Nisingelifaulu mtihani wa Bashiru


Na Jesse Kwayu

BASHIRU Ally ni mwalimu wa sayansi ya siasa, ni mbobezi wa eneo hilo. Anafahamu nadharia na falsafa nyingi za siasa siyo za Tanzania au Afrika tu, bali duniani. Ni mwalimu, amefundisha wengi. Sasa hivi ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Bashiru kwa umri anaweza kutajwa kuwa ni kundi la kizazi kipya cha uongozi wa CCM.

Katika siku za hivi karibuni umeibuka mjadala mkubwa nchini kutokana na kauli ya Bashiru kwamba ‘CCM inatumia nafuu ya aliye na dola kuitumia dola kubaki madarakani.’ Alifafanua zaidi na kueleza kuwa nafuu ya mwenye madaraka anashika dola, anaitumia dola kubaki kwenye dola. Bashiru amesema ataitumia dola vilivyo kuhakikisha CCM inabaki madarakani. Anaeleza kuiogopa njia ya uzembe waliopita vyama vilivyoleta uhuru Kenya, Kanu na Zambia UNIP, kwani baada ya kutoka madarakani kwa kushindwa kwenye uchaguzi, havijarejea tena.

Bashiru alifafanua nini maana ya kutumia nafuu ya dola kuwa ni kuisimamia serikali itimize wajibu wake wa kuwatumikia wananchi. Kukusanya kodi, kupiga vita rushwa, kusimamia rasilimali za taifa kwa faida ya wananchi. Lakini pia alisema kuwa kutumia nafuu ya dola siyo kukandamiza wapinzani.

Ningelikuwa ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya sayansi ya siasa, Mwalimu Bashiru alete swali la PS 100 juu maana ya nafuu ya mwenye madaraka kutumia dola kubaki madarakani, ni hakika ningelikuwa miongoni mwa wanafunzi ambao wangefeli kama majibu ya swali hilo ni kama alivyoeleza.

Majibu ya Bashiru kuhusu nafuu ya mwenye dola kuitumia kusalia madarani hakika ni jambo linaloweza kuzaa mjadala mpana na kuibua wabobezi wa sayansi ya siasa kuandika machapisho mengi. Kikubwa ambacho Bashiru anaweza kupata nacho nafuu kwa maoni yangu ni kauli kwamba ‘kuisimamia serikali’ ili kama itatimiza wajibu wake basi chama tawala kipendwe na kuendelea kuchaguliwa. Kwa manaa hiyo Bashiru anaweza kuwa anasema ukweli, lakini kwamba chama hicho hakitatumia nafuu hiyo kukandamiza wapinzani wake, kujitengenezea mfumo wa chama kimoja ni jambo ambalo dhamira yake pia iwe huru kufafanua zaidi.

Nitafafanua baadhi ya mambo. Mwishoni mwa mwaka jana kwa mara ya kwanza tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 tulishuhudia uchaguzi wa ovyo kabisa wa serikali za mitaa. Kulikuwa na uhuni mwingi ulioakisi nafuu ya mwenye dola. Wasimamizi wa uchaguzi huo walifanya madudu ambayo huwezi kusadiki kwamba yanafanywa katika nchi yenye uzoefu wa kuendesha chaguzi za namna hiyo kwa zaidi ya miaka 25.

Chaguzi za serikali za mitaa chini ya vyama vingi zilifanyika mwaka 1994, 1999, 2004, 2009, 2014 na huo wa mwaka jana, 2019. Hatujapata kuona wagombea wa vyama vya upinzani takribani wote wakienguliwa ilhali wa chama tawala, chenye nafuu ya dola, wakipitishwa wao tu. Hii nayo ni nafuu ya mwenye dola? Bashiru anaweza kufafanua zaidi.

Nafuu ya mwenye dola haionekani hapo tu. Tangu awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015, haki na uhuru wa kufanya siasa kwa viongozi wa vyama vya siasa vya kambi ya upinzani wenye nyadhifa za kitaifa iliharamishwa. Haki ya kuendesha siasa iliachwa tu kwenye nafasi ya wabunge kwenye majimbo yao ya uchaguzi, nako kwa mbinde. Hii yaweza kuwa pia nafuu ya mwenye dola kwa mujibu wa Bashiru?

Bashiru ni mwanafalsa, ni mjamaa, ni mpenda haki, lakini kuna kitu ama hataki kukisema kwa uwazi na ukweli wake. Kwamba ni kwa jinsi gani siasa za upinzani zimekuwa ngumu kwa kipindi cha miaka takribani mitano sasa? Je, Watanzania siyo wale wale, katiba za vyama siyo zilezile, na je, kuna nafuu gani ya kuwa mpinzani kwa sasa na kumudu kupumua katika uwanja wa siasa.

Bashiru kwa hakika anajua ni kwa jinsi gani wapo watu wapo katika ofisi za umma, yaani watumishiwa umma, lakini matendo yao na mwenendo wa utumishi wao unaakisi ukada wao zaidi kuliko utumishi wa umma. Kutumikia wananchi wote sawa bila kuwabagua kwa misingi yoyote, iwe ya kiitikadi, iwe ya eneo, iwe ya nasaba au chochote kile.

Watumishi hawa wamekuwa na jeuri ya kutenda mambo na kutamka kauli ambazo hakika inawaondolea sifa ya kuwa viongozi wa umma. Wamefanya haya mchana kweupe, wametenda haya kwa kuwa wana nafuu ya dola na chama tawala ni chao. Je, katika hili Bashiru analijua au ni bahati mbaya yamempita.

Ni hakika Bashiru angelikuwa mwalimu wangu ningfeli mtihani wake kwa dhana yake ya “mwenye nafuu ya dola kuendelea kusalia madarakani,”

spot_img

Latest articles

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

TANZANIA KUPAMBANA NA JANGWA

Na Mwandishi wetu Serikali imejipambanua katika kupambana na kuenea kwa jangwa, kurejesha ardhi iliyoharibiwa pamoja...

More like this

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...