Taifa lina umri mkubwa, mifumo yetu iakisi ukubwa huo

Ukitafakari vema safari ya umri wa taifa letu, yapo mambo kadhaa yanayojitokeza yakiashiria kwamba huenda kuna mahali tuliruka hatua, au tulikwepa kujenga wajibu wetu wa kitaifa. Ni kama vile kwa kitambo sasa kumekuwa na mkakati wa makusudi wa ama kupuuza kupitia hatua husika kwa ukamilifu wake, au kukwepa kwa visingizio mahususi vya kutopitia hatua hizo.

Nitazungumzia mambo machache. Ni kwa nini mwaka jana, 2025, tulikuwa na aina ya uchaguzi wa aina ile tulioshuhudia ambayo hata marafiki damudamu wa taifa letu, walijitenga nasi?

Tulifikia hatua hiyo kwa sababu moja kubwa. Kwamba tumekubali kuingia katika mfumo wa siasa za ushindani za vyama vingi, lakini ndani ya nafsi zetu tumekataa katakata kukubali kuundwa na kufuatwa kwa mfumo unaohakikisha ushindani wa kisiasa unakuwapo. Ndiyo maana tunaunda taasisi za kusimamia uchaguzi kama kiini macho. Kwamba tunaona fahari kuwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo kimsingi imejithibitisha kuwa ni ‘kituko’ kwa jinsi ilivyoendesha uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kukataa au kukwepa kujenga mfumo na taasisi thabiti za kuratibu na kusimamia uchaguzi, ni moja ya kielelezo cha kukataa kukua na kukomaa kama taifa. Matokeo yake, mwaka jana tumejikuta katika hali inayofanana na taifa lililotoka vitani.  Ambalo makundi mbalimbali ya kijamii yanagombea madaraka. Ingelikuwa tumejiruhusu kukua kwa wakati, leo tusingejiruhusu kuwa na INEC inayofanana na hii iliyoko. Na ni hakika matukio ya Oktoba 29 mpaka Novemba 2, 2025 ya mauaji, umwagaji mkubwa wa damu na aibu ya taifa yasingetufika.

Hali hii ya kukataa kukua na kukubali wajibu kama taifa huru, linalojitegemea, linaloheshimu haki za raia wake, na kusimamia pasi na shaka mfumo wa utawala bora na utawala wa sheria, ndiyo mpaka leo inaleta mashaka ya kukubali kuwa na katiba mpya inayoakisi hali halisi ya matarajio ya watu wa taifa letu kwa sasa.

Kukwama kwa katiba mpya mwaka 2014, haikuwa bahati mbaya, ni mwendelezo wa kukataa kukua.

Bunge mojawapo wa mihimili mitatu ya madaraka ya dola, linatoa sura ya kuhuzunisha kama taifa kweli hili linasonga mbele katika utawala wa sheria, demokrasia na haki za raia wake.

Mijadala na uhuru wa Bunge, unaacha maswali mengi. Majadiliano ya sheria yanaendelea kuzunguka masuala ya utawala bora, mageuzi ya kiuchumi, na umoja wa kitaifa, lakini wakosoaji wanasema taasisi hiyo inazidi kuwa si jukwaa la mijadala huru bali nyongeza ya mamlaka ya serikali kuu.

Umiliki wa chama tawala bungeni, ni matokeo ya hali iliyotokana na mwenendo wa INEC katika kusimamia uchaguzi kwa sura ya ‘kimakengeza’, ambayo imezaa Bunge ambalo kwa sura ya uwakilishi wake, imeturejeshea Bunge la kabla ya mageuzi ya vyama vingi mwaka 1992.

Umiliki mkubwa wa CCM bungeni umebana nafasi ya sauti pinzani, jambo linaloimarisha wasiwasi kwamba usimamizi wa Bunge kwa serikali unadhoofika. Hili limekuwa suala kuu katika mijadala ya kiraia: kwamba Bunge haliwezi kuikosoa serikali kwa nguvu, hivyo swali kuu linakuwa uwajibikaji utapatikana wapi?

Katika sura kama hii, nani anaweza kusema kwa ujasiri kabisa kwamba taifa linakua, linakomaa na kufanana na umri wake wa uhai wa miaka 65 sasa? Kwamba kama taifa hatujawahi kuonja utamu wa Bunge la vyama vingi, lililokuwa na meno na liking’ata kwelikweli? Walau, mara baada ya uhuru hasa kabla ya kuharamishwa kwa vyama vingi, na baadaye baada ya uchaguzi mkuu wa 1995 hadi mwaka 2015 tuliporejea tena kwenye ngome ya ‘kulindana’, tulikuwa na Bunge lenye makali ya kuweza kuiwajibisha serikali.

Mabunge yote ya utawala wa awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa na utawala wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete, hayakuwa mabunge ya mzaha.

Kwa nini kumekuwa na juhudi zote hizi za kuua sauti mbadala katika taifa, kuua uwajibikaji, kujenga ‘kulindana’? Ni kielelezo cha kukataa kukua, kuamini kwamba kwa kuahirisha matatizo yetu leo, kwa kukataa kukubali kubadilika na kwenda na wakati, eti hali hiyo itapotea tu kama umande. Tunakataa kukua.

Pamoja na ukweli kwamba Tume ya Jaji Mohammed Chande ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 imekabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Aprili 23, 2026, tafakari ya kina ya kauli za viongozi wakuu nchini hapa, kabla ya ripoti hiyo iliwasilisha simulizi (narrative) moja muhimu, kwamba yaliyotokea tumesababishiwa, na wala hatujasababisha wenyewe kwa kukataa kukua, ama kukataa kupiga hatua ili kubaki salama kama taifa komavu.

Kwa hiyo, tunaposhuhudia kurejea nyuma kwa demokrasia au kukomaa kwa utawala wa kiimla, ni sura nyingine ya kutamani ‘utoto’ wetu. Kutamani tulivyokuwa miaka ya 60, 70, 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90, hata kama uhalisia haukubali kuendesha hali hii kwa sasa.

Kielelezo ni matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo siyo tu yalishangaza wengi, bali yanaweza kuendelea kushangaza kama tutatamani kuendelea na umri wetu wa utotoni. Umri wa utawala wa kuamrisha, utawala wa kukataa mawazo mbadala, utawala wa kuamini katika chama kimoja, utawala wa chama kushika hatamu. Dunia ya sasa inakataa kabisa kukubaliana na mizania ya namna hiyo. Hii ni dunia ya kipekee sana. Inataka uwazi, uwajibikaji, ujumuishi, na zaidi ya yote haki sawa kwa wote.

Mizania ya gia ya serikali kwamba inatafuta utulivu, ukuaji wa uchumi, na mageuzi yanayodhibitiwa kama mfumo halali na unaosukumwa kwa nguvu kubwa kwa upande mmoja, bila kutambua kuwa kuna upande mwingine wa jamii inayozidi kuwa na ufahamu wa haki zake za kidemokrasia na isiyokubali tena uwakilishi wa ishara bila ushindani wa kweli, ni mambo ambayo yanafaa kutafakariwa kwa kina sana. Ustawi hautakuwapo katika mizani isiyotambua ukweli huu. Kutambua hayo, ndiko kukua kwenyewe.

Hatari kubwa iko katika pengo linalozidi kupanuka kati ya mielekeo hii miwili. Kama mageuzi yatakuwa ya polepole au ya juujuu, imani ya wananchi inaweza kupungua zaidi. Lakini kama serikali itafungua mfumo kwa haraka bila kusimamia mvutano wa kisiasa, inaweza kusababisha misukosuko. Hii ndiyo ile hatari ya kuruka hatua katika ukuaji, unaweza kujikuta katika mtanziko mkubwa uzeeni.

Wakati huu masikio na macho ya Watanzania yakiwa yanataka kuitafakari ripoti ya Tume ya Jaji Chande, taifa ni lazima liamke na kuishi kadri ya umri wake.

Yafaa kutafakari, juu ya njia sahihi ya kutekeleza mageuzi ya katiba na uchaguzi kwa uaminifu na ushirikishwaji; kulegeza kabali isiyo dhidi ya vyama vya upinzani ili kuachia uwanja wa ushindani wa kisiasa na kutoa fursa ya chaguo kwa umma juu vyama hivyo; na mwisho, dola itambue na kuruhusu nafasi ya vyama vya kiraia kutekeleza wajibu wake badala ya kuendelea kuvikaba koo.

Fursa hii ni pamoja na kuachia uhuru wa habari utamalaki katika nchi. Haya yakiachiwa yanaweza kutufanya kama taifa tulandane na ukubwa wa umri wetu.

spot_img

Latest articles

Waziri Ndejembi awasilisha bajeti ya 2026/26, kipaumbele umeme wa uhakika nchini

Na Mwandishi Wetu Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya...

Rais Samia akabidhi 94.1 bilioni mikopo ya wanawake, vijana

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imekabidhi hundi ya shilingi 94.1 bilioni kwa ajili ya mikopo ya...

Mganga tiba za asili jela miaka 30 kwa kubaka

Na Mwandishi Wetu Mahakama ya Wilaya ya Kasulu imemhukumu mshitakiwa Nuru Hamimu Omary (48), mkulima...

DAWASA yawaunganishiwa maji kwa mkopo wakazi wa Kibosha

Na Mwandishi Wetu Wakazi zaidi ya 100 wa Kitongoji cha Kibosha Mji Mpya wamejitokeza kuomba...

More like this

Waziri Ndejembi awasilisha bajeti ya 2026/26, kipaumbele umeme wa uhakika nchini

Na Mwandishi Wetu Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya...

Rais Samia akabidhi 94.1 bilioni mikopo ya wanawake, vijana

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imekabidhi hundi ya shilingi 94.1 bilioni kwa ajili ya mikopo ya...

Mganga tiba za asili jela miaka 30 kwa kubaka

Na Mwandishi Wetu Mahakama ya Wilaya ya Kasulu imemhukumu mshitakiwa Nuru Hamimu Omary (48), mkulima...