Na Mwandishi Wetu, Media Brains
Mfanyabiashara Rostam Aziz kupitia Kampuni ya Taifa Gas ya Tanzania ametangaza uwekezaji mkubwa nchini Zambia wa uzalishaji umeme kwa kutumia Gesi itokanayo na mafuta (LPG).
Kwa mujibu wa Rostam, Taifa Gas itashirikiana na Kampuni ya wazawa ya Delta Marimba Limited kuzalisha megawati 100 za umeme ambao utaingizwa kwenye gridi ya Taifa la Zambia.
Mpango huo wa uwekezaji umetangazwa leo Juni 26, 2023 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na Waandishi wa Habari ambao ulihusisha kampuni hizo mbili.
Mapema, Mkurugenzi wa Kampuni ya Taifa Gas, Hamis Ramadhan alisema uwekezaji huo utakuwa wa kwanza kwa kampuni hiyo kuzalisha umeme kwa kutumi gesi ya LPG nakwamba mradi huo utatekelezwa nchini humo huku ikiangalia fursa nyingine za uwekezaji ikiwemo matumizi ya kupikia kama ilivyo hapa nchini.
“Taifa Gas itafungua kampuni ya kwanza ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia Gesi ya LPG Kaskazi mwa Zambia, mradi huu ukikamilika utazalisha umeme wa MW 100 na kuingiza kwenye gridi ya Taifa la Zambia. Taifa Gas itaongoza uwekezaji kwenye mradi huu nchini Zambia ambao utafikia dola za Marekani milioni 100 (zaidi ya Sh bilioni 240 bilioni.
“Uamuzi huu wa kuwekeza Zambia umechochewa na mazingira mazuri ya uwekezaji na sera madhubuti za Rais Hakainde Hichilema na chama chake cha UPND. Hivyo tunaipongeza Serikali ya Zambia kwa kufanikiwa kupata makubaliano ya deni la nchi hiyo hivyo kupata unafuu mkubwa kwa uchumi wa Zambia,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa Gas, Rostam Azizi amesema: “Tanzania na Zambia zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu, na uhusiano huu unapaswa kuuendeleza kwenye shughuli za kiuchumi na, tuna furaha kubwa kusaidia kuwekeza kwenye sekta ya nishati ya Zambia.
“Zambia ni nchi ambayo kwa sisi Watanzania tumekuwa na historia nao wakati wa shida na raha na mambo yanapokwenda vizuri kwenye uchumi maana yake tunapaswa kutafasiri mahusiano ya nchi mbili hizi kwa kuangalia fursa za kiuchumi,” amesema Rostam na kuongeza kuwa wanatarajia kuongeza zaidi uwekezaji Zambia kwa kutazama fursa zaidi katika sekta ya Nishati na Madini huku akisisitiza juu ya kutunza mazingira.
Naye Padmore Muleya ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya Delta amesema mradi huo unatarajiwa kumakilika ndani ya miezi 24 kuanzia sasa huku akieleza umuhimu wa uwekezaji huo kwa maendeleo ya wana ‘Chipolopolo’
Uwekezaji huo wa Taifa Gas umetangazwa ikiwa ni mwezi takribani mmoja umepita tangu ilipoingia makubaliano na Serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na Kampuni ya Generation Capital Ltd ya nchini Mauritius kuzalisha umeme wa nishati ya jua kiasi cha megawati 180.
Ikumbukwe kuwa kwasasa Zanzibar inapokea megawatt 125 kutoka Tanzania Bara- kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambapo uwezo wake umefikia zaidi ya asilimia 90 na kuanza kwa mradi huo kunaifanya Zanzibar kuanza safari ya kujitegemea kwenye nishati hiyo.