Nani amwambie Rais Samia: ‘Name and Shame’ bila vyombo vya habari imara haifui dafu

SUALA la utawala bora halijawahi kuwa eneo rahisi katika uendeshaji na usimamizi wa ofisi za umma. Hii ni changamoto ya kidunia. Hata mataifa yaliyopiga hatua, nayo yanasumbuliwa na maadili ya uadilifu (noble principles) katika kusimamia ofisi za umma.

Kwa bahati njema kwa mataifa yaliyopiga hatua, taasisi za kusimamia uadilifu na uwajibikaji zina nguvu. Ndiyo maana unaweza kusikia mihimili ya madaraka ya dola, kwa maana ya mahakama, bunge na serikali (utawala) kila moja kwa nafasi yake na kwa madaraka yaliyoainishwa kikatiba, yakisaidia uwajibikaji kutokea katika mataifa yao.

Tanzania katika eneo la utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka ya dola na kuwapo kwa vyombo vya kusimamia ‘kanuni za maadili ya uadilifu katika ofisi za umma, imesimika vyombo mahususi vya kutekeleza wajibu huo.

Miongoni mwa vyombo hivyo, ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo huongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Ofisi hii imeanzishwa kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 143 ndiyo inaunda ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hiki ni chombo cha kikatiba cha kusukuma uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma – fedha za umma.

Hii ndiyo mamlaka mwaka baada ya mwaka hukagua jinsi fedha za umma zilivyotumika. Katika ukaguzi huo, hutoa hati za aina mbalimbali. Zipo hati safi, zipo hati za kuridhisha na zipo hati chafu. Mwaka baada ya mwaka ofisi hii hufanya kazi hiyo na ripoti yake hukabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye naye ana wajibu wa kuhakikisha inafikishwa bungeni ili wabunge waijadili. Bunge ndiyo chombo cha kimamlaka kikatiba kinachoruhusu matumizi ya fedha za umma kulingana na bajeti ya serikali inayowasilishwa kwenye Bunge kila mwaka.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere alikabidhi ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2024/25 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 30, 2026. Pamoja na mambo mengi ambayo ripoti ya CAG kwa mwaka 2024/25 iliibua ni mwendelezo wa matumizi mabaya ya fedha za umma. Ukiukaji mkubwa wa taratibu za zabuni na manunuzi, uzembe wa kutokutekeleza mapendekezo mbalimbali yanayotolewa na CAG mwaka baada ya mwaka. Kukataa au kupuuza kutekeleza maelekezo hayo, ndiko mwaka baada ya mwaka udhaifu ule ule wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma unajirudia tena na tena.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Samia kwa kutaka kusaidia kujengwa kwa tabia ya uadilifu katika usimamizi na uendeshaji wa ofisi za umma, alishauri Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ianze kutaja kwa majina taasisi zinazokiuka taratibu za manunuzi ya umma. Hali hiyo itasaidia kile alichotaja kwa kimombo ‘name and shame’ (kutaja na kuabisha).  Siku hiyo Rais alipokea ripoti tatu, ikiwa ni ya CAG, ya PPRA na ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB).

Kwa nini Rais alipendekeza ‘name and shame’? Duniani kote inajulikana kwamba kutaja na kuaibisha ni mkakati uliokubalika kitaifa na kimataifa katika kuhamasisha uwajibikaji.

Mkakati wa ‘Kutaja na Kuaibisha’ kwa kawaida hufanya kazi kwa kuweka mambo hadharani. Kwa maana hiyo matumizi ya vyombo vya habari kwa njia ya kuchapisha majina ya watu wanaohusishwa na makosa (kama vile ufisadi au udanganyifu) inakuwa ni nyenzo ya lazima ambayo haiepukiki. Katika zama za sasa, mitandao ya kijamii nayo ni nyenzo ya lazima kupitia majukwaa hayo watu husambaza machapisho wakikosoa au kufichua tabia fulani isiyofaa.

Hapa ndipo orodha za taasisi za umma ambazo zimetopea katika ukiukaji wa maadili – ufisadi, rushwa, uzembe, upendeleo na kila aina ya tabia ambazo zinakinzana na utaratibu wa kisheria na utawala bora, huwekwa hadharani ili kuibua uwajibikaji na maadili mema ya kitaasisi.

 ‘Kutaja na Kuabisha’ ni mkakati unaotumika kuwasilisha shinikizo la uwajibikaji. Kwa kutaja, zile mamlaka zenye wajibu wa kuadhibu na kuwajibisha wahusika hutarajiwa watekeleze wajibu wake wa usimamizi. Kwa Tanzania, ‘Kutaja na Kuaibisha’ ni ujumbe unaostahili kusukumwa serikalini, kwa taasisi kama TAKUKURU, PPRA yenyewe, Bunge, na vyombo vingine vya kimamlaka.

Nikijaribu kumsoma Rais juu ya ‘Name and Shame’, nia yake ilikuwa ni kupeleka ujumbe kwa taasisi na watendaji wa umma ambao wamekuwa sugu kiasi cha kutopea katika ukiukaji wa wajibu wao, hasa katika eneo la usimamizi wa rasilimali za umma. Ili wabadilike, ili waondoke katika tabia hiyo ambayo kimsingi imekuwa chanzo kikubwa cha kupotea kwa fedha za umma; kuibuka kwa hasira ya wananchi dhidi ya serikali yao, lakini pia kuliweka Bunge katika mtego mbaya wa kuonekana kuwa limeshindwa katika wajibu wake wa kuisimamia serikali hasa katika eneo la matumizi ya fedha za umma.

Hata hivyo, nia njema ya Rais inaweza kujikuta ikizingwa katika mazingira hasi yaliyoshamiri nchini ambayo hayalandani na mkakati mzima wa ‘name and shame’. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ufanisi wa mkakati wa ‘name and shame huwa na athari kubwa zaidi katika jamii yenye utamaduni unaothamini sifa na heshima. Kwa maana hiyo, katika jamii ambayo hadhi na heshima ni muhimu, kufichuliwa hadharani huwa na nguvu kubwa ya watu kujirudi. Lakini, katika jamii ambayo mtu anayetumia ofisi ya umma kujinufaisha binafsi anaonekana shujaa, suala la ‘name and shame’ haliwezi kuzaa matunda yoyote.

Ni ukweli usiopingika, ndani ya taifa letu, tumefika hatua ya kuwatukuza na kuwaheshimu wezi wa mali ya umma, wapiga dili, na kila aina ya tabia ya kukwepa mifumo halali ya kisheria iliyowekwa ili kusimamia na kuendesha ofisi za umma. Yetu ni jamii siyojali aibu ya kutajwa hadharani kwa wizi na ubadhirifu, yetu ni jamii inayoshangilia na kukuza wizi na uporaji wa mali ya umma.

Hadhi ya vyombo vya habari kwa sasa nayo ni mojawapo ya vikwazo vya kufanikisha mkakati wa ‘name and shame’. Mahali penye vyombo huru vya habari na uwazi wa taarifa, ni uwanja mzuri wenye rutuba ya kustawisha mkakati wa ‘name and shame’. Nachelea kusema kuwa kwa sasa Tanzania tunaweza kutajwa kama taifa lenye vyombo huru vya habari. Kwamba kwa nyakati za sasa uthubutu wa vyombo vya habari umekwenda chini sana, uhuru wa uhariri umeshuka sana, ujasiri wa waandishi wa habari nao umeporomoka sana; katika mazingira ya namna hiyo, kufanikisha mkakati wa ‘name and shame’ inakuwa ni kazi ngumu sana.

Ni katika hali hii, watawala wetu wanapaswa kujua kwamba taifa linalokuza uhuru wa vyombo vya habari linajitengenezea lenyewe mfumo bora zaidi wa uwajibikaji.

spot_img

Latest articles

Tume Jaji Chande imekwepa kututajia aliyekutwa na ngozi ya ng’ombe

NINGALI ninaitafakari ripoti ya Jaji Mohammed Chande ya matukio ya Oktoba 2025 wakati na...

Adaiwa kumuua mtalaka wake kwa panga kisa nguvu za kiume

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi mkoani Lindi linamshikilia Hassan Athuman Mpogo (46), mvuvi na...

Rais Ruto kuhutubia Bunge Tanzania

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Kenya, William Ruto, anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania Mei 5,...

Mwigizaji, msanii wa Bongo Flava wafariki dunia

Na Mwandishi Wetu MSANII wa filamu nchini, Hashim Kambi, amefariki dunia leo alasiri akiwa anapatiwa...

More like this

Tume Jaji Chande imekwepa kututajia aliyekutwa na ngozi ya ng’ombe

NINGALI ninaitafakari ripoti ya Jaji Mohammed Chande ya matukio ya Oktoba 2025 wakati na...

Adaiwa kumuua mtalaka wake kwa panga kisa nguvu za kiume

Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi mkoani Lindi linamshikilia Hassan Athuman Mpogo (46), mvuvi na...

Rais Ruto kuhutubia Bunge Tanzania

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Kenya, William Ruto, anatarajiwa kuhutubia Bunge la Tanzania Mei 5,...