Na Mwandishi Wetu
MHITIMU wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA, Ernest Maranya, amebuni na kutengeneza mashine za kuongeza thamani ya mazao mbalimbali ya kilimo, hatua iliyomwezesha kujiajiri kwa kuanzisha kampuni inayotengeneza teknolojia za usindikaji wa mazao.
Maranya amesema kampuni yake yenye makao makuu jijini Dar es Salaam inatengeneza mashine za kusindika mazao mbalimbali, ikiwemo karanga, kahawa na karafuu, kwa lengo la kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa zao kabla ya kuzipeleka sokoni.

Amesema mashine hizo huchakata mazao kwa ufanisi, jambo linaloboresha ubora wa bidhaa na kuongeza thamani yake sokoni, hivyo kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wadogo kupata faida zaidi.
Kwa mujibu wake, tayari ametoa huduma kwa wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Mbeya, ambapo baadhi yao wamefanikiwa kuanzisha au kupanua shughuli zao za uzalishaji kwa kutumia mashine hizo.
Maranya amesema ujuzi alioupata kupitia mafunzo ya VETA ndio uliomuwezesha kubuni mashine hizo na kuanzisha biashara yake, badala ya kusubiri ajira rasmi.

Amewahimiza vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi, akisema huwapa ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri, kubuni teknolojia na kuanzisha biashara zinazotoa suluhisho kwa jamii.
Aidha, amesema mafanikio aliyoyapata yanaonesha kuwa ujuzi unaotolewa na VETA unaweza kuwa msingi wa kujikwamua kiuchumi, huku akiwataka vijana kuitumia fursa hiyo kwa bidii, ubunifu na kujituma.


