MSINGI ni neno linalobeba maana kubwa katika mambo mengi. Katika ujenzi iwe wa barabara au nyumba, msingi ni kitu cha umuhimu wa kipekee ili kufanikisha hicho kinachotakiwa kujengwa. Msingi ni kila kitu, ukikosewa iwe katika ujenzi, iwe katika malezi, iwe katika elimu, iwe katika mahusiano, kila mahali, basi hicho kitakachofuata kitakuwa na hitilafu kubwa. Kitaharibika. Hakitastawi kama ilivyotarajiwa.
Jumatatu wiki hii, yaani Mei 18, 2026 ilitangazwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Tume hii imeundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, chini ya mamlaka aliyonayo kwa Sheria ya Tume ya Uchunguzi Sura ya 32. Tume hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Vurugu za Oktoba 29, 2025 zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na baada ya hapo.
Tume ya Uchunguzi wa Kijinai inaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Jaji Shabani Ally Lila. Ina wajumbe watatu ambao wote ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Hawa ni Jaji Mstaafu Gad John Mjemmas, Jaji Mstaafu Awadh Mohamed Bawazir na Aishiel Nelson Sumari. Tangazo la uteuzi huo ambalo lilitolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka, halikueleza muda wa uhai wa Tume hiyo.
Tume hii ya Jaji Lila ni ukuta unaojengwa kwenye msingi ulioandaliwa na Tume ya awali ya kutambua vyanzo vya vurugu za Oktoba 29, 2025 iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Othman Chande. Kama taarifa kwa vyombo vya habari inavyoeleza Tume ya Jaji Lila ni utekelezaji mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande.
Sasa kama Tume ya Jaji Chande ndiyo msingi wa Tume ya Jaji Lila, basi ni haki kabisa kutafakari juu ya uhusiano wa Tume hizi mbili. Ya Chande ni msingi, na ya Lila ni ukuta unaojengwa juu ya msingi huo. Bila kuingia katika mjadala wa kutafakari wajumbe wa Tume ya Jaji Lila, wala kuingia katika kutoa hukumu juu ya uwezo wao au uadilifu wao, kwa maana siyo busara kutoa hitimisho la kitabu kwa kuangalia tu jalada lake, yafaa kukumbuka na kuangalia jinsi ripoti ya Tume ya Jaji Chande ilivyopokewa na wananchi – watu.
Hakuna ubishi kabisa kwamba tukio la Oktoba 29, 2025 lilikuwa ni tukio la kisiasa ambalo lilizaa maafa. Ni tukio ambalo kwa vyovyote litakavyoangaliwa, halitaweza kuzaa matokeo chanya kwa kudhani kwamba mbio zipigwe zaidi kwenda kwenye kusaka ‘ujinai’.
Nitafafanua kidogo. Kwa yeyote mwenye kuitakia nchi hii mema atagundua kwamba sura ya mijadala ndani ya jamii, kwenye mitandao ya kijamii na hata miongoni mwa makundi ya wasomi na wanazuoni, inaonyesha kwamba ripoti ya Tume ya Jaji Chande imewakatisha tamaa wengi. Ni kama vile kile ambacho watu licha ya kuwa na shaka juu ya uhuru (independence) wa baadhi ya wajumbe wa Tume ya Jaji Chande, waliamua kusubiri kuona labda, itawaletea jambo la muhimu juu ya kilichotokea Oktoba 29, 2025 na kwamba taifa lingetoka vipi katika mkwamo ule ambao ni wa kwanza na wa kihistoria nchini kwa vyombo vya dola kuwakabili wananchi kwa mitutu ya bunduki kwa kiwango cha ukatili ulioshuhudiwa.
Kwamba pamoja na ubobevu wa wajumbe wa Tume ya Jaji Chande, ripoti yake (hotuba) aliyoisoma mbele ya Rais Samia Aprili 23, 2026 Ikulu Dar es Salaam, iliacha maswali makubwa na magumu kuliko majibu.
Hali hii ndiyo imekuwa chanzo cha minong’ono, malalamiko, shutuma, lawama na kurushiana mpira kuhusu suala la uwajibikaji. Hasa uwajibikaji wa kisiasa. Tangu siku ya kwanza, umma ulikuwa unalilia kuona hata chembe ya uwajibikaji wa kisiasa. Kiu na shauku hii ilizimwa na kuzikwa mazima siku ripoti iliposomwa mbele ya Rais Ikulu ya Dar es Salaam.
Kwa mfano, ukipitia tamko la Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) lenye pointi 53; au ukapitia tamko la la Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) lenye pointi kuu 29 kuhusu udhaifu wa ripoti ya Tume ya Jaji Chande; au ukasikiliza mahojiano ya wiki iliyopita ya Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba, sauti pekee ya wazi ya wastaafu inayothubutu kuzungumza bila kumung’unya maneno, akihojiwa na Mwandishi wa Habari Nguli, Jenerali Ulimwengu, utaona anavyoiona ripoti ya Jaji Chande. Warioba anaonyesha mambo mengi ya msingi ya kuangaliwa kwa sasa ili kulitibu taifa. Anaonyesha wazi kwamba kitendo cha ripoti ya Tume ya Jaji Chande kutotolewa kwa umma, ili kuruhusu watu kuisoma kwa kina inajenga picha kwamba kuna kitu kinafichwa! Ni hatari.
Kwa maneno mengine, ufuatiliaji wa mijadala mbalimbali unaonyesha kwamba wananchi- watu hawajui undani wa ripoti ya Jaji Chande. Watu wanaibua maswali magumu ambayo hayana majibu. Watu wametafuta kujua ni kwa nini Rais ameamua kuikalia ripoti na kusema ni yake, kwa kuwa yaliyotokea yaliwafika Watanzania. Walioumia ama kwa kuuawa kinyama, ama kwa kujeruhiwa, ama kwa kuharibiwa mali, ama kwa kuletewa matatizo ya kisaikolojia ni Watanzania. Kwa maana hiyo, Watanzania, walau wale wenye ubavu na uthubutu wa kusoma, kama UDASA, TLS, Waandishi wa Habari, wanaharakati, vyama vya siasa, wangelipata fursa ya kujua hasa ni kitu gani Tume ya Jaji Chande ilikutana nacho.
Mlango huo umefungwa. Na umefungwa moja kwa moja, sasa umefunguliwa mwingine wa Jinai.
Katika mazingira haya, swali moja linaibuka, kama msingi wa Tume ya Jaji Lila haujulikani sawasawa kwa wananchi – kwa kufichwa kwa ripoti ya Jaji Chande; na kama ambavyo hisia na mwelekeo wa mjadala kuhusu ripoti (hotuba) ya Jaji Chande ilivyopokewa, watu kutokuiamini, ni kwa jinsi gani sasa kazi ya Tume ya Jinai ya Jaji Lila inakwenda kukubalika kwa umma?
Katika kujisokota huku kwa Tume juu ya Tume hata kama ile ya awali ya kuweka msingi haijaeleweka na imeacha maswali mengi kuliko majibu, umma utarajie nini, kuvuka au kutumbukia zaidi katika hatua ya sasa ya Tume ya Jaji Lila?


