Ya Makonda ni jeuri, huruma au kujisahaulisha?

Katika jamii ya binadamu yapo mambo ambayo hayakatazwi kisheria, lakini yanabebwa kwa tahadhari na uangalifu mkubwa sana. Miongoni mwa mambo hayo ni uadilifu au unyoofu wa matendo. Kwa kimombo huitwa moral. Jamii ikipuuza uadilifu au unyoofu inakuwa imechagua kukumbatia uovu. Unyoofu na uovu hawakai zizi moja.

Kuna siku nilikuwa nikifuatilia mjadala kwenye Kamati ya Bunge la Uingereza, ikimhoji mmoja wa wakurugenzi wa kampuni maarufu duniani inayouza kahawa, Starbucks. Wabunge walikuwa mbogo dhidi ya kampuni hiyo yenye migahawa mikubwa ya kahawa duniani, kwa sababu ilipofungua migahawa yake nchini humo mwaka 1998 ilikuwa imefanya mauzo ya zaidi ya Pauni bilioni 3 katika mnyororo wa migahawa yake 735.

Katika fedha hiyo iliyokuwa imetengeneza, walikuwa wamelipa kodi kidogo tu kama Pauni milioni 8.6. Kiukweli wabunge waliona kampuni hiyo kama ilikuwa inacheza na sheria za kodi, hivyo kufanikiwa kuepa (avoid) kulipa kodi stahiki kwa serikali.

Mkurugenzi huyo alipobanwa sana alisema hakuna sheria yoyote wamevunja, wamezingatia taratibu zote. Wabunge walikuwa na msimamo mmoja kwamba suala lililokuwa mbele yao siyo la kisheria, bali la kimaadili, suala la unyoofu wa matendo. Kwamba kampuni inayotengeneza mabilioni haijali kulipa kodi. Mbunge mmoja aling’aka akasema: ‘What we are saying it is immoral, is not an issue of legality.” (tunachosena hapa ni suala ukengeufu wa uadilifu na siyo suala la sheria).

Ni kutokana na kauli hizo, mkurugenzi wa Starbuck aliinama chini, hakuweza kuwatazama usoni wabunge. Yaani kwa jamii ile (Waingereza) Starbucks pamoja na kutafuta njia ya kuepuka kulipa kodi, kisheria, walikosa kabisa unyoofu wa matendo katika kufanya biashara zao nchini Uingereza.

Tumesimuliwa mara kadhaa kisa cha mke wa Mfalme ambaye alituhumiwa uzinzi. Uchunguzi ulifanyika na ikaonekana haikuwa kweli. Hata hivyo, aliachwa kwa kile Mfalme alichosema ‘mke wa mfalme anapswa kuishi maisha ambayo hata tuhuma hazipaswi kumfika’. Kwa maneno mengine, mwenendo wa maisha ya mke huyo yanapaswa kuwa ya kiuadilifu kiwango kwa ambacho hata hawezi kufikiriwa kwenye jambo lolote la ovyo.

Viongozi wa umma, iwe kwenye serikali au taasisi za umma kama vyama vya siasa, wanapaswa wakati wote wajipime kwenye mzani wa uadilifu. Unyoofu wa matendo yao wakati wote wanapotumika kwenye nafasi za kutumikia umma. Hili ni jambo la msingi siyo kwa sababu nyingine yoyote bali ili umma uwe na imani na hao waliokali ofisi za umma.

Uadilifu hupimwa katika mawanda mapana. Ni kwa jinsi gani madaraka uliyopewa unayatumia katika staili ambayo haileti ukakasi kwa wengine, hasa wasiyokuwa nayo. Umma. Ni kwa jinsi gani unajiepusha na mfumo wa maisha ambao kimsingi unajivalisha madaraka na kuyatumia katika staili ambayo unataka uonekane wewe tu, usikike wewe tu, ujulikane wewe tu, utukuzwe wewe tu, na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Mwishoni mwa wiki Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata kiongozi mpya kwenye nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uendezi, Paul Makonda. Huyu alipata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kabla ya kuamua kwenda kujaribu kutafuta ubunge akaishia kwenye kura za maoni katika jimbo la Kigamboni mwaka 2020. Wakati huo, Rais wa awamu ya Tano, John Magufuli, alikuwa amekwisha kutangaza kwamba yeyote mwenye nafasi ya uteuzi atakayekwenda kujaribu ubunge, nafasi yake ataijaza mara moja. Alisema wazi anachukizwa na watu wenye tamaa.  

Rais Magufuli Machi 13, 2016 alimteu Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, sambamba na wakuu wengine 25, wakiwamo 13 wapya na saba wakibakizwa kwenye vituo vyao kazi, watano wakihamishwa, na mmoja kupangiwa mkoa mpya wa Songwe ulioanzishwa kisheria kwa tangazo la serikali (GN) number 461 Januari 29, 2016. Kabla ya hapo Makonda alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Tangu aliopoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda aliamua kujiweka katika nafasi ya kipekee kabisa kiutawala, kimwenendo na kimamlaka. Ni kiongozi aliyejikuta akibuni mikakati mingi na mbinu nyingi za kiutawala, ambazo mara nyingi ziliacha maswali kuliko majibu. Kwa mfano, ni Makonda aliamua kukarabati magari ya polisi katika mkoa wa Dar es Salaam – hatujui kwa yakini ni nani alilipa hizi gharama.

Ni Makonda aliyeamua (akiwa DC Februari 2016) kutangaza kwamba walimu wa shule za serikali Dar es Salaam kuanzi Machi 7, 2026 wangepanda daladala bure – haikutokea. Ni Makonda alitangaza hadharani orodha ya watu waliodaiwa kuwa ni wauza dawa za kulevya, na kuwataka waende Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kutoa maelezo.

Ni Mkonda aliyeitisha wanawake wanaodaiwa kutelekezwa na wanaume wao ofisini kwake Ilala jijini Dar es Salaam, katika mkutano ambao baadhi ya majina ya watu yalitajwa kuwa wameteleza wanawake na watoto.

Kadhalika, ni Makonda aliyedaiwa kuwa na kikosi chake kinachomlinda na ambacho alikuwa anakiendesha yeye, ni makonda tu miongoni mwa wakuu wote wa mikoa wa Tanzania aliyekuwa na msafara wake.

Ni Makonda akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alisababisha miongoni mwa mwaziri vijana apoteze nafasi yake kutokana tukio lake la kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds. Nape Nnauye akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliamua kuvalia njuga suala la Makonda kuvamia kituo cha habari, aliunda kamati iliyoongozwa Mkurugenzi wa Habari Melekezo wakati huo, Hassan Abbas. Baada ya kamati hiyo kufanya kazi kwa siku kadhaa na kutoa ripoti yake, Magufuli alitengua nafasi ya Nape. Dalili za kwamba Magufuli angemlinda Makonda dhidi ya utovu wa uongozi aliofanya Clouds, zilianza kujionyesha siku akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Ubungo (Ubungo Interchange), ambako alimwambia Makonda “wewe chapa kazi mimi ndiye nimekuteua.” Magufuli alisema hayo wakati kamati ya Nape ikikamilisha kazi yake.

Kumekuwa na madai au tuseme tuhuma nyingi zikimzingira Makonda, nyingine ni za kuogofya sana. Kumekuwa na madai pia kwamba Makonda alikuwa mtoto deko kwa Rais Magufuli. Mtindo wake wa kuendesha ofisi, magari aliyokuwa anatembelea, ulinzi aliokuwa amepewa na kauli zake za mara kwa mara kuonyesha kwamba yeye alikuwa ni maalum, vilifanya umma usadiki kwamba alikuwa na nafasi maalum kwa Rais Magufuli. Hata hivyo, Makonda hajawahi kufikishwa kwenye mahakama yoyote kujibu mashitaka ya tuhuma zozote zile. Na kwa kuwa hakujawahi kuwako na mashitaka dhidi yake, hizi zinabakia kuwa ni tuhuma tu.

Hata hivyo, kama ambavyo nilisema hapo juu, unyoofu wa matendo, hasa katika ofisi ya umma ni mambo makubwa na mazito. Uongozi siyo suala la kisheria tu, ni zaidi ya sheria, ni kwa jinsi gani mtu mwenye madaraka anajiweka mbele ya umma ni jambo la msingi sana.

Ni katika kutafakari unyoofu huu, mtu anawaza na kuwazua, hivi CCM katika wanachama wake wote hakuwamo mwingine ambaye hana tuhuma kama hizi? Je, hisia za umma kwa wateuaji wa nafasi hizi siyo kitu cha kuwasumbua akili kabisa? Kwamba siku hizi CCM inaweza kuamua kutokujali kwa kiasi hicho, kwamba wapo watu wenye madai yao ya kuumizwa ama kwa maelekezo au matendo ya Makonda moja kwa moja, siyo jambo la kusumbua hili? Tafakari.

spot_img

Latest articles

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

More like this

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...