Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI wa mpira wa wavu ‘volleyball’ wanaoshiriki Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kutumia jukwaa hilo kuonyesha vipaji vyao ili kujiongezea nafasi ya kuonekana na mawakala, timu za ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Ligi ya Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA), Joseph Mwaduwa wakati huu ambao ligi hiyo inaendelea.
Mwaduwa amesema ligi hiyo imekuwa daraja muhimu kwa wachezaji wanaotamani kufikia timu za taifa na kupata fursa za kucheza kimataifa.

Amesema wachezaji wanapaswa kujituma na kuonyesha uwezo wao kila wanapopata nafasi ya kucheza kwani mawakala na wadau mbalimbali wa mchezo huo wanafuatilia maendeleo ya wachezaji kupitia mashindano ya ligi.
“Niwaombe wachezaji watumie vizuri nafasi hii ya ligi kuonyesha vipaji vyao. Kupitia ligi wanaweza kuonekana na kupata nafasi ya kuitwa katika timu ya taifa au hata kusajiliwa na klabu za nchi jirani na nyingine za nje ya Tanzania,” amesema.
Ameeleza kuwa ligi ya mwaka huu imekuwa bora kutokana na maandalizi yalifanyika tofauti na mwaka jana.


