UNGUJA.
Watu saba wamepofuka macho Visiwani Zanzibar, kutokana na kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa wa macho mekundu (red eyes). Zaidi ya watu 12,860 wameugua ugonjwa huo, wengine wakiwa wamepona na baadhi wanaendelea na matibabu. Mratibu wa huduma za afya msingi ya matibabu ya macho, Dk Rajab Muhammed Hilali amesema dawa za kienyeji zimewasababishia upofu watu hao na kwamba miongoni mwa wagonjwa waliopata upofu yupo mtoto wa miaka 11.
Dk. Hilal amesma jicho la kulia la mtoto huyo limeathirika na kwamba walimpeleka Hospitali ya CCBRT lakini ilionekana haliwezi kurejea katika hali ya kawaida. Dk. Hilali amesema watu wengi wanaoenda hospitalini wanakuwa wameshazidiwa baada ya kutumia dawa ambazo si sahihi kwa ajili ya tiba. “Kwa wagonjwa hao wana jicho ambalo limepata upofu, ukiuliza unaambiwa alikuwa anatumia dawa za kienyeji, chumvi na vitu vingine kwa hiyo vimeleta athari kwenye jicho,” amesema.
Meneja wa kitengo cha elimu ya afya cha Wizara ya Afya (Zanzibar), Dk Bakar Hamad Madarawa amesema kuna wagonjwa wengi waliougua ugonjwa wa macho lakini hawajaenda kupata matibabu. Amesema takwimu za wagonjwa hao ni takribani asilimia 20, lakini kwa mazingira ya kawaida asilimia 80 ya wagonjwa hao bado hawajafika katika vituo vya afya.
“Takwimu hizi ni asilimia 20 ambazo tunazo sisi Serikali, lakini asilimia 80 wapo wagonjwa wengi, kila familia kwa sasa kuna angalu mgonjwa mmoja, kwa hiyo tuendelee kutoa elimu,” amesema Dk. Madarawa.
Mwishoni wa Januari, 2024 wataalamu wa afya na madaktari bingwa wa macho walinukuliwa na Mwananchi Digital wakisema wamekuwa wanapokea idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa katika hali ya ugonjwa mkali, kutokana na matumizi ya njia mbadala kutibu macho, ikiwamo matumizi ya mkojo, chumvi na vitunguu saumu.
Wataalamu walisema wagonjwa wanaotumia vitu tajwa macho yao huvimba na kuuma zaidi pamoja na kupatwa homa, huku hasi zinazotajwa zaidi ni kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho. Tiba hizo mbadala zinaelezwa kuwa zinaweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.
Ugonjwa huo ujulikanao viral keratoconjunctivitis (red eyes), mbali ya Zanzibar, pia umesambaa maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.
Chanzo: Mwananchi