Lissu aibwaga Jamhuri, kesi yahamia Mahakama ya Rufani

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imekubali mapingamizi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, dhidi ya notisi ya ushahidi wa ziada iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri kupitia shahidi ACP Amini Mahamba katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Katika uamuzi mdogo uliotolewa leo, Mahakama imeeleza kuwa notisi hiyo haikukidhi matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo haiwezi kupokelewa kama sehemu ya ushahidi katika hatua ya sasa ya kesi.

Awali, Februari  23, 2026, Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, aliieleza Mahakama kuwa upande wa Jamhuri uliwasilisha notisi hiyo ukiambatanisha ushahidi wa ziada wa ACP Mahamba, aliyekuwa kiongozi wa upelelezi wa matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Upande wa mashtaka ulidai kuwa waliutambua ushahidi huo wakati wa maandalizi ya shahidi huyo aliyepaswa kuanza kutoa ushahidi Februari 16, 2026.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Dunstan Ndunguru alisema Mahakama ilichambua hoja za pande zote mbili Jamhuri na utetezi ambazo zote zilijengwa kwa kutegemea kifungu cha 308 (1), (2), (3) na (4) cha sheria hiyo, kabla ya kufikia hitimisho kuwa notisi iliyowasilishwa haikukidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria.

Jaji Ndunguru alifafanua kuwa kifungu hicho kinaruhusu kuwasilishwa kwa ushahidi wa shahidi ambaye maelezo yake yalikuwepo lakini hayakusomwa wakati wa mwenendo wa ukabidhi (committal proceedings), lakini hakitoi nafasi ya kuingiza ushahidi mpya ambao haukuwahi kuwepo au uliopatikana baada ya hatua hiyo kukamilika.

Mahakama pia ilibainisha kuwa kwa mujibu wa rekodi za kesi na maelezo ya upande wa Jamhuri, ACP Mahamba tayari alikuwa ametoa maelezo yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wa hatua ya ukabidhi. Hata hivyo, ushahidi wa ziada uliokusudiwa kuwasilishwa ulihusu matukio yaliyopatikana wakati na baada ya uchaguzi mkuu, jambo lililoifanya Mahakama kuhitimisha kuwa hauingii ndani ya wigo wa kifungu cha 308 cha CPA.

Katika hatua nyingine Jamhuri imefungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kutupilia mbali notisi yake ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo. 

Kutokana na hatua hiyo Mahakama Kuu kupitia kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Dunstani Ndunguru, kama ilivyo utaratibu wa kisheria imetangaza kusimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo mpaka Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wa shauri hilo.

spot_img

Latest articles

MIF 2026 kujadili mikakati ya kufikia uchumi wa kati wa juu 2050

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imesema Mkutano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji...

Kombe la Shirikisho hatua 32 Yanga yaangukia Polisi, Simba B19

Na Winfrida Mtoi DROO ya hatua ya 32 wa Kombe la Shirikisho  msimu wa 2025/26,...

Rais Samia azindua jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa

Na Mwandishi Wetu Rais Samia Suluhu Hassan, leo Februari 24, 2026, amezindua jengo la Makao...

Wizara ya Madini na CRDB wasaini makubaliano kurahisisha mikopo kwa wachimbaji wadogo

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Madini kupitia Tume ya Madini leo Februari 23, 2026...

More like this

MIF 2026 kujadili mikakati ya kufikia uchumi wa kati wa juu 2050

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imesema Mkutano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji...

Kombe la Shirikisho hatua 32 Yanga yaangukia Polisi, Simba B19

Na Winfrida Mtoi DROO ya hatua ya 32 wa Kombe la Shirikisho  msimu wa 2025/26,...

Rais Samia azindua jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa

Na Mwandishi Wetu Rais Samia Suluhu Hassan, leo Februari 24, 2026, amezindua jengo la Makao...