DCEA yakamata Tani 9.93 za Dawa za Kulevya, Watuhumiwa 151 Watiwa Mbaroni

Na Tatu Mohamed 

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 9.93 za dawa za kulevya za aina mbalimbali na chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya katika kipindi cha Januari hadi Februari 2026.

Mbali na ukamataji huo, Mamlaka imeteketeza ekari 87.5 za mashamba ya bangi, kukamata magari sita na pikipiki 29 zilizokuwa zikitumika katika usafirishaji wa dawa hizo, huku jumla ya watuhumiwa 151 wakitiwa mbaroni katika operesheni zilizofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 4, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni maalum zilizotekelezwa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine za Serikali.

Ameeleza kuwa katika tukio la Mutukula, kwa kushirikiana na maafisa wa forodha, Mamlaka ilikamata boksi 105 za dawa aina ya Pethidine zenye chupa 1,045, boksi 31 za Morphine Sulphate zenye chupa 310 na boksi 44 za Fentanyl zenye chupa 440. 

“Dawa hizo zilikutwa ndani ya basi la abiria la kampuni ya SR Classic lenye usajili namba 5673AB04 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lililokuwa likifanya safari zake kati ya Uganda, Tanzania na Congo.

“Watuhumiwa saba walikamatwa kuhusika na tukio hilo, akiwemo Hassan Omary Mwambashi maarufu Macheni (50) mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam; Ibrahim Saidi Malindi (36) anayeishi Kampala, Uganda,Yassa Said Hamood (38) mkazi wa Magomeni, Hamad Said Hamad (46) mkazi wa Mombo, Tanga; Abdul Athuman Khamis (31) mkazi wa Amana, Mohamed Abdallah Sako (34) mkazi wa Ilala, na Mwinshaa Mohamed Abdalla (47) mkazi wa Magomeni,” amesema.

Amefafanua kuwa dawa aina ya Pethidine, Morphine na Fentanyl ni dawa tiba zenye asili ya kulevya katika kundi la afyuni (opioids) zinazotumika hospitalini kwa ajili ya kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, wagonjwa wa saratani, ajali na wenye selimundu. 

Hata hivyo, ameonya kuwa dawa hizo zikichepushwa hutumika kama dawa za kulevya na zinaweza kusababisha uraibu wa haraka na hata vifo kutokana na kuathiri mfumo wa fahamu, mapigo ya moyo na upumuaji.

“Dawa zilizokamatwa zinadhibitiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura ya 219, dawa hizo zimedhibitiwa kisheria na huingizwa na kusambazwa na Bohari ya Dawa (MSD) pekee,” amesema.

Kuhusu bangi aina ya skanka, Kamishina Lyimo amesema imeendelea kukamatwa kwa wingi katika operesheni mbalimbali ambapo jijini Dar es Salaam, Jontwa Samwel Mwaikonyole (43) mkazi wa Gogoni Kibamba alikamatwa akiwa na kilogramu 81.883 za skanka ndani ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili CAA 129054 na tela CAA 22911 kutoka Afrika Kusini lililokuwa limebeba matunda aina ya apples.

Ameongeza kuwa, katika eneo la Chanika Buyuni, Masudi Rajabu (38) na Shafii Mohamed (30) walikamatwa wakiwa na kilogramu 488.64 za skanka. 

“Jijini Mbeya, watuhumiwa sita walikamatwa kwa nyakati tofauti wakisafirisha skanka kupitia mabasi ya abiria, akiwemo Lenard Paulo (21) aliyekutwa na kilogramu 46.46; Maria Kandonga (18), Monica Kandonga (41) na Ibrahim Mwakibete (26) waliokamatwa na kilogramu 9.68; Joseph Mkwala (30) raia wa Malawi aliyekamatwa na kilogramu 4.62; pamoja na Esther Mbise (22) aliyekamatwa na kilogramu 16.1.

“Mkoani Arusha, Fatuma Mussa Mohamed (45) maarufu Mama Arapha na Elibaraka Martin Kingu (29) maarufu Baraka walikamatwa wakiwa na bunda 937 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 363.45, huku Mama Arapha akitajwa kuwa mhalifu wa muda mrefu aliyekuwa akiendesha mtandao wa usafirishaji wa mirungi,” amesema.

Aidha, amebainisha kuwa katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Tabora, Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Katavi, Mtwara, Mara, Morogoro, Kigoma, Ruvuma na Kilimanjaro, jumla ya tani 5.24 za bangi, tani 4.04 za mirungi na gramu 72 za heroin zilikamatwa.

Amesisitiza kuwa DCEA itaendelea kuimarisha operesheni dhidi ya wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya na kuhakikisha dawa tiba zenye asili ya kulevya hazichepushwi kutoka katika matumizi halali ya hospitalini.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha biashara hiyo, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja.

spot_img

Latest articles

Media Brains yaendesha mafunzo kwa wanahabari kutumia dijitali

Kampuni ya Media Brains ikishirikiana na Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) wanaendesha mafunzo...

Msajili wa Hazina afanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Lifezone Metal

Na Mwandishi wa OMH Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amefanya mazungumzo na Bw. Keith Liddell,...

RC Chalamila akemea wimbi la utapeli na uporaji wa ardhi

Na Tatu Mohamed MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa muda wa...

Rais Samia kuzindua ujenzi wa matanki 15 ya mafuta Bandari ya Dar es Salaam

Na Tatu Mohamed RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa...

More like this

Media Brains yaendesha mafunzo kwa wanahabari kutumia dijitali

Kampuni ya Media Brains ikishirikiana na Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) wanaendesha mafunzo...

Msajili wa Hazina afanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Lifezone Metal

Na Mwandishi wa OMH Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amefanya mazungumzo na Bw. Keith Liddell,...

RC Chalamila akemea wimbi la utapeli na uporaji wa ardhi

Na Tatu Mohamed MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa muda wa...