BRELA YAIBUA FURSA MPYA ULINZI WA ALAMA ZA BIASHARA KWA WAJASIRIAMALI

Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutumia fursa ya uwepo wa BRELA kwenye maonesho hayo kwa kupata huduma za sajili na leseni ili kujiendesha kwa mujibu wa sheria na kuepuka changamoto za kisheria.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 10, 2026 na Afisa Usajili wa BRELA, Benedickson Wilson, akitoa mafunzo kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara kwa wajasiriamali wanawake katika banda la Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) na banda la Wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma katika Maonesho hayo jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia Sheria ya Alama za Biashara na Huduma, Bw. Wilson alisema usajili wa alama humpa mmiliki haki ya kipekee kuitumia na kumlinda dhidi ya mtu mwingine anayeweza kuitumia bila idhini au kusajili alama inayofanana na kusababisha mkanganyiko sokoni.

“Usajili wa alama hufanyika kulingana na aina ya biashara, ambapo kuna madaraja 45 ya bidhaa na huduma, kwa mfano, mfanyabiashara wa vipodozi atasajili alama katika Daraja la 3. Baada ya usajili mmiliki anapata haki ya kipekee ya kuitumia na kumzuia mtu mwingine kuitumia bila ruhusa.” alibainisha Bw. Wilson.

Bw. Wilson aliongeza kuwa usajili wa alama unasaidia kutofautisha bidhaa au huduma za mzalishaji mmoja na mwingine, hivyo kuongeza ushindani wa haki na kuwalinda watumiaji dhidi ya mkanganyiko unaoweza kutokea pindi wanaponunua bidhaa sokoni.

Aidha, alisema endapo mfanyabiashara mmoja atakuwa amesajili alama yake na mwingine akaitumia au akasajili alama inayofanana bila idhini, mwenye alama iliyosajiliwa ana haki ya kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Biashara na Huduma.

Kwa upande wao, baadhi ya wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kuongeza uelewa wa hatua za kurasimisha biashara na faida za kusajili majina yao ya biashara pamoja na faida za kulinda alama zinazotambulisha bidhaa zao kwenye soko.

“Nilikuwa sifahamu vizuri huduma za sajili na leseni kutoka BRELA, lakini leo kupitia haya mafunzo nimeelewa umuhimu wa kutumia huduma za BRELA kusajili jina la biashara na alama yangu, nimefahamu pia usajili wa jina unaweza kukamilika ndani ya siku moja na kupata cheti changu cha usajili, tunawashukuru sana BRELA kwa elimu hii,” alisema Bi. Melania Shawa.

BRELA inaendelea kutoa elimu na huduma kwa washiriki wa Maonesho ya Sabasaba kupitia mabanda yake mawili; banda kuu lililopo karibu na Banda la Wizara ya Fedha na lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara. Wananchi na washiriki wa maonesho wanakaribishwa kutembelea mabanda hayo ili kupata elimu zaidi pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na BRELA hadi siku ya kilele cha maonesho hayo tarehe 13 Julai, 2026.

spot_img

Latest articles

TTB yakutanisha wadau kujadili mustakabali wa Destination Tanzania

Na Mwandishi Wetu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya...

Sangweni: Sekta ya Mafuta na Gesi Ni Chachu ya Ukuaji wa Uchumi wa Taifa

Na Mwandishi Wetu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli...

VETA Kihonda yaja ‘cold room’ kupunguza upotevu wa mazao ya wakulima

Na Mwandishi Wetu UBUNIFU wa mfumo jumuishi wa kuhifadhi mazao kwa kutumia teknolojia ya ubaridi...

Ofisi ya Msajili wa Hazina yalenga kukusanya Sh2 trilioni mwaka 2026/27

Na Mwandishi Wetu OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) imejiwekea lengo la kukusanya Sh2...

More like this

TTB yakutanisha wadau kujadili mustakabali wa Destination Tanzania

Na Mwandishi Wetu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya...

Sangweni: Sekta ya Mafuta na Gesi Ni Chachu ya Ukuaji wa Uchumi wa Taifa

Na Mwandishi Wetu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli...

VETA Kihonda yaja ‘cold room’ kupunguza upotevu wa mazao ya wakulima

Na Mwandishi Wetu UBUNIFU wa mfumo jumuishi wa kuhifadhi mazao kwa kutumia teknolojia ya ubaridi...