Tanesco hoi, shida ni Tanesco au Serikali?

WIKI iliyopita katika safu ya Nyuma ya Pazi nilijadili suala la mgawo wa umeme. Nilijielekeza kwenye hoja moja muhimu, kwamba Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limebweteka sana.

Katika kubweteka kwake limefika mahali na kuamini kwamba kwa fikra zake, linaweza kuandoa mgawo wa umeme nchini kwa kuendelea kuamini vyanzo vya umeme wa maji (hydroelectricity) vitaivusha. Tanesco inaendelea kuamini hivyo kwa sababu zilizowazi kabisa, bado inaelekeza nguvu kubwa huko.

Soma pia: https://themediabrains.com/2023/11/21/tanesco-imebweteka-itoke-kwenye-boksi-la-raha/

Ingawa, Tanesco inakiri kuwa kwa sasa kiasi cha asilimia 64 ya nishati ya umeme unaotumika nchini unazalishwa kutokana na gesi asilia, inakuwa ni vigumu kujua kwa mfano ni kwa nini haijielekezi kwa vyanzo vingine vya kuzalisha umeme kama joto jua na upepo. Vyanzo hivi hapa nchini havijazaendelezwa kabisa. Bado Tanesco inafikiri inaweza kutoboa kwa hydroelectricity.

Leo naomba kupiga hatua moja mbele zaidi juu ya hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme nchini. Kwamba bado mgawo wa umeme unaendelea nchini kote. Tanesco hawasemi ni mgawo wa umeme, bali ni ratiba ya upatikanaji wa umeme. Kwa vyovyote wanavyojaribu kuficha ‘ugonjwa’ bado hali ya taifa letu juu ya upatikanaji wa nishati hii siyo ya kutia moyo hata kidogo. Ni kero na karaha kubwa. 

Wakati Tanesco ikitaabika na kugawa umeme kila leo, naomba kulikumbusha shirika hili la nishati nchini kwamba mwaka jana siku ya Jumatano Novemba 23, yaani mwaka mmoja kamili mpaka sasa, Tanesco walitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikielezea upungufu wa umeme nchini. Katika taarifa hiyo, pia walieleza mipango ya kukabiliana na upungufu huo.

Kwa mfano, Tanesco walisema wanapitia katika kipindi kigumu cha upungufu wa umeme unaosababishwa na ukame na matengenezo ya mitambo. Walisema jumla ya megawati 300 hadi megawati 350 za umeme zilikuwa zimepungua katika uzalishaji.

Leo mwaka mmoja tathimini yoyote itakayofanywa inaonyesha kuwa Tanesco wanasema mambo ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza. Kwamba inakuwaje leo mwaka mmoja hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana kipindi kama hiko?

Iliorodhesha vituo vya kufua umeme vilivyokuwa vimeathiriwa na ukame kuwa ni Kihansi kilichokuwa kinazalisha megawati 17 badala ya megawati 180, kwa hiyo megawati 163 zilikuwa hazizalishwi; Pangani kilichokuwa kinazalisha megawati 10 badala ya megawati 68, hivyo kuwa na  upungufu wa megawati 58; Mtera nayo ilikuwa inazalisha megawati 75 badala ya megawati 80 hivyo kutokuzalisha megawati tano; Nyumba ya Mungu ilikuwa inazalishaji megawati 3 badala ya megawati 8 ukiwa ni upungufu wa megawati tano.

Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kuwa kituo cha Kidatu kilichokuwa kinazalisha megawati 200 kilikuwa kikizalisha megawati 150 ukiwa ni upungufu wa megawati 50; Ubungo III kilikuwa kinazalisha megawati 37 badala ya megawati 112, ukiwa ni upungufu wa megawati 75; Kinyerezi II ilikuwa ikizalisha megawati 205 badala ya megawati 237, hiyo megawati 32 hazikuwa zikizalishwa. Kwa hesabu za Tanesco mwaka mmoja uliopita ukame na matengenezo ya vituo vyake vilisababisha upungufu wa megawati 388 za umeme.

Shirika hili kongwe na pekee la kuzalisha nishati ya umeme nchini lilisema kwamba walikuwa wana mipango ya muda mfupi kukabiliana na hali hiyo, ambayo ni kuharakisha matengenezo ya mitambo hiyo ambayo ingesaidia kurejesha megawati 90 kwenye gridi ya taifa.

Tanesco ilisema ingekarabati kituo cha Ubungo III ili kuingiza megawati 35 za umeme kwenye gridi ya taifa ilipofika tarehe 25 Novemba 2022; matengenezo ya mitambo miwili ya Ubungo III nayo yangesaidia kuingiza megawati 40 za umeme ilipofika mwishoni mwa Disemba 2022; kukamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu ili kuingiza megawati 50 za umeme tarehe 30 Novemba 2022; kufunga mitambo miwili katika kituo cha Kinyerezi I ili kuingiza megawati 90 za umeme kabla ya mwisho wa mwezi Disemba 2022. Kazi zote hizo zililenga kuingiza megawati 277 kwenye gridi ya taifa.

Shirika hilo lilisema kuwa lingetekeleza mipango ya muda wa kati kwa kupanua kituo cha Kinyerezi I ili kuingiza megawati 90 za umeme kwenye gridi ya mwezi Februari 2023 na kufikisha jumla ya megawati 337 za umeme.

Leo mwaka mmoja tathimini yoyote itakayofanywa inaonyesha kuwa Tanesco wanasema mambo ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza. Kwamba inakuwaje leo mwaka mmoja hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana kipindi kama hiko?

Tafakari ya kina kuhusu mwenendo wa Tanesco unaonyesha kuwa shirika hili limekwama sana. Kukwama huku kunaweza kuthibitishwa hata na kasi ya kubadili menejimenti yake kila baada ya muda mfupi sana. Wakurugenzi wakuu hawadumu Tanesco. Serikali inafikiri tatizo ni wakurugenzi wakuu, lakini ukweli ni kwamba tatizo la shirika hili ni zaidi ya wakurugenzi wakuu.

Tangu utawala wa Rais Benjamin Mkapa alipojaribu kutafuta mwarobaini wa Tanesco kwa kuleta kampuni ya kimanejimenti kutoka Afrika Kusini, Net Group Solution, ambayo licha kuingizwa ofisini kwa lazima kwa mtutu wa bunduki kwa kuwatisha wafanyakazi, hakuna cha maana ilichofanya Tanesco mbali ya kuzidi kudidimiza shirika hili kongwe la umma.

Utawala wa Rais Kikwete ulirithi Tanesco iliyokuwa imechoka mbaya. Ni hali hiyo ilisababisha kampuni binafsi ya Richmond ikipewa kandarasi ya kuzalisha umeme megawati 120 ambao hata hivyo nazo hazikuzalishwa. Hali ya shirika hili chini ya utawala wa Kikwete haikuwa na nafuu yoyote, liliendelea kuelemewa na madeni makubwa ya makampuni binafsi ya kuzalisha umeme chini ya mikataba ya Power Purchase Agreement (PPA).

Hali hii ndiyo ilikutwa na utawala wa awamu ya tano ya Dk. John Magufuli. Pamoja na utawala wa Magufuli kuipeleka puta Tanesco, na kupigwa marufuku kuwa na mgawo wa umeme, leo hali ya shirika hili inathibitisha pasi na shaka yoyote kuwa ugonjwa wake haujawahi kupatiwa tiba.

Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani Machi 2022. Mwaka huo huo Novemba Tanesco wakatangaza hali mbaya ya upatikanaji wa umeme, hali ambayo ukitafakari ni kama imekuwapo nchini tangu mwaka 1996. Yaani miaka 27, muda unaokaribia miongo mitatu, shida za Tanesco ni zile zile.

Wiki iliyopita niligusia hapa kwamba hivi karibuni kulikuwa na picha iliyokuwa ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa Tanesco walipata kuwa na mgawo wa umeme tangu mwaka 1975. Hakika, chanzo kikuu cha nishati cha kutegemea maji kimekuwa tanzi kwa Tanesco. Leo miaka takribani 50, nusu karne, shida za Tanesco ni zile zile. Uzalishaji mdogo wa umeme, mabwawa kukauka maji!

Swali la kujiuliza ambalo serikali inapaswa kujitafakari ni hili, hivi kama miaka 50 iliyopita shida za Tanesco zimekuwa ni zile zile, bado inafikiri shida ni Mkurugenzi Mkuu? Au ni muundo wake au ni aina ya vyanzo vya kutengeneza nishati hii ambavyo serikali imekuwa ikikimbizana navyo miaka yote hii? Nani alaumiwe, serikali au Tanesco? Serikali sasa ni lazima ifikiri upya juu ya Tanesco.

spot_img

Latest articles

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

TANZANIA KUPAMBANA NA JANGWA

Na Mwandishi wetu Serikali imejipambanua katika kupambana na kuenea kwa jangwa, kurejesha ardhi iliyoharibiwa pamoja...

More like this

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...