Upole wa Watanzania umezaa kujipendekeza?

KUNA watu wanaishi mwaka 2023, lakini wanatamani sana wawe katika mfumo wa siasa za mwaka 1977. Mfumo wa chama kushika hatamu, mfumo wa wanasiasa uchwara kuibuka huko na huko kutaka kuwapelekesha watendaji serikalini, kisa eti wanatokana na chama kilichoshinda uchaguzi.

Kwa bahati mbaya sana tangu taifa hili liingie kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 hadi leo wangalipo watu wanaofikiri na kutamani kuona kama mfumo huo ni fadhila, ni haki ya chama tawala na kwamba wangependa tuishi kana kwamba bado tunaendelea na mfumo wa chama kimoja.

Ujinga huu tuliushuhudia ukiasisiwa kama siyo kufufuliwa kwa nguvu sana kuanzia mwaka 2015, hata leo bado kuna nguvu kubwa sana ya kuendelea kuudekeza na kutaka kuaminisha umma kwamba mfumo wa chama kimoja ni bora katika kuletea wananchi maendeleo. Ukweli usio na chembe ya shaka ni kwamba mfumo wa chama kimoja ni janga kwa maendeleo, kwa uwajibikaji na ustawi wa taifa kwa ujumla wake.

Hivi karibuni kwenye mitando ya kijamii imesambazwa picha ya mtendaji mmoja wa serikali ngazi ya Ofisa Elimu Mkoa akizungumza maneno ya kushangaza. Kwamba: “Anayetoka chumbani kwa mama yako na taulo ndiye baba yako, haiwezekani walimu mlipwe mshahara na serikali ya CCM halafu mnashabikia vyama vya upinzani, tukikubaini tutakutafutia kesi hata ya ubakaji au uhujumu uchumi ukafie gerezani.”

Haya ni maneno yanatamkwa na mtu mwenye dhamana kubwa kiasi hicho, na anayeona ni sawa tu. Huyu hana kingine anachotamani badi mfumo wa chama kimoja, ambao anafikiri unaruhusu uendeshaji wa mambo kama jamii ya kambale, isiyotii sheria bali viongozi kufanya lolote bila kujali mipaka ya sheria kanuni na taratibu.

Juzi hapa amesikika Paul Makonda, Katibu wa CCM wa Itikadi na Uenezi, akiamrisha mawaziri kwamba wanatakiwa kuwasilisha kwa sektretariati utekelezaji wa ilani ya CCM kila baada ya miezi mitatu. Anadai hayo ni maagizo ya chama. Katika mkutano huo Makonda huyo pia alionekana akimuamrisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kukimbia mara moja pale alipokuwa ili akajibu maswali yake. Na mkuu huo wa mkoa naye akakimbia kwenda alikokuwa amesimama Makonda kujibu hicho alichokuwa anaulizwa.

Ukiangalia mkorogo unaoendelea, ni kama CCM au niseme baadhi ya viongozi wa CCM aina ya Makonda wanafikiri kwa kuwa serikali iliyopo madarakani inatokana na chama chake, basi wao wana haki ya kuwaagiza watendaji wa serikali na hata mawaziri wapendavyo. Kwamba sasa mawaziri watakuwa wanawasilisha taarifa ya utendaji wao kwa sekretariati kila baada ya miezi mitatu. Mtu anaweza kujiuliza, je, katika masharti haya mapya, nini kina na kiwango cha chama kuingia ndani ya utendaji wa serikali?

Je, utaratibu wa zamani wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ndani ya vikao rasmi vya chama kama kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa na kwenye Mkutano Mkuu wa CCM hautoshi kupima utendaji wa serikali?

Kama Mawaziri wanawajibika kuwasilisha taarifa hiyo kwa sekretariati, je, Bunge nalo litawasilisha wapi? Na je, mahakama nayo itawasilisha wapi? Ni ipi mipaka ya sektretariati kutaka kuingia ndani kabisa ya serikali na kuwawajibisha mawaziri? Je, Rais ambaye ndiye mkuu wa serikali naye atawasilisha ripoti ya utendaji wa serikali Bungeni au kwa sektretariati pia? Na yeye kama Mwenyekiti wa CCM atapokea ripoti hiyo kutoka kwake mwenyewe au kutoka kwa makamu wake au kutoka kwa Waziri Mkuu? Na kazi ya Bunge ambayo ni ya kikatiba ya kuisimamia serikali imepokwa na sekretariati chini ya maelekezo ya Makonda kwa kisingizo ni agizo la chama?

Makonda ambaye anamwita Mkuu wa Mkoa na kutaka akimbie mara moja pale alipo, yeye wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, siyo tu alijiona mungu mtu, bali alijigamba kuwa yuko juu sana kiasi cha kuwataka mawaziri wawe na adabu kwake. Aliwataka watambue kuwa wapo wakubwa wa nchi wanaomuheshimu sana, alijiona ana hadhi maalum. Lakini leo hataki kuona Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa naye ana hadhi na kwa maana hiyo ajaribu kumuheshimu walau kwa nafasi hiyo ya kumwakilisha Rais katika mkoa wa Dodoma.

Makonda siyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wa kwanza. Walipata kuwapo kina Kungunge Ngombale Mwiru, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, John Mngeja, Samson Msoma, John Chiligati, Nape Nnauye, Humphrey Polepole, Shaka Hamdu Shaka, Sophia Mjema na wengine, lakini hakuna ambaye amekuwa na hulka, majivuno na udhalilishaji wa aina ya Makonda. Hata pale walipotaka kuona serikali ikitekeleza ilani ya uchaguzi ya chama chao kwa kasi zaidi, walau walikuwa na lugha ya staha.

Ni kwa nini ni Makonda tu anaingia na gia ya kutaka kushindwa kutambua kuwa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, serikali inaendesha mambo yake kwa kufuata katiba na sheria. Kwamba mgawanyo wa madaraka umewekewa mfumo wazi wa uwajibikaji. Kila muhimili una njia na mipaka ya kuwajibika. Na katika njia hizo, viongozi wa chama kinachotawala hawawezi sasa kuanza kutaka kuingia jikoni ndani ya serikali na kutaka kuamrisha mambo. Chama hicho kina mfumo wa vikao, kuna ratiba ya kazi. Serikali inawajibika kwenye Bunge. Bunge lina wajibu wa kuisimamia serikali. Je, kwa akili ya ki-Makonda Mahakama nayo iwasilishe taarifa kwa sektretariati? Na Bunge je?

Mkorogo huu wa Makonda unatokana na kitu kimoja tu. Ukosefu wa maadili. Makonda ni mtovu wa maadili siyo leo wala jana, ndivyo alivyo. Ni asili yake. Ni mtu mtukutu.

Mara nyingi amekuwa ama akitumwa kufanya kazi chafu au amekuwa akijituma mwenyewe kufanya kazi chafu ili kujitengenezea uhalali. Ni Makonda huyu huyo akiwa kinda kabisa kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM) zama za kina Nape alipewa kazi ya kumtukana aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wakati huo Jakaya Kikwete akiwa Rais na Mwenyekiti wa chama tawala. Ni wakati huo Kikwete baadaye alimzawadia ukuu wa wilaya ya Kinondoni baada ya kazi yake chafu ya kumtukana Lowassa.

Kwa hiyo, Makonda huyu ni kama alitumiwa na watu wa Kikwete kumtukana na kumdhalilisha Lowassa. Ni Makonda huyu huyu chini ya Magufuli alipanda chati na kuwa Mkuu wa Dar es Salaam, akanyanyua mabega na kuota pembe, akawa mtu maalum, akawa anadhalilisha kila mtu. Alipata hata kujaribu kumtikisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro tena mbele ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa. Busara ya Majaliwa ndiyo ilimuokoa Sirro.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda kabla ya mazungumzo yao ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma,

Orodha ya watu ambao Makonda akiwa Mkuu wa Mkao wa Dar es Salaam aliwadhalilisha, kuwavunjia heshima na hata kuwasababishia madhara makubwa, ni ndefu mno. Hata leo hajawahi kujutia na kuwaomba radhi.

Katika hali ya kawaida, Makonda ni kielelezo cha taifa hili kusahau kuwa maadili ya uongozi ni kitu chenye umuhimu wa kipekee kwa yeyote anayekalia ofisi ya umma. Ni katika mazingira haya, mtu anashindwa kujizuia kuuliza hivi katika taifa hili ni nani tena anajali kuhusu maadili? Hivi kile kiapo cha maadili wanachokula wateule wa Rais baada ya kuapishwa kina nguvu gani? Hivi taarifa za ukiukaji wa maadili ambazo aghalabu hufika kwenye Tume ya Maadili kwa malalamiko rasmi au kwa njia ya Tume kuanzisha uchunguzi wake huru, zina nafasi gani katika kusaidia kuteuliwa kwa watu wa kukalia ofisi za umma?

Kuna wakati maswali magumu yanakosa kabisa majibu. Nchini Uingereza mwaka 2019 wakati chama tawala, Conservative wakitafuta kiongozi mpya wa chama kufuatia kujiuzulu wa Waziri Mkuu Theresa May, aliyekuwa Waziri wa Mazingira, Michael Gove, alianza harakati za kutaka kuwania nafasi hiyo, vyombo vya habari vikamkumbusha kwamba alipata ‘kubuya unga’ (cocaine). Harakati zake ziliishia hapo hapo.

Hapa kwetu, siyo tu tuhuma hazitoshi kumfanya mtu aepukwe kupewa nafasi kwenye ofisi ya umma kama dhana ya mke wa mfalme asivyotakiwa kuwa karibu na tuhuma, bali hata waliotiwa hatiani wanatetewa. Ushahidi wa kimazingira upo, lakini nani anajali?

Kwa nini kiburi chote hiki? Kwamba wateuaji wana ujasiri na jeuri wa kuteua watu wenye tuhuma chafu, mikono michafu? Ni kwa sababu wananchi wetu wamepuuzwa sana? Kwamba utamaduni wa kutokuadhibu maovu umeota mizizi kiasi kwamba sasa ni halali kwa lolote kiongozi afanyalo, liwe zuri au baya. Kwamba kwani wananchi watafanya nini?

Nilipata kutafakari na kujiuliza ni nini hasa gharama za wananchi kulishwa pilau ya bure, Tshirt za bure, kofia za bure, kusafirishwa bure kwenda kwenye mikutano wakati wa uchaguzi? Ni kwa nini imefika hatua eti wapo watu wenye ujasiri wa kukusanya kadi za wapiga kura na kukaa nazo mpaka siku ya kura? Ni kwa sababu watu wetu wamekuwa waoga na wapole mno kiasi cha kupokwa haki zao bila kufanya lolote. Hata kununia uovu wameshindwa.

Matokeo ya upole huu mbaya ni kuzaliwa kwa tabia ya kujikomba na kujipendekeza ambayo imeathiri kabisa uwezo wa kufikiri wa watu wetu. Ni katika mazingira hayo watu kama Makonda wanaonekana ni mashujaa kumbe walipaswa kuwa mahakamani wakijitetea dhidi ya uovu waliotenda wakiwa kwenye ofisi za umma.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...