CCM miaka 38 si haba, kataa hila


Na Jesse Kwayu

MWISHONI mwa wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilihimisha maadhimisho yake ya miaka 38 tangu kuzaliwa kwake kufuatia kuunganishwa kwa Tanu, iliyokuwa inatawa Tanzania Bara (Tanganyika) na ASP iliyokuwa inatawala Zanzibar.

Maadhimisho hayo yalifanyika wiki ambayo kimsingi ilikuwa imechafua sana taswira ya nchi kutokana na vitendo vya kikatili vilivyopfanywa na askari polisi jijini Dar es Salaam dhini ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CIF), waliookuwa wanataka kuandamana kukumbuka wenzao waliouawa Januari 27, 2001 na polisi visiwani Zanzibar.

Kwa walioona picha za vipigo vya kinyama vya polisi dhidi ya raia, walikumbuka mengi. Mosi, walikumbuka dhahiri mauaji hayo ya Januari 27, 2001 ambayo kwa uchache watu 34 waliuawa. Wengi wakiwa ni kisiwani Pemba, iliko ngome kuu ya CUF.

Ni mauaji ambayo yalisababisha kwa mara ya kwanza tangu uhuru Watanzania kukimbia nchi yao kama wakimbizi na kwenda kuishi nchini Kenya. Ilikuwa ni aibu, imebakia kuwa aibu ya taifa kwamba eti maadamano yanawakera sana watawala kiasi cha kukosa kabisa uvumilivu wa kuona wananchi wakiingia mitaani kwa amani kabisa kuelezea tu hisia zao juu ya mwenendo mzima wa utawala wa nchi yao.

Mvutano uliotokea bungeni kuhusu matendo haya ya kinyama ya polisi dhidi ya raia huku serikali ikionyesha dhahiri kuunga mkono matendo hayo, siyo tu unatoa picha kwamba kama taifa hili bado tuna kazi kubwa ya kuheshimu haki za binadamu, bali pia tunapata fursa nyingine ya kutambua kwamba watawala wangali wanatamani sana uimla na kuepuka kwa nguvu zao zote uwajibikaji.

Kwa hakika kufanyika kwa sherehe za chama tawala wakati kukiwa na madhila kama hayo, ni jambo linalostahili kushughulisha vichwa vya wote wanaoitakia mema nchi hii na watu wake.

Haiingi akilini kwamba chama tawaka kipo kwenye shamrashamra za kukumbuka kuzaliwa kwake, vyombo vya ulinzi kama polisi wafanye wajibu wa kulinda raia na mali zao, vinaendesha vipigo vya kiwango kile. Huu kwa hakika ulikuwa ni upungufu kwa yeyote aliagiza wananchi kupigwa kwa staili ile. Ni jambo lisilokubalika katika zama za utawala wa sasa wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Tukiachana na aibu hiyo, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alihutubia taifa katika sherehe hizo. Alizungumza mengi. Nitajishughulisha tu na suala la mbio za urais kupitia chama chake.

Ni jambo jema kwamba sasa imeingia sawasawa katika akili ya Kikwete kwamba muda wake wa kukaa ikulu umekwisha. Ndiyo maana anazungumza wazi kwamba suala la mrithi wake na kukumbushia kanuni za kuzingatiwa.

Katika hotuba hiyo Rais Kikwete aligusia kwamba CCM itatatoa wagombea wenye sifa zisizotiliwa shaka kwenye ngazi zote, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, ubunge na uwakilishi.

Lakini pia aliwataka wanachama kama wanaoona w anachama walioanza kujitokeza kuwania uteuzi wa urais hawana sifa, wasisite kushawishi watu wengine wenye sifa wajitokeze kuchukua fomu.

Katika hotuba hiyo Kikwete alitoa angalizo kwamba wagombea wote watapimwa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na maadili ya chama hicho. Pia ambao hawatazingatia maadili ya chama wasije kumlaumu mtu bali wajilaumu wenyewe.

Rais Kikwete atakuwa ni Rais wanne wa Tanzania kusimamia mchakato wa kukabidhi madaraka ya dola kwa njia ya kidemokrasia kwenda kwa rais mwingine.

Wa kwanza kufanya hivyo alikuwa ni Mwalimu Nyerere. Alifanya hivyo mwaka 1985 alipoondoka madarakani kwa hiari yake na kumwachia Ali Hassan Mwinyi wakati wa mfumo wa chama kimoja. Lakini pia kwa kiasi, Mwalimu alihusika katika kupitishwa kwa Benjamin Mkapa mwaka 1995 kuwa mgombea urais, ingawa pia Mwinyi alishiriki.

Mwaka 2005 Rais Mkapa alikuwa nguzo katika kusimamia mchakato wa kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine, ni mchakato uliohitimishwa kwa Kikwete kuteuliwa na CCM kuwania urais.

Historia inaonyesha kwamba tangu kuanza kwa utaratibu wa kidemokrasia wa kuachiana madaraka, hasa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi mkuu kufanyika mwaka 1995, haijapata kutokea, siyo 1995 wala 2005 kwa chama kuhusika moja kwa moja na hujuma za dhahiri na za chini chini kushughulikia makada wake kwa kuwa tu wameonekana wana nguvu.

Kwa kipindi cha miaka mingi sasa, hasa kuanzia mwaka 2009 juhudi hizi zimelenga kuwaumiza baadhi ya makada, lengo kuu likiwa ni kuwandoa kwenye mstari wa kuwania nafasi ya juu ya uongozi wa nchi kupitia chama tawala.

Kumekua na kampeni hizi, na hata wakati mwingine wapo watu wameibua maswali, hivi Rais Kikwete ana mgombea wake hata kabla ya mchakato wa uchujaji wagombea wa chama kufanyika?

Majuzi hapa, kwenye hotuba yake Rais Kikwete alisema chama kina utaratibu unaoeleweka na kutabirika wa kupata wagombea. Kwamba CCM ni chama kilichokomaa na imara. Kina kanuni na vigezo. Kina vikao rasmi vya kuchuja na kuchangua wagombea. Kwa maana hiyo, aliwahakikishia wanachama wake kwamba hapataharibika jambo.

Ninataka kusadiki kwamba angalizo na hakikisho hili ni la dhati kutoka kwa Rais Kikwete ili pamoja na mambo mengine tabia hii inayotaka kuota mizizi ya kuwindana, kuzungukana na kujengeana fitina katika kusaka uongozi ufike mwisho.

Ni matumiani ya wengi kwamba CCM kama alivyosema Rais Kikwete akiwa ni mwenyekiti wake, kimekomaa kweli, kitafuata kanuni zake, kitazingatia maadili yake, kitafuata utaratibu na kuzingatia katiba yake. Kwamba haki itatamalaki.

Lakini wakati CCM ikijikita katika mambo hayo yote ambayo ni misingi yake, ni lazima sasa kiwe na ujasiri na udhubutu wa kusema kwamba kama chama kinaendesha je mambo yake kwa maana ya vyanzo vya mapato? Ghama zake zinalipiwa na nani kwa njia ya wazi kabisa?

Kwamba tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, CCM imekuwa na mfumo gani wa haki, kweli na uwanja sawa kwa wanachama wake wote katika kushindana kusaka nafasi za uongozi?

Je, ni lini CCM ilikataa fedha kama moja ya kigezo cha kujipanga, kujitayarisha kwenye harakati za kisiasa? Je, tangu kuachwa kwa mfumo wa kutafuta kura chini ya mfumo wa chama kimoja, ambako wagombea ubunge walikuwa wanahutubia mkutano mmoja wa kampeni kwa pamoja, kusafiri kwenye gari moja kwa pamoja kwa sasa ni upi ulioko wa kuweka uwanja sawa?

Inawezekana kwamba kadri joto la uchaguzi linavyopanda ndivyo hadhari inachukuliwa, lakini kuchukua hadhari hizi CCM itakuwa inajikangaa kwa mafuta yake yenyewe kama itafikiri fitina na ghilba zitaivusha.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...