Na Winfrida Mtoi, Media Brains
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amezipongeza kampuni ya Media Brains na Shirika linalojihusisha na Kuendeleza Mifumo ya Chakula Afrika (AGRA) kwa kuandaa mafunzo kwa wanahabari yanayohusu mbegu bora za kilimo na mfumo wake wa uzalishaji.
Media Brains na AGRA zimeandaa mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika Novemba 3-4, 2023 katika hoteli ya Oceanic iliyopo Bagamoyo, yakihusisha wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari.
Balile ambaye ni kati ya washiriki, amesema mafunzo hayo ni ya kipekee ambayo ni tofauti na waliyozoea kufanya mengi yakilenga zaidi masuala ya siasa.

“Niwapongeze Media Brains na AGRA kwa kuandaa mafunzo haya ya kipeke, mikutano kama hii inayogusa wananchi moja kwa moja imekuwa haipewi kipaombele,” amesema Balile.
Wawezeshaji katika mafunzo hayo ni watafiti wabobezi katika masuala ya mbegu kutoka taasisi mbalimbali, akiwamo Dk. Emmarold Mneney ambaye amebainisha kuwa mbegu bora ina uwezo wa kukabiliana na tabianchi.

Dk. Mneney amefafanua kuwa mabadiliko ya tabianchi hayawezi kukwepeka na njia ya kukabiliana nayo ni kuzalisha mbegu zilizoboreshwa ili kufikia lengo la kuilisha dunia.
“Elimu ya mbegu haipo ya kutosha, inatakiwa kutolewa kwa vitendo ili wananchi waweze kuhamasika na kuzalisha mbegu zenye ubora,” ameeleza Dk. Mneney.
Naye Dk. Geradine Mzena kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI, amesema kutokana na ongezeko la idadi ya watu na wazalishaji wa mbegu wanatakiwa kuwa wengi ili kupata chakula kinachotosheleza.
“Ni kweli mbegu hazitoshi lakini Serikali imeanza kujenga maeneo mengine ya kuzalisha mbegu ili kulinda chakula,” amesema.