Tume Jaji Chande imekwepa kututajia aliyekutwa na ngozi ya ng’ombe

NINGALI ninaitafakari ripoti ya Jaji Mohammed Chande ya matukio ya Oktoba 2025 wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge kwa tahadhari kubwa sana. kinachonisukuma kuwa na tahadhari hiyo ni vitu viwili. Mosi, ni kama kazi yenyewe ya kukabiliana na yaliyotokea ndiyo kwanza inaanza. Pili, kuna mambo yamefungwa kitaalam sana kwenye ripoti kiasi kwamba inahitajika tafakari pana sana kuyaelewa kwa nini yamefungwa hivyo.

Kabla sijafika mbali katika uchambuzi huu, niseme neno moja, kwamba Tume imetupa walau kwa uchache mawanda ya mauaji yaliyotokea. Kwamba waliuawa watu 518. Tume imesema idadi hii siyo ya mwisho. Inaweza kuongezeka. Kwa maana hiyo, kama taifa sasa tupo kwenye ukurasa mmoja. Watu kwa mamia waliuawa kinyama kabisa kati ya Oktoba 29, 2025 hadi Novemba 3, 2025. Hili sasa halina ubishi. Kwamba wale waliokuwa wanafumba idadi ya vifo kwa kisingizio chochote, sasa watulie tuingie hatua ya pili, kukabiliana na machungu ya uwajibikaji.

Hadi sasa hakuna uwajibikaji wowote umetokea. Hili ni kwa sababu kama alivyosema Jaji Chande mwenyewe na Tume yake ya watu weledi kabisa, hadidu za rejea walizokuwa wanafanyia kazi ziliwapeleka kwenye kazi moja kubwa, kubaini vyanzo vya vurugu. Ilikuwa ni kubaini zaidi kuliko ‘kumwamba yeyote msalabani’. Kwa mantiki hii, kazi iliyoko mbele ni kubwa na ngumu zaidi katika kufikisha mwisho matukio ya Oktoba 2025. Ni ngumu sana kama nia ya kutibu taifa ipo!

Hata hivyo, leo nijiruhusu kujadili mambo machache kwa undani. Mojawapo ni hili ambalo Tume imesema kulikuwa na kambi za mafunzo ya jinsi ya kufanya vurugu siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Na kwamba mafunzo haya yalifanyika kwa kitambo kidogo ndani ya nchi. Kwamba wapo watu walikuwa wanatumia ushawishi wa fedha, kujenga kikosi cha kuendesha uovu siku ya uchaguzi. Kwamba watu hao walikuwa nchini, wanaendesha ‘uovu’ wao. Wengine walikuwa kwenye nyumba karibu kabisa na kituo cha polisi.

Kwa hakika, eneo hili limenisumbua sana. Limenisumbua sana kwa sababu moja tu. Hivi uwezo wa vyombo vya usalama kuchunguza mambo siku hizi umeenda wapi? Hivi, ile Jeshi la Polisi kila siku linaposema wana taarifa za kiintelijensia kwamba ukifanyika mkutano wa hadhara au maandamano kutakuwa na uvunjaji wa amani, na hivyo kuzuia vitu hivyo kufanyika, hii intelijensia ilienda wapi? Yaani watu wapo ndani ya nchi, wanapanga uhalifu, tena karibu na kituo cha polisi. Watu wanapita vyuoni, mitaani kurecruit watu, intelijensia ya polisi haijui kabisa?

Ukimsikiliza vema Jaji Chande ameifanyia rejea mara kadhaa ripoti nyingine ya Tume ya Haki Jinai ambayo pia alikuwa Mwenyekiti wake. Katika ile ripoti masuala ya utendaji na uadilifu wa Jeshi la Polisi yamejadiliwa kwa kina. Na moja ya hitimisho muhimu sana katika suala hili ni kuundwa upya kwa ‘Jeshi la Polisi’. Kuna watu huwa hawaelewi tunapozungumza habari ya Jeshi la Polisi. Wapo wanaodhani kwamba labda tuna chuki na Jeshi hili, au huenda tuna ajenda mbaya dhidi yake. Ukweli ni kwamba uimara, uadilifu na uaminifu wa Jeshi la Polisi ni nguzo kuu ya kujengwa kwa jamii inayoheshimu haki za watu.

Ni nguzo muhimu inayofanya amani ndani ya taifa kuwa na maana kwa kuwa watu wana uhakika na haki zao. Watu wana uhakika na ulinzi wa maisha na mali zao. Watu wana uhakika hawataonewa wala kupokwa haki zao kwa njia yoyote ile.

Kwa bahati mbaya, tangu ripoti hiyo ilipokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Julai 2023, ni vigumu mno leo kueleza kwa yakini ni kwa kiwango gani mapendekezo ya Tume hiyo yametekelezwa kuhusu Jeshi la Polisi.

Tume ya Haki Jinai ilipendekeza hivi: “Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayowezesha Jeshi hilo kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo; Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service) ili kutoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi; Kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi (police force) kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service ); Jeshi la Polisi liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi na Jeshi la Polisi liimarishe huduma za Intelijensia ya jinai na Polisi Jamii na kuanzisha programu za kuisogeza zaidi kwenye jamii.”

Haya mapendekezo yamo kwenye ripoti ya Tume ya Haki jinai mpaka sasa. Wiki iliyopita, Jaji Chande amefanya rejea ya ripoti hii. Miaka miwili na miezi mitatu, walau kungelikuwa na kitu cha kutekelezwa, inawezekana sana matukio ya Oktoba 29, 2025 yasingelikuwapo. Kwa nini? Kwa sababu Jeshi hilo ambalo ndilo linategemewa na taifa kufanya uchunguzi wa matukio yote ya kiuhalifu nchini, lingekuwa walau limepata taarifa za awali juu ya wapanga mikakati yote kama ambavyo ripoti ya Matukio ya Oktoba 2025 imeainisha.

Ukifanya rejea ya ripoti ya Tume ya Haki Jinai jinsi umma unavyoliona Jeshi la Polisi kwamba: Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi. Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio. Hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.

Jaribu kupima maneno haya ya kwenye taarifa ya Tume ya Haki Jinai na haya ya juzi ya Tume ya Matukio ya Oktoba 2025, unapata siyo mfanano tu, bali unapata picha ile ile, copy and paste ya tabia, mwenendo na hulka ya Jeshi la Polisi. Ukitafakari sana kwa kina unashindwa kujua ni kweli Tume haikuwa na neno la kusema juu ya uwajibikaji wa sasa hivi kuhusu Jeshi la Polisi? Nimesikia mahali ubishi wa kisheria kwamba Tume ya Jaji Chande ya safari hii, ilikuwa na uwezo au mamlaka kutaja majina ya wahusika wa vurugu za Oktoba 2025. Kwamba ingeliweza kabisa kutaja majina na kutaka uwajibikaji wa moja kwa moja, badala yake imetumia njia ndefu ya kutaka ngazi za kimamlaka kuanzisha uchunguzi wa kijinai kwa kuwa haikuwa sehemu ya hadidu za rejea kufanya uchunguzi wa kijinai.

Nimetanguliza hadhari hapo juu, kwamba ningali ninaitafakari taarifa ya Tume ya Matukio ya Oktoba 2025, kwa leo itoshe kusema tu kwamba Tume inafahamu kwamba anayekutwa na ngozi ya ngo’mbe ndiye mwizi wa ng’ombe. Tume imekwepa kutaja kwa uwazi ni nani kakutwa na ngozi ya ng’ombe, lakini dunia inajua ng’ozi I mikononi mwa nani. Tusubiri hatua za kijinai zifuatazo. Ila bado tupo nyuma sana kutibu ugonjwa wetu.

spot_img

Latest articles

Adaiwa kumuua mtalaka wake kwa panga kisa nguvu za kiume

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi mkoani Lindi linamshikilia Hassan Athuman Mpogo (46), mvuvi na...

Rais Ruto kuhutubia Bunge Tanzania

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Kenya, William Ruto, anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania Mei 5,...

Mwigizaji, msanii wa Bongo Flava wafariki dunia

Na Mwandishi Wetu MSANII wa filamu nchini, Hashim Kambi, amefariki dunia leo alasiri akiwa anapatiwa...

Watu 37 washikiliwa kwa makosa ya mtandao

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewakamata watu 37 kwa...

More like this

Adaiwa kumuua mtalaka wake kwa panga kisa nguvu za kiume

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi mkoani Lindi linamshikilia Hassan Athuman Mpogo (46), mvuvi na...

Rais Ruto kuhutubia Bunge Tanzania

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Kenya, William Ruto, anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania Mei 5,...

Mwigizaji, msanii wa Bongo Flava wafariki dunia

Na Mwandishi Wetu MSANII wa filamu nchini, Hashim Kambi, amefariki dunia leo alasiri akiwa anapatiwa...