Tusimsifu Rais Samia hadi kumfubaza macho, masikio

MACHI 19, 2024 ndiyo siku Rais Samia Suluhu Hassan alitimiza miaka mitatu madarakani. Kumekuwa na shughuli nyingi nzuri za kuonyesha kilichofanyika katika utawala wake kwenye hiyo miaka mitatu. Kumekuwako na makongamano, mijadala na matukio mengi kusheherekea hiyo miaka mitatu ya Rais Samia. Ni jambo jema. Binafsi ninampongeza.

Shughuli za mwaka huu za kusheherekea utawala wa Rais Samia ni kama kielele za utaratibu uliaoanza kwa kasi kubwa alipotimiza mwaka mmoja madarakani. Sote tutakumbuka kuwa kulikuwa na kampeni ya nchi nzima ya kusimika mabango yakionyesha mafanikio ya Rais SSH.

Yamkini msukumo wa mashangilio yale, labda na ya sasa ni kielelezo cha hisia za ndani za watu kutokana na mapito ya aina mbalimbali, hasa tangu mwaka 2015 baada ya Rais Marehemu John Magugufuli ‘alipochaguliwa’ katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Zipo simulizi nyingi juu ya aina na mwenendo wa utawala wa Rais JPM. Wapo wenye kukumbuka na mengi magumu, lakini pia wapo wanaokumbuka nchi ya asali na maziwa.

Kwa kawaida serikali yoyote inayoongoza nchi ni lazima iwe na mipango yake ya kutekeleza. Mipango hii hupangwa kwa vipindi vya muda mfupi, wa kati na muda mrefu. Kila mpango wa serikali shurti uwe na muda wa utekelezaji. Na katika kutekeleza ni shurti pia kuwa na vipindi vya kufanya tathmini. Kwa mantiki hiyo, ni jambo la haki na halali kabisa kufanya tathmini ya nini utawala wa Rais SSH umefanya tangu achukue kijiti cha uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Marehemu JPM, japo alilazimika kuingia Ikulu katika mazingira magumu na machungu ya msiba wa Rais.

Unapomzungumzia Rais SSH na utawala wake huwezi kuacha kuweka ulinganifu na aliyemtangulia. Hii ni hulka ya binadamu, akitaka kujua amepiga hatua kiasi gani, basi anaangalia labda pale alipoanzia na malengo aliyojiwekea au ataangalia wanaofanana naye katika mazingira yaliyo sawa. Kwa mantiki hii, ni sawa kabisa kuulinganisha utawala wa Rais SSH na ule wa mtangulizi wake.

Kwa bahati njema, tathmini za sherehe na majukwaa mbalimbali ambayo yamefanyika hivi karibuni, kwa sekta zote zimesaidia kujenga picha ya mafanikio ya serikali ya Rais SSH, ingawa wasemaji wote wanasema ni mafanikio ya Rais. Wazungumzaji wengi wanawasilisha picha na kauli inayoonyesha kwamba haya ni mafanikio ya Rais SSH, wanakwepa au nisema wanachelea kusema ni ya serikali ya awamu ya sita.

Na ndiyo maana katika miaka ya hivi karibuni misemo kama fedha za Mama, mafanikio ya Mama, maji ya Mama na sifa nyingine za namna hiyo vimekuwa ni vitu vya kawaida. Imekuwa ni halali. Ukisoma ujumbe mbalimbali katika mabango, iwe ni kuonyesha jinsi bajeti imeongezeka kwa sekta yoyote, iwe ni kufanikisha kupeleka huduma ya maji, au barabara, au zahanati au kituo cha afya au hospitali, kila kitu, kinaelezwa ni Mama amewezesha.

Hali hii ya kummiminia sifa Rais SSH, imekuwa ni utamaduni. Kwamba hata Bunge ambalo wajibu wake ni kuidhinisha bajeti ya serikali, halijitaji, kwa maana ya mawaziri na hata wabunge kueleza kwamba fedha za zinazotolewa na serikali ni mali ya umma, ni kodi za wananchi, na kwa vyovyote vile haziwezi kuwa za mtu yeyote.

Hawasemi kwa sababu santuri inayovuma sana kwa sasa ni ‘Mama’. Kila kitu ni cha Mama. Maji ni ya Mama, umeme ni wa Mama, gesi ni ya Mama, barabara ni za Mama, fedha za kila kitu ni za Mama. Hakuna hata mtu mmoja anasimama na kuzungumza mpango wowote wa serikali bila kusema ni wa Mama.

Kwa bahati mbaya sana, katika tathmini yote hii ambayo inafanywa na watu wa aina mbalimbali, wakiwamo watendaji wakuu serikalini, kwenye sekta ya umma na hata baadhi kwenye sekta binafsi, kimbilio limekuwa ni kuonyesha mazuri na kuyafungamanisha na Mama. Nisema kwa uwazi kabisa, ni haki yao kutoa tathmini hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa wameamua kummilikisha kila kitu Mama, basi ingelitarajiwa basi waonyeshe upande wa pili wa sarafu kwa kutonyesha au kugusia hata yale ambayo tumeshindwa. Na haya waseme kwa mantiki ile ile ni ya Mama.

Kwa mfano, hakuna ubishi kwamba kwa sasa hivi sarafu ya Tanzania iko hoi dhidi ya Dola ya Marekani. Ndani ya miezi 12 iliyopita thamani ya Shilingi ya Tanzania imeporomoka sana. Wakati kipindi kama hiki mwaka jana Dola Moja Marekani ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh. 2,332, leo Dola ile ile inabadilishwa kwa Sh. 2,552. Hili ni anguko la Sh. 220 kwa mwaka mmoja tu. Hizi ni takwimu za Benki Kuu ya Tanzania. Mtaani hali ni mbaya zaidi. Mwelekekeo huu haonyeshi kuwa utageuka na hivyo sarafu yetu ikaimarika. Inawezekana sana ifikapo mwisho wa mwaka huu hali ikawa mbaya zaidi.

Tukizungumza mfumuko wa bei kwa ujumla wake hali siyo ya kufurahisha. Kwa wale wanaokwenda katika masoko ya ndani, bei ya vyakula kama maharage, mchele, unga, nyama na vitu vingine vya lazima ili mtu ale viko juu. Bei hizi zimechangamka katika kipindicha mwaka mmoja au tusema katika hiki kipindi kinachosheherekewa. Kwa muda sasa kilo ya nyama katika mabucha mengi iko Sh. 10,000; bei ya maharage inakimbilia Sh. 4,000; kwa kifupi ni kwamba leo hii ukiwa na noti ya Sh. 10,000 ikishaivunja inakuwa kama umeiwasha moto. Haifui dafu kwenye manunuzi.

Bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nazo hazijawa rafiki kabisa kwa kipindi hiki tunachosheherekea mafanikio ya Rais SSH. Tunajua kuna mambo ya vita vya Urusi na Ukraine, ambavyo vimeathiri bei ya mafuta na bidhaa za ngano duniani kote, lakini katika hali halisi ya uchumi wa Tanzania, watu wanasikia maumivu yake.

Vipo vitu vingi sana haviko sawa ndani ya nchi, hasa kwenye uchumi. Kwenye huduma za afya na elimu pia kuna shida. Ni kweli hali ya kisiasa imeimarika sana, usalama uko sawa, tumesikia watu wakitaja takwimu kubwa kubwa za uwekezaji kutoka nje, lakini bado tathmini tunduizi inaonyesha kuwako kuna mapengo mengi. Rushwa imerejea kwa kasi sana, watendaji serikalini wamerejea kwenye ‘umangi meza’ hofu ya fedha za umma hakuna tena, kuna shida nyingi za kutosha kabla ya kudhani kwamba tumefikia hali ya utawala bora uliokusudiwa.

Nimetaja haya machache kutaka kukumbusha jambo moja, kwamba tunapompongeza na kushangilia mwaka wa tatu wa utawala wa Rais SSH, ni vema na haki tukawa na ujasiri wa kusema na kutaja hata yale ambayo yanaleta sura mbaya ili kujipa fursa ya kuyatendea kazi. Kikubwa tusije tukamsifu sana Rais SSH hadi tukamfubaza macho na masikio ya kuona wapi panavuja. Tuwe na kiasi!

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...