Na Mwandishi Wetu
MAPAMBANO dhidi ya upotevu wa maji yamepokelewa vyema na uongozi wa Mkoa wa Pwani, huku Mkuu wa Mkoa huo, Mheshimiwa Aboubakar Kunenge, akitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuongeza kasi ya maboresho ya huduma ya maji ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka kutokana na kasi ya uwekezaji na ukuaji wa viwanda mkoani humo.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa kikao kati ya uongozi wa Mkoa wa Pwani na Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang’ingo, aliyefuatana na Afisa Mtendaji Mkuu pamoja na Menejimenti ya Mamlaka kwa lengo la kujadili namna bora ya kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Pwani.

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Kunenge amesema Mkoa wa Pwani unaendelea kukua kwa kasi, jambo linaloongeza mahitaji ya huduma ya maji kwa wananchi, taasisi na viwanda, hivyo kuitaka DAWASA kuendelea kujipanga kimkakati ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa uhakika wa sasa na wa baadaye.
“Nikushukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa ziara yako hii ya kujitambulisha rasmi kwa uongozi wa Mkoa. DAWASA endeleeni kujipanga vyema ili kukidhi mahitaji ya wananchi na viwanda katika Mkoa wa Pwani, jambo ambalo nina imani mna uwezo wa kulitekeleza,” amesema Mheshimiwa Kunenge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang’ingo, ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Pwani kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka, huku akiweka wazi kuwa agenda kubwa ya DAWASA kwa sasa ni kupambana na upotevu wa maji unaosababishwa na uchakavu wa miundombinu pamoja na vitendo vya wizi wa maji.

“Nikushukuru sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano mnaotupatia. Tunaomba ushirikiano huu uendelee hasa katika ulinzi wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha huduma hii inakuwa endelevu kwa wananchi. Aidha, suala la upotevu wa maji ni agenda namba moja ya DAWASA kwa sasa na kwa pamoja tutamaliza changamoto hii,” amesema Mhandisi Mwang’ingo.
DAWASA imeeleza kuwa imejipanga kushusha kiwango cha upotevu wa maji hadi kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha huduma ya majisafi kwa wakazi wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.


