Tusimamie sera ya kutofungamana, pia uwajibikaji matukio ya Oktoba 29

SIJAWAHI kuwa msemaji wa serikali, hivyo sina utaratibu wa kuizungumzia au kuisemea. Siyo jukumu langu. Jukumu langu kubwa ni kuiuliza maswali ili wananchi wajue nini kinaendelea katika nchi yao.

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, kuna siku nililazimika kuisemea serikali. Nilikuwa katika kikao kimojawapo nikatakiwa nieleze ninafikiri ni kwa nini Serikali ya Tanzania haikuunga mkono azimo la kuiwekea vikwazo Urusi (Russia) baada ya kudaiwa kuivamia Ukraine.

Tanzania ilijizuia (abstain) kupiga kura wakati wa upigaji kura wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililolaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Machi 2, 2022. Azimio hilo, lililojulikana kama Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ES-11/1, lilitaka Urusi kusitisha mara moja matumizi ya nguvu na kuyaondoa majeshi yake Ukraine.

Matokeo ya kura yalikuwa: Nchi 141 zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo; nchi tano zilipiga kura kupinga; na nchi 35, ikiwemo Tanzania, zilijizuia kupiga kura. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika zilizochagua kutounga mkono wala kupinga azimio hilo.

Baadaye mwaka 2022, Tanzania pia ilijizuia kupiga kura katika baadhi ya maamuzi mengine ya Umoja wa Mataifa yaliyohusiana na Ukraine, ikiwamo kura ya kuisimamisha Urusi kutoka kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN Human Rights Council).

Katika mazingira yale, nilijitahidi kueleza kile ambacho serikali ilifanya. Kwanza nilisema Tanzania na Urusi tangu zama za Muungano wa Nchi za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) ilikuwa mshirika mkubwa wa Tanzania katika misaada ya elimu na ulinzi. Kwamba USSR ilisaidia juhudi za Waafrika kupambana dhidi ya ukoloni. Nikasema ukizingatia Tanzania ilikuwa kinara katika mapambano ya kutokomeza ukoloni kusini mwa Bara la Afrika, msaada wa USSR ulikuwa na manufaa makubwa katika kufanikisha ndoto ya Waafrika kujikomboa kwenye makucha ya ukoloni.

La pili, nilijielekeza kwenye sera ya mambo ya nje ya Tanzania kwamba kama ilivyokuwa wakati ule, hata leo, bado ni ile ile ‘kutofungamana na upande wowote’. Tanzania ni miongoni mwa kundi la Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Alignment Movement -NAM) – huu ni ushirika wa kimataifa unaojumuisha nchi ambazo zilichagua kutofungamana rasmi na, wala kupinga, kambi yoyote kubwa ya nguvu za kisiasa duniani, hususan wakati wa Vita Baridi. Kwamba mpaka leo, Tanzania bado inashikilia msimamo huo wa sera ya nje.

Ninakumbuka sikueleweka wala kuwafurahisha wauliza swali. Sikueleweka kwa sababu majibu yangu hayakuwa ndiyo tarajio lao. Tulizima koleo, kusubiria mambo mengine.

Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kiserikali nchini Urusi. Amekuwa Rais wa pili kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitembelea Urusi baada ya zama za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alipata kufanya ziara hizo mara kadhaa. Chini ya marais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwingi; Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa; Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Awamu ya Tano, John Magufuli, hakuna ziara ya kiserikali ilifanywa na viongozi hao Urusi.

Katika miaka ya hivi karibuni mahusiano ya kitaifa yamegubikwa na mambo mengi. Ingawa vita baridi vilikwisha baada ya kusambaratika kwa dola ya USSR Desemba 1991, kumekuwa na dalili za siasa za kibabe zaidi katika mahusiano ya kimataifa. Kumekuwa na kulazimishana mwelekeo katika zama hizi mpya ambazo kuna kila dalili ya ongezeko la mivutano mikubwa zaidi ya mataifa yenye nguvu – wakiongozwa na Marekani kutokuheshimu uhuru wa mataifa mengine.  

Katika nyakati hizi, ziara ya Rais Urusi inaweza kuamsha shauku na maswali kutoka kwa washirika wa maendeleo kutoka magharibi. Hawa wakiongozwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, wana vigezo vyao vingi vya kuzingatia katika mahusiano vikiwamo utawala bora na demokrasia.

Kwa tathmini ya haraka, ziara hii inatazamwa na wengi kama Tanzania kuendelea kubakia katika njia yake. Hii ni kwa sababu kuna faida za kidiplomasia (anga za kimataifa) na matokeo chanya ya kiuchumi.

Ziara hii inathibitisha kuwa Tanzania inaendeleza urithi wa kutofungamana na upande wowote (non-alignment). Ziara kama hii inaonyesha kwamba Tanzania ina uhusiano na Mashariki na Magharibi. Hatua hiyo inatoa nafasi ya “kujitegemea kimkakati” katika sera ya nje na pengine kuongeza ushawishi wa Tanzania kimataifa. Kwa kawaida kwa miaka mingi Tanzania imeonekana kama nchi yenye sauti huru kwenye masuala ya kimataifa. Kwa maana hii inaonyesha kuwa inao uwezo wa kushiriki majadiliano ya dunia bila kushinikizwa na upande mmoja.

Pengine faida kubwa ya ziara hii ni kupanua fursa za kiuchumi kwa Tanzania. Urusi ni taifa lenye nguvu kubwa katika nyanja za nishati, ulinzi, na teknolojia. Kwa hiyo mikataba iliyosainiwa inaweza kutoa msukumo mkubwa wa kiuchumi kwa Tanzania.

Pia kuna fursa za kibiashara na uwekezaji zinakwenda kufunguka kama masoko ya bidhaa za kilimo, madini, na bidhaa za baharini pamoja na uwekezaji kutoka makampuni ya Urusi. Hapa ndipo suala la teknolojia ya nishati hasa nyuklia ya amani inatazamwa kama mwarobaini wa kukabiliana na mahitaji makubwa ya nishati ya umeme.

Kwa miaka na miaka Urusi imekuwa inatoa fursa za masomo kwa maelefu ya Watanzania. Ziara hii huenda ikapanua mlango huo.

Hata hivyo, Tanzania inapaswa kujipanga na kujipima sawasawa katika mizania mpya ya mahusiano ya kimataifa duniani kwa sasa. Kikubwa ni uwezekano wa kuibuka kwa shinikizo kutoka nchi za Magharibi – Marekani na EU. Kwa sasa mataifa hayo hayatazamani usoni na Urusi kutokana na vita vya Ukraine. Hii inaweza kusababisha Tanzania kuchukuliwa kama mtoto mtukutu na pengine imeamua kuchagua upande katika mgogoro wa Ukraine na Urusi.

Ukisikiliza kauli za nchi za magaharibi kuhusu Urusi ni dhahiri zingependa kuona ikitengwa na nchi zote duniani. Kumekuwa na juhudi kubwa za kushawishi, na shinikizo kubwa la kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi kwa sababu ya vita vya Ukraine.

Kinyume na kilichotarajiwa kuwa vita hiyo ingechukua muda mfupi sana baada ya nchi za magharibi kuamua kuisadia Ukraine, sasa imevuka miaka minne. Ni mzigo mkubwa kwa nchi za magharibi kiuchumi, ni mgogoro mkubwa wa kidiplomasia na mahusiano ya kimataifa, pia ni jambo ambalo mataifa haya yanatumia kutafuta washirika na kinyume chake.

Tayari Tanzania inakabiliwa na shinikizo kubwa huko nje linalotokana na suala la uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Umoja wa Ulaya uko kwenye mchakato wa kuzuia misaada ya maendeleo kwa Tanzania kutokana na uchaguzi huo, nako Marekani upo muswada wa sheria unaochakatwa kulenga baadhi ya viongozi wa serikali ya Tanzania kutokana na matukio hayo ya Oktoba 2025.

Haya ni mambo yanayoweza kutuathiri kwenye njia kuu ya kuiendea Dira ya Maendeleo ya 2050 kwa ukamilifu wake. Hali yetu kama taifa huko nje haijatulia. Tunatuhumiwa pakubwa hasa kutokana na matukio ya Oktoba 29, 2025. Hiki ndicho kipindi cha kuwa na wanadiplomasia nguli wa kufanya kazi, lakini pia tukumbuke kwa mioyo hakutakuwa na mafanikio ya maana kama hakutakuwa na uwajibikaji kwa yale yaliyotokea nchini wakati wa uchaguzi mkuu. Bila uwajibikaji kwa yaliyotokea Oktoba 29, 2025, tutajichosha sana.

spot_img

Latest articles

DAWASA, Madiwani waja na suluhisho changamoto ya maji Ubungo

Na Mwandishi Wetu Madiwani wa Manispaa ya Ubungo wamekubaliana kwa kauli moja na Mamlaka ya...

Dawasa, madiwani Ubungo ziarani kutafuta suluhu ya maji

Na Mwandishi Wetu Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe Albert Msando, ameongoza ziara maalum...

Mchezo wa kuogelea wazidi kupaa nchini, TSA  yafichua siri

Na Winfrida  Mtoi MCHEZO wa kuogelea umezidi kushika kasi nchini  kutokana na kuongezeka idadi ya...

Dkt Nchimbi atembelea banda la Tanesco

Na Mwandishi Wetu MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi...

More like this

DAWASA, Madiwani waja na suluhisho changamoto ya maji Ubungo

Na Mwandishi Wetu Madiwani wa Manispaa ya Ubungo wamekubaliana kwa kauli moja na Mamlaka ya...

Dawasa, madiwani Ubungo ziarani kutafuta suluhu ya maji

Na Mwandishi Wetu Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe Albert Msando, ameongoza ziara maalum...

Mchezo wa kuogelea wazidi kupaa nchini, TSA  yafichua siri

Na Winfrida  Mtoi MCHEZO wa kuogelea umezidi kushika kasi nchini  kutokana na kuongezeka idadi ya...