Na Mwandishi Mbeya
TANZANIA imepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Marekani baada ya Serikali na Panda Hill Tanzania Limited kusaini makubaliano ya kuendeleza Mradi wa Niobium wa Panda Hill—hatua inayolenga kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa madini mkakati.
Kupitia mradi huo, Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, itamiliki asilimia 16 ya hisa chini ya mfumo wa ‘free carried interest’, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa Taifa katika maamuzi ya kimkakati na manufaa ya mradi.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, iliyohudhuriwa pia na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema mradi huo unahusisha uzalishaji wa madini adimu yasiyopatikana kwa wingi duniani, na kwamba Tanzania inalenga kujipatia nafasi ya kipekee katika soko la kimataifa la niobium.

Alibainisha kuwa soko la dunia kwa sasa linatawaliwa na wazalishaji wachache wakubwa, hivyo utekelezaji wa mradi wa Panda Hill utaiweka Tanzania kwenye ramani ya wazalishaji wakuu wa madini hayo duniani.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, uzalishaji wa niobium duniani kwa sasa unatawaliwa na wazalishaji wachache, akibainisha kuwa mzalishaji mkubwa zaidi kutoka Brazil huchangia takriban asilimia 80 ya mahitaji ya dunia, huku mzalishaji mwingine kutoka nchi hiyo hiyo akichangia takriban asilimia 11, na Canada ikichangia takriban asilimia 6.
Aliongeza kuwa kupitia mradi wa Panda Hill, Tanzania inalenga kuwa mzalishaji wa nne duniani kwa kuchangia takriban asilimia 4 ya mahitaji ya dunia, huku uzalishaji ukitarajiwa kufikia takriban tani 100,000 kwa mwaka.

Akisisitiza dira ya Serikali, Mavunde alisema mwelekeo wa Dira 2025–2050 pamoja na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unalenga kuhakikisha madini yanaongezewa thamani ndani ya nchi ili kuongeza manufaa kwa wananchi.
Alieleza kuwa Tanzania sasa inapanua wigo zaidi ya uchimbaji wa kawaida kwa kuwekeza katika uchakataji na uzalishaji wa bidhaa za viwandani zenye thamani ya juu.
Niobium, madini yanayotarajiwa kuzalishwa katika mradi huo, hutumika kuongeza uimara wa chuma na kutengeneza aloi za kiwango cha juu zinazotumika katika miundombinu mikubwa na teknolojia za kisasa, ikiwemo magari ya umeme na injini za ndege.
Kwa upande wa mwekezaji, Meneja Mkuu wa Panda Hill Tanzania Limited, Dennis Cook, alisema kampuni imeingia katika hatua mpya ya utekelezaji wa mradi kwa kushirikiana rasmi na Serikali, baada ya kipindi kirefu cha majadiliano.
Alisema mradi ulikuwa karibu kuanza mwaka 2017 kabla ya mabadiliko ya kisheria, na tangu wakati huo kampuni imekuwa ikishirikiana na Serikali kukamilisha makubaliano muhimu ya kuusukuma mbele.

Cook alitaja hatua zinazofuata kuwa ni pamoja na kupata Leseni Maalum ya Uchimbaji Madini, kusasisha taarifa za upembuzi yakinifu ili kuendana na gharama za sasa, kuingiza matumizi ya umeme wa gridi, pamoja na kufanya tathmini ya soko la ferroniobium ili kuhakikisha ushindani kimataifa, ikiwemo soko la Marekani.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina alisema mradi huo unatarajiwa kuleta faida kubwa kiuchumi, ukiwa na uwekezaji wa awali wa $442 milioni. Bw. Mchechu alieleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka 5 hadi 8, gharama za uwekezaji zinatarajiwa kurejeshwa.
Aliongeza kuwa katika uhai wa mradi, Serikali inatarajiwa kupata mapato ya $686 milioni (takribani Sh2 trilioni), yatokanayo na mrabaha, kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya mapato ya asilimia 30, kodi ya gawio, pamoja na gawio la hisa za Serikali.
Alisema kupitia hisa zake pekee, Serikali inatarajiwa kupata $134 milioni (takribani Sh300 bilioni), fedha ambazo zitachangia maendeleo ya miundombinu na huduma muhimu za kijamii kama barabara, shule na hospitali.
Kwa mujibu wa kampuni, mradi unahusisha ujenzi wa mgodi wa niobium, kituo cha uchenjuaji na kiwanda cha kuzalisha ferroniobium—bidhaa yenye thamani kubwa inayohitajika katika viwanda vya chuma.
Bidhaa hiyo inalengwa kuuzwa katika masoko ya Afrika, Asia, Ulaya na Marekani, hatua itakayoiwezesha Tanzania kushiriki moja kwa moja katika minyororo ya thamani ya viwanda vya kimataifa.
Kipekee zaidi, mradi huo utajumuisha ujenzi wa kiwanda cha ferroniobium kitakachokuwa cha kwanza barani Afrika na cha nne duniani kujengwa ndani ya kipindi cha miaka 40 iliyopita.
Kwa biashara za ndani, mradi unatoa fursa kubwa ambapo thamani ya manunuzi ya ndani inatarajiwa kufikia $1.77 bilioni, huku asilimia 70 ya bidhaa na huduma zikitarajiwa kununuliwa ndani ya nchi wakati wa uzalishaji.
Hii inafungua milango kwa kampuni za Kitanzania kunufaika kupitia mikataba ya muda mrefu katika sekta mbalimbali kama ujenzi, usafirishaji, matengenezo, huduma za kiufundi na nyinginezo.
Kuhusu ajira, zaidi ya watu 1,600 wanatarajiwa kuajiriwa wakati wa ujenzi, na ajira za kudumu zipatazo 600 kuundwa, huku wanufaika wa moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja wakifikia takriban 7,000.
Mradi huo unatekelezwa katika eneo la Gereza la Kilimo la Songwe, ambapo takriban ekari 5,434 zitatumika kwa shughuli za mradi.
Katika hafla ya utiaji saini, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, alisaini Framework Agreement kwa niaba ya Serikali, huku yeye pamoja na Msajili wa Hazina wakisaini pia Shareholders Agreement, kukamilisha muundo wa ushiriki wa Serikali na usimamizi wa mradi.


