ROMBO, KILIMANJARO
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeeleza kutoridhishwa kwake na usimamizi wa mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, huku ikisema kuwa kuna dalili zinazoonyesha waziwazi kuna ubadhirifu wa fedha.
Kaimu Mwenyekiti wa LAAC, Ester Bulaya akiwa na wajumbe wa kamati hiyo amesema wamesikitishwa na utekelezaji wa miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kuchukua muda mrefu na hivyo kutokukamilika kwa wakati, licha ya Serikali kuwapatia fedha za utekelezaji wake.
Bulaya alikuwa mesema hayo baada ya kamati hiyo kukagua ujenzi wa miradi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Rombo na jengo la halmashauri, katika ziara iliyofanyika Machi 20, 2024.
Bulaya amesema katika kuangalia kuangalia matumizi ya fedha za umma na ubora wa kazi zilizofanyika, Kamati yake imebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa maelekezo yalitolewa na Serikali na miongozo ya Ofisi ya Rais TAMISEMI yaliyotaka shilingi milioni 800 kukamilisha ujenzi wa majengo manne.
Amesema badala yake kwa kutumia fedha hizo na nyongeza ya fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri hiyo zaidi ya Shilingi milioni 170, yamekamilika majengo mawili tu, hali inayoonyeha kuwapo viashiria vya ubadhirifu wa fedha hizo za umma.
“Mnajiamulia wenyewe kufanya maamuzi yenu hakuna vibali vya kubadilisha matumizi kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI, kuna hospitali zimepewa bilioni 3.1 majengo yote yamekamilika, nyie hamjakamilisha na mmetumia zaidi ya fedha hizo,” amesema Bulaya.