Sophia Mjema na staili mpya ya ‘atake asitake’

KATIKA vitu vinavyotajwa kuliangusha Bara la Afrika kiasi cha kushindwa kupiga hatua za maana za maendeleo ni tabia ya watu wake, hasa wanasiasa, kuwaza tu uchaguzi kama mfumo mzima wa maisha yao na kuyafunga mataifa yao katika minyororo ya siasa za uchaguzi. Ndiyo maana uchaguzi ukifanyika leo, kesho zinaanza harakati mpya za kujipanga kwa ajili ya uchaguzi unafuata hata kabla ya kutumikia dhamana iliyopatikana katika uchaguzi husika.

Hali hii ndiyo imejikita katika harakati za kubadili katiba za mataifa mbalimbali ya Afrika kwa kuondoa vifungu vya katiba vinavyoweka masharti ya kushika nafasi hiyo kwa muda usiozidi vipindi viwili vya uchaguzi.

Zipo nchi zinazofanya uchaguzi baada ya miaka mitano, nyingine miaka saba nk, kwa muktadha huo, katiba zinataka anayekalia kiti cha urais awe na haki ya kuchaguliwa mara mbili tu.

Utaratibu huu uko pia katika mataifa makubwa kama Marekani ambako Rais anaruhusiwa kugombea mihula miwili tu ya miaka minne kila mmoja, hivyo kuongoza kwa miaka minane tu. Zipo sababu nyingi za kuweka ukomo wa mtu kuwa Rais.

Kubwa ya yote ni kuepusha hatari ya kuwa na marais wafalme, kujenga uwajibikaji, lakini kubwa zaidi ni mbinu ya kusaidia kujenga uvumilivu kwa taifa kwamba hata kama aliyekalia kiti cha urais amekuwa mtu wa ovyo sana, muda si mrefu ataondoka na kuachia mwingine naye ajaribu kuongoza. Mfumo huu husaidia pia kuepusha vitu kama mapinduzi ya kijeshi kwa wananchi kumkinai akiyekalia kiti cha urais hasa inapokuwa amekuwa ni kiongozi ambaye amepoteza kabisa mwelekeo.

Sophia Mjema.

Hivi karibuni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliingia madarakani Machi 2021 kufutia kifo cha mtangulizi wake, Rais John Pombe Magufuli, ana haki ya kugombea nafasi hiyo kwa vipindi viwili vya urais vya miaka mitano kila kimoja.

Yaani mwaka 2025 na 2030, kwa maana hiyo kama atakuwa amepata ridhaa ya wananchi, basi Rais Samia atakuwa anamaliza muda wake wa utawala mwaka 2035. Kwa maneno mengine, Sophia ni kama anatoa ilani kwa wanaCCM kwamba asiwepo yeyote wa kupambana na Rais Samia kwa sasa kwa sababu bado ana nafasi ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Na kwa utaratibu na utamaduni wa CCM, Rais anayetokana na chama chao kama hajamaliza kipindi chake akishachaguliwa kwa mara ya kwanza huwa hana mpinzani bali hupitishwa tu kama mgombea pekee.

Sophia amesema haya angali akijua wazi kwamba urais wa Tanzania unapatikana kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni katiba hiyo ndiyo imeweka utaratibu wa masharti ya kupata urais. Sophia anajifunika kwenye hoja kwamba kama Rais Samia atakuwa anapitishwa kugombea urais mwaka 2025, itakuwa ndiyo mara yake ya kwanza. Kwa maana hiyo, anaanza kuheshabiwa kipindi chake cha kwanza 2025 – 2030 na cha pili 2030 – 2035, kwa maana hiyo kukamilisha miaka 10 ya kikatiba madarakani.

Ingawa Sophia anaweza kuwa na hoja juu ya Rais Samia kupigiwa kura kwa mara ya kwanza mwaka 2025, lakini anasahau kwamba kwa sasa Samia ni Rais kikatiba. Kwamba alichukua madaraka kutoka kwa Magufuli kulingana na mashari ya Ibara 37(5) ya Katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania inayoainisha wazi kwamba Rais akifa akiwa madarakani nafasi yake itachukuliwa na Makamu wa Rais.

Samia alikuwa Makamu wa Rais wa Magufuli. Hata hivyo, ibada hiyo inafanyiwa ufafanuzi wa kina na ibara nyingine ya 40 (4) inayoeleza muda ambao huyo aliyerithi kiti cha urais kwa sababu ya kifo atakuwa na haki ya kutumikia kiti hicho. Masharti ya ibara ya 40 (4) yanafafanua kuwa kama aliyerithi kiti cha urais (kama ilivyotokea kwa Samia) atakuwa na haki ya kumalizia kipindi cha rais aliyefariki. Katika kumalizia muda huo, kama ni miaka mitatu au zaidi, basi kipindi hicho kitahesabiwa kuwa ni awamu ya kwanza ya huyo Rais aliyerithi mikoba na kwa maana hiyo, atakuwa na haki kikatiba kugombea kipindi kimoja tu. Lau, kama ni chini ya miaka mitatu, basi atakuwa na haki ya kuwania vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.

Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika mazingira ya Rais Samia, aliingia madarakani Machi 2021 na ifikapo Desemba 2025 atakuwa amehudumu nafasi ya urais kwa muda wa miaka minne na miezi kama tisa hivi, yaani zaidi ya miaka mitatu inayotajwa na katiba. Katika hali hiyo akichaguliwa kuwa Rais mwaka 2025 akafika mwaka 2030 kwa neema za Mungu, basi atakuwa ametumikia kiti cha urais miaka tisa na miezi tisa. Kikatiba hana nafasi ya kuiwania tena kiti hicho, labda lifanyike jambo moja tu. Mabaliko ya katiba ili kuondoa masharti ya sasa ya kikatiba ya kuwania nafasi hiyo kwa mujibu wa ibara ya 40 (4).

Ni kwa kutambua msingi huu, mtu anapaswa kujiuliza, je, Sophia alikuwa amepitiwa kiasi cha kusahau kuwa kuna masharti haya ya kikatiba kuhusu nafasi ya kuwania urais? Na je, kama aliteleza anaweza kusahihisha? Na kama hatasahihisha anataka kualika nini katika mchakato wa kuwania urais katika taifa letu?

Ni vema pia Sophia akakumbuka kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya Watanzania wote, ni makubaliano ya Watanzania walivyoamua kuendesha mambo yao, sasa akitokea mtu mmoja au kikundi cha watu kutaka kubadili makubaliano hayo, inabidi ahojiwe. Kwamba anafanya hayo kwa maslahi ya nani? Je, ametumwa au amejituma mwenyewe? Kwa nini anaanza kuzungumza mwaka 2030 hata kabla ya kuvuka 2025? Anataka kujenga taswira gani?

Si vibaya kujikumbusha tulikotoka. Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 walitokea watu walioasisi maneno yafuatayo “atake asitake” tutamlazimisha kuwania kipindi cha tatu. Ilikuwa ni bahati mbaya sana maneno hayo yalitamkwa na kiongozi mkuu wa muhimili wa Bunge, Spika Job Ndugai, katika akili ya kujituma na kutaka kufurahisha kama siyo kujifurahisha.

Akiwa amekwisha kukolea uvunjifu wa taratibu, sheria na kanuni, Ndugai alimshauri aliyekuwa Mbunge wa Nkasi wakati huo, Ally Kessy, aweke akiba hoja yake kuwa hata kama Rais Magufuli alikuwa hataki kuwania kipindi cha tatu cha urais, basi watamlazimisha kwa kubadili katiba ili aendelee kuwania nafasi hiyo baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na cha mwisho.

Ndugai alimshauri Kessy kuweka kiporo hoja yake, akimsihi kwamba ngoja kwanza waende kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na wakisharejea tena bungeni, basi hoja yake itawekwa mezani ili kuanza mchakato wa ‘kulazimisha’ muhula wa tatu wa Rais Magufuli. Ni kwa nguvu za Mungu hayo yote hayakutokea. Kwanza Kessy hakurudi bungeni, mbili Rais Magufuli alimaliza safari ya maisha yake Machi 17, 2021 na baadaye Ndugai naye aliachia kiti cha uspika takribani mwaka mmoja baadaye, yaani Alhamisi Januari 6, 2022.  Kwa hiyo, Kessy, Ndugai na huyo aliyekuwa anataka kutafutiwa “atake asitake” wote ama hawapo madarakani au duniani.

Job Ndugai.

Nimejiuliza maswali kimya kimya, je, Sophia haijui katiba ya Tanzania kiasi cha kujikuta akitoa kauli hii? Au Sophia anataka kupima upepo?

Nilitahadharisha hapo awali kwamba bara la Afrika limekwamishwa na watu wanaotafuta kura ili kuongoza, lakini wakishapata madaraka walioomba badala ya kuongoza ili kuletea matiafa yao maendeleo, wanaanza upya shughuli ya kutafuta kura, siyo kutafuta maendeleo. Sophia anawaza vipi urais wa mwaka 2030 sasa wakati hata 2025 hatujavuka? Anawaza vipi urais huo wakati yapo mambo makubwa mazito ambayo watawala wa sasa wanapaswa kuyafanyia kazi ili walau wapate uhalali wa kuomba kura 2025, achilia mbali 2030.

Naomba kumuuliza Sophia ni nani amekutuma au umejituma mwenyewe?

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...