MUNGU akimjalia binadamu yeyote umri wa miaka 98 ni baraka kubwa. Ni wachache sana wanaopata baraka ya kupata umri huo. Ukifika makaburini kokote na kusoma maandishi kwenye utambulisho wa kila kaburi utagundua kwamba watu wengi hawaishi umri mrefu.
Kujaliwa umri mrefu ni baraka, lakini pia ni neema kama anayepata anakuwa na uzee mwema. Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye alitangulia mbele ya haki jioni ya Februari 29, mwaka huu ni miongoni mwa watu wachache ambao Mungu amewakarimu neema ya uzee mwema ulioshiba miaka.
Rais Mwinyi alikuwa mtu rahimu, walau kwa macho ya kibinadamu. Wakati taifa likiomboleza msiba huu wa Rais wa awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umma umepata wasaa wa kumfahamu kiongozi huo alikuwa mtu wa namna gani.
Kiongozi huyu aliyeingia madarakani zama za mfumo wa chama kimoja cha siasa mwaka 1985 na huhitimisha muhula wake wa kwanza yake mwaka 1995, ameacha nyuma hazina kubwa ya elimu kuhusu uongozi, utu, uvumilivu na kikubwa ya vyote moyo na roho ya kusamehe.
Kuna usemi maarufu kwamba huwezi kumfahamu vizuri mtu hadi pale unampomjaribu kwa mambo mawili, madaraka na mali/pesa. Mzee Mwinyi ambaye alijipatia jina la Mzee Rukhsa kutokana na kuridhia mambo mengi, ni miongoni mwa viongozi wakuu katika bara la Afrika wanaoweza kutajwa kwamba alifaulu mtihani huo. Kwamba madaraka na mali/pesa havikumjaza kiburi kiasi cha kupoteza hulka yake ya uungwana, uvumilivu na roho ya kusamehe.
Nitafanya rejea ndogo hapa ambayo binafsi nilishuhudia. Mwaka 1990 tulikuwa wanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wakati huo Rais Mwinyi alikuwa anahitimisha ngwe ya kwanza ya miaka mitano ya utawala wake. Alikuwa ndiye Mkuu wa Chuo. Zama zile, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye alikuwa Mkuu wa Chuo hicho, tangu zama za Mwalimu Julius Nyerere.
Kukawa na mgomo wa wanafunzi ambao ulikwenda kwa muda mrefu. Mgomo huu ulikuwa umejikita katika madai ya wanafunzi juu ya kudorora kwa huduma katika chuo hicho. Majengo yalikuwa yamechakaa, huduma za kitaaluma zilikuwa zimeathirika pakubwa hii ikichangiwa na mageuzi ya mfumo wa uchumi ambayo yalikuwa yamekwisha kuanza nchini juu ya kuchangia gharama za huduma za kijamii kama elimu.
Katika mgomo huo, Makamu Mkuu wa Chuo wakati huo, Profesa Geoffrey Mmari alialikwa na Baraza la Wanafunzi waliokuwa wamekutana kwa zaidi ya wiki mbili mfululizo, wakijadili hali ya kuzorota kwa hali ya huduma katika chuo hicho. Katika Baraza hilo, Profesa Mmari alitumwa na Baraza kwenda kumleta mtu ambaye angejibu maswali ya wanafunzi kuhusu kuzorota kwa hali ya huduma. Profesa Mmari alikwenda kumwita Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu wakati huo, Joseph Ngonyani.
Ngonyani alifika na timu ya wakurugenzi kutoka wizarani, aliwekwa kiti moto akitakiwa aeleze jinsi wanavyopitisha bajeti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa muda pale chuoni, Katibu Mkuu huyo akijaribu kujieleza, majibu yake hayakukata kiu ya wanafunzi.
Uongozi wa wanafunzi, chini ya Daruso ulimtamkia Ngonyani kuwa ameshindwa kujibu maswali yao, hivyo wakamuagiza aende kumleta Mkuu wa Chuo ili aje kujibu maswali yao. Kikao kiliahirishwa na wanafunzi wakaanza kutoka nje na kumuacha Katibu Mkuu na timu yake pale.
Hata hivyo, baadaye taarifa ililetwa chuoni kwamba Mkuu wa Chuo, yaani Rais Mwinyi alikuwa tayari kuja kuzungumza na wanafunzi endapo tu “fujo zingetulia.” Hakika hakukuweko na fujo. Profesa Mmari alitumwa tena kwenda kwa Mkuu wa Chuo kumpa taarifa kwamba hakukuwa na fujo chuoni, yamkini alikuwa amepotoshwa na Ngonyani. Siku hiyo hiyo Ngonyani alifutwa kazi.
Hata hivyo, Mkuu wa Chuo hakufika chuoni hapo kuja kuzungumza na wanafunzi. Hali hii iliongeza muda wa wanafunzi kuwa nje ya madarasa wakidai kuwa wapo kwenye extended Students Baraza. Hali ya mgomo huo ikazidi kubadilika, hadi ilipofika sasa ikawa ni vita ya mapambano ya fasihi kwenye mabango (literature wall) dhidi ya Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Rais wa nchi.
Ghafla picha yenye sura ya Mwinyi ikawa deal, ikawa inatumika isivyo, yote ikiwa ni kuwasilisha ujumbe kwake. Wenye staha na usiokuwa na staha. Kejeli na hata pengine matusi ya nguoni. Kulishuhudiwa hali wanafunzi kutokutaka kurejea madarasani.
Siku moja lilitokea tukio la kufyatuliwa kwa risasi katika eneo la chuo. Ilielezwa kwamba wanafunzi walimzingira mtu mmoja ambaye walimshuku kuwa ni mwanausalama. Katika rabsha hizo, mwanausalama huyo alijihami kwa kufyatua risasi na kufanikiwa kuponyoka. Baada ya tukio hilo hali ilizidi kuzorota siku baada ya siku.
Katika mfululizo wa hayo mabaraza ya wanafunzi, siku moja niliamka asubuhi, nilipofika eneo la Cafeteria, picha za Mzee Mwinyi nilizoziona zimebandikwa ukutani, moyo ulienda mbio, nilihisi baridi, nilipotafakari nilijua kwa hakika uwezekano wa chuo kuendelea na shughuli zake kama kawaida ulikuwa mgumu. Na kweli, siku hiyo katika taarifa ya habari ya saa saba mchana Serikali ikatangaza kukifunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani kwa muda usiojulikana.
Wanafunzi wote waliamriwa kurejea makwao na hadi ifikapo saa 10 jioni siku hiyo wawe wamekwisha kuondoka chuoni hapo. Baadaye walitakiwa kuripoti kwa wakuu wa wilaya zao. Na waliwekewa zuio la kupewa ajira kokote ndani ya nchi.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam katika utaratibu ambao zamani wakuu wa nchi walikuwa wanautumia kuhutubia taifa, Mzee Mwinyi alisema “nimetukanwa mpaka matusi ya nguoni” na wanafunzi wa Chuo Kikuu.
Hata hivyo, baada ya kupoteza mwaka mmoja wa masomo, Chuo kilifunguliwa. Wapo waliotajwa kuwa ni viongozi wa mgomo, baadhi hawakurudi kabisa, wengine walirudi baada ya muda mrefu zaidi, lakini la muhimu kulikuwa na msamaha mkubwa kwa wengi.
Kumbukumbu hii ninaioanisha na uhuru wa vyombo vya habari ambavyo serikali ya Mzee Mwinyi ilikuwa imeachia kati ya 1990 hadi 1995. Sheria zilikuwa ni zile zile za mtangulizi wake, Mwalimu Nyerere. Lakini Mzee Mwinyi, siyo tu kuwa baadhi ya vyombo vya habari vilimvunjia heshima, kwa habari nyingi za kuzusha na kutunga, bali pia vilivuka mipaka mpaka mara nyingi kuingilia uhuru wake wa faragha.
Mzee Mwinyi alistahimili dhoruba ya mageuzi ya kisiasa, aliacha waliokuwa na kiu ya kuanzisha vyama vya siasa wafanye hivyo baada ya Tume ya Nyalali ya Mfumo wa vyama vingi na kutungwa kwa sheria ya vyama vingi vya siasa. Alimeza na kuvumilia kauli ambazo hazikupima staha wala heshima ya mkuu wa nchi.
Hakutaka kupambana na sauti yoyote iliyomkosoa yeye na utawala wake. Katika kitabu chake cha Safari ya Maisha Yangu alichokitoa mwaka 2020, anaeleza jinsi ambavyo alikaa kimya bila kumjibu Mwalimu Nyerere kila alipokuwa akiushambulia utawala wake. Alichagua fungu jema, kutokulumbana na yeyote.
Katika hali ya kawaida, sioni Rais wa Tanzania anayeweza kujizuia kujibu mashambalizi dhidi ya serikali yake na hasa yanapomlenga yeye binafsi. Baada ya Mzee Mwinyi walikuja marais wengine wanne, pamoja na huyo aliyeko sasa. Tulisikia kauli za ‘mimi sipangiwi’, ‘mimi ni jiwe’, ‘wavivu wa kufikiri’, ‘malofa wakubwa’ nk. Lakini pia Tumeshuhudia watu wakifilisiwa biashara zao kwa hila mbaya, tumeshuhudia watu wakipotezwa, tumeshuhudia kwa hisia tu, watu wakiteswa kwa sababu waliwaza tofauti na Rais. Mwinyi hakuingia katika mitego hiyo.
Mwinyi ameacha somo, kwamba maisha ni hadithi tu, kila mmoja ajitahidi kuacha simulizi njema kuhusu maisha yake – uvumilivu, huruma na msamaha vilikuwa ngao na kigao katika maisha yake. Yamkini ndiyo maana Mungu akamkirimu umri ulioshiba miaka, furaha na amani. Pumzika kwa amani Alhaj Ali Hassan Mwinyi.ends `