ya DRC unaonyesha kuwa kadri Kagame alivyojichimbia madarakani Rwanda, ndivyo hali inakuwa mbaya zaidi DRC. Hali ya DRC tangu mwaka 1998 imeelezwa kuwa mbaya sana. Watu waliokufa wanadaiwa kuwa ni milini 5.4 tangu 1998 hadi sasa.
Rwanda chini ya Kagame imekuwa ikitajwa wazi kabisa kwamba inahusika ama kwa kupeleka wanajeshi wake moja kwa moja kwenye uwanja wa mapigano mashariki ya DRC au wamekuwa ndiyo walezi na wawezeshi wa kikundi cha M23. Taarifa za hivi karibuni zaidi za Umoja wa Mataifa juu ya mzozo wa DRC, zinaitaja Rwanda kuwa ndiyo inabeba waasi wa M23 ambao wamekuwa na nguvu zaidi katika siku za hivi karibuni katika kuendesha uasi wa kivita na kuteka maeneo mengi zaidi DRC mashariki.
Rwanda kama ilivyo DRC ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini serikali ya Rais Felix Tshekedi imekuwa hamung’unya maneno kwani anamtuhumu Kagame kwa kuchochea shida za DRC kwa kuwaunga mkono waasi. Rwanda imekuwa ikikanusha kuhusika kwake, lakini picha za wachunguzi wa Umoja wa Mataifa zilizopatikana mpakani mwa DRC na Rwanda zinadaiwa kuowaonyeshwa wanajeshi wa Rwanda akivuka mpaka kwenda kwenye mapigano ya moja kwa moja DRC kwa kuwasaidia M23 dhidi ya Jeshi la DRC.
Tunapokuwa na viongozi wa Afrika wa namna hii, tena ambao kwa kweli wamekaa madarakani kwa muda wa kutosha wa kujua kwamba shida za bara hili hazina mjomba wa kuzitatua kama siyo Waafrika wenyewe, lakini wao kwa mlango wa nyuma wanachochea maafa haya, wana sababu gani ya kuongoza watu wa bara hili?
Ukiangalia Ulaya ilivyoungana kuisaida Ukraine dhidi ya Urusi katika vita vyao, unapata picha tofauti kabisa na hali ilivyo miongoni mwa viongozi wa Kiafrika. Huwezi kusikia ndani ya Umoja wa Afrika kwa mfano wakielezana ukweli. Kwamba huwezi kusikia viongozi hawa wakielezana kwa mfano kuwa wao wenyewe ndiwo wahusika wakuu katika vita vya DRC au Sudan. Huwezi kuona wakithubutu kunyooshena kidole, ili kusaidia kurejea kwa amani ama DRC au Sudan. Ni kama vifo vya Waafrika katika nchi hizo haviwahusu. Ni aibu kubwa sana kwa bara la Afrika.