Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan
amemuagiza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi
wa Chakula (NFRA) ianze kununua mahindi kwa wakulima kote nchini kwa bei ya
shilingi 700 kwa kilo, nyongeza kutoka bei ya awali ya shilingi 500 kwa kilo iliyokuwepo
wakati msimu wa ununuzi unaanza.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo Julai 17,2024 wakati akihitimisha ziara yake mkoani Rukwa kwa kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Mandela, Sumbawanga Mjini.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka wananchi wa Rukwa wauze mazao ya kilimo kwa
watu na taasisi ambazo zina vibali halali vya kufanya biashara hiyo kutoka Wizara ya
Kilimo ikiwemo vibali vya kuuza mahindi nje ya nchi.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya uvuvi katika
Ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa meli na kuongeza meli mpya
katika ziwa hilo.
“Serikali imetoa boti nne za kisasa katika Ziwa Rukwa na Tanganyika ili zisaidie kuweka
usalama ndani ya ziwa na kufanya shughuli za uvuvi wa kisasa,” alisema Rais Dkt. Samia.
Awali Rais Dkt. Samia aliweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana
ya mkoa wa Rukwa iliyopo kijiji cha Mtindilo Laela ambapo amewataka wanafunzi kote
nchini kuongeza bidii ya kujiendeleza katika masomo ya sayansi ili kupata wanafunzi
wenye vipaji.
Rais Dkt. Samia pia alitembelea na kuzungumza na wanafunzi na Mapadri wa Shule ya
Sekondari ya Seminari ya Kaengesa kabla ya kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Barabara
ya lami ya Kaengesa.
Akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya
kampasi ya Rukwa, Rais Samia amesema mradi huo utaleta mapinduzi katika elimu ya
juu ambapo utawasaidia vijana kupata mafunzo kwa vitendo ambavyo vitawawezesha
kujiajiri na kuajiriwa.