Rais Samia hawezi kujivua uanadiplomasia akiwa ikulu

Dunia tunayoishi sasa mataifa hutegemeana. Huheshimiana na kuhitajiana. Ndiyo maana hata nchi za ulimwengu wa tatu japo zinajulikana kuwa ni masikini – kwa maana kuwa hazijapiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi, kisayansi na nyinginezo, bado mataifa tajiri yanazihitaji.

Yanazihitaji kwa sababu nyingi. Moja kutafuta washirika wa kuwaunga mkono katika mambo mbalimbali yanayohitaji ushawishi, hasa kwenye kuwasilisha hoja kama kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa au kuanzisha ajenda ya kidunia na mambo kama hayo. Pia kutafuta fursa za kiuchumi. Hii inawezakana kwa kutafuta maelewano ya kufikia rasilimali ambazo ni muhimu kwa maendeleo, lakini ni adimu. Mahusiano haya husaidia kufungua milango ya kiuchumi- ndiyo maana siku hizi kauli iliyoshika kasi ni ‘diplomasia ya uchumi.’

Ni katika mantiki hiyo, kwa mfano, nchi hufungua ofisi za kibalozi katika nchi mbalimbali kusaka fursa. Hizi ni fursa za ushawishi au hata kupata rasilimali za moja kwa moja – madini adimu, maji, njia za mawasiliano na uchukuzi, rasilimali za misitu, bahari na hata masoko ya bidhaa mbalimbali.

Katika muktadha kama huu, mawanda ya diplomasia ni makubwa sana. Kikubwa ni kujua kwamba diplomasia inagusa kiini cha jinsi mataifa yanavyofanya kazi katika uhalisia wa dunia ya leo.

Katika uelewa huo, mataifa hutumia nguvu kubwa ya kufungua balozi zake katika nchi mbalimbali, huteua wawakilishi wa kuiwakilisha nchi huko. Gharama hizi ni za lazima ili taifa liwe taifa, kwanza linalochangamana na mataifa mengine; pili, liwe na uwezo wa kusukuma ajenda zake katika mahusiano ya kimataifa na kubwa zaidi, kuwa na uwezo wa kushawishi upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa ustawi wa nchi zao. Hili ni jambo muhimu.

Ni kwa msingi huo, dunia ya diplomasia inakubaliana kwamba wakuu wa nchi kama marais au mfalme au waziri mkuu, kulingana na mfumo wa nchi, ndiye mwanadiplomasia mkuu wa taifa husika, hata kama si mwanadiplomasia wa taaluma.

Sifa kuu za kidiplomasia zinazotarajiwa kwa kiongozi mkuu wa nchi kwa uchache ni kuliwakilisha taifa lake wakati wote. Mkuu wa nchi huliwakilisha taifa lake kimataifa. Ndiyo maana anapozungumza mkuu wa nchi, kauli yake ni ya taifa. Yaani huchukuliwa na kutambuliwa kwamba ni taifa husika ndilo limezungumza. Hapa ni muhimu kuweka angalizo, akizungumza mkuu wa nchi siyo chama chake cha siasa kimezungumza, wala siyo mtu binafsi amezungumza. Ni taifa limezungumza.

Hadhi na nafasi hii ya mkuu wa nchi katika ulimwengu wa diplomasia inamlazimisha wakati wote, kujitafakari juu ya anachotaka kuzungumza. Ni wajibu wake kujua ni lini azungumze au ni lini ajizuie kuzungumza, ili asiongeze ama mvutano, au migogoro baina ya mataifa.

Kwa ujumla wake, wakuu wa nchi ndiyo waidhinishaji wa majadiliano ya kimataifa na ushawishi wake. Wakuu wa nchi hujadili mikataba, husimamia ushirikiano wa kimataifa na kutatua migogoro, mara nyingi kwa njia zisizo za moja kwa moja. Kwa maana hii, kuelewa, kutambua na kuzingatia jinsi maneno, ishara na mtindo wa kauli zinavyotafsiriwa katika mazingira ya kimataifa, ni jambo la umuhimu wa kipekee kwa mkuu wa nchi.

Wiki hii Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa kauli ya kushtua kidogo katika uga wa diplomasia. Akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Rais alisema kuwa katika mawanda ya kidiplomasia (ubalozi) watu wanafundishwa kuwa  wapole kuwajibu waliowakera, jambo ambalo yeye hawezi na ndiyo maana alisema yeye: “wakinikera mimi nabwatuka tu.”

Ujumbe wa rais hapa unaweza kuwa na maana nyingi, kubwa ni kwamba hawezi kuwa mwanadiplomasia, na ndiyo maana akishabwatuka washauri wake huonyesha kama alikwenda mrama, naye huwaeleza kuwa ni kazi yao. Bila shaka kuwaachia kazi ya kufanya katika diplomasia ya kunyoosha mambo ambayo huenda yameharibiwa kwa ‘kubwatuka.’

Kwanza ni vema ikaeleweka kwamba diplomasia hujenga uthabiti na kuaminiana. Kama hakuna kuaminiana baina ya mataifa, hali hiyo huzaa kutokutabirika ambayo inaweza kudhoofisha hadhi na ustawi wa taifa.

Ni kweli duniani humu kuna viongozi wenye mtindo wa kutoa kauli tata, za kukera wengine au za kuonyesha msimamo mkali katika kusimamia kile wanachokiamini, hata hivyo, katika hali hiyo mkuu wa nchi anatarajiwa kuheshimu misingi ya kidiplomasia wakati wote.

Ingawa nchi nyingi, hasa za ulimwengu wa tatu ambazo zina katiba dhaifu kabisa wakuu wa nchi aghalabu huwa kama wao ndiyo katiba, kuna madhara makubwa taifa linaweza kupata, kama mkuu wa nchi akipuuza diplomasia. Mojawapo ni kutengwa, kupoteza washirika, kupoteza fursa za kiuchumi na mambo mengine ambayo hupatikana katika ushirikiano chanya unaoheshimu dhana ya kidiplomasia.

Diplomasia si suala la mtindo tu, bali ni njia mahususi ya kulinda maslahi ya taifa bila migogoro isiyo ya lazima. Mkuu wa nchi anapopuuza diplomasia, hufungua mlango mbaya utakaoingiza madhara mabaya yasiyotarajiwa kwa taifa lake. Miongoni mwake ni kama kupotea kwa uaminifu wa kimataifa; kupungua kwa ushawishi katika majukwaa ya kimataifa; kuzorota kwa ushirikiano wa kimataifa, kutengwa na hata kuporomoka kwa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.

Kupuuza diplomasia kwa kawaida kunaweza kumfanya mkuu wa nchi aonekane shujaa, hivyo kushangiliwa na wananchi wake. Hupata pongezi za makofi ya mashangilio kwa kitambo kidogo tu, lakini hupoteza ushawishi, uaminifu na utulivu kimataifa. Mara nyingi matokeo yake ya muda mrefu ni kuleta uharibifu unaohitaji gharama kubwa kurekebishwa ama na warithi wake au hata yeye mwenyewe kugeuka mambo yanapokuwa magumu.

Ni kwa kuzingatia ukweli huu, Rais Samia anapaswa wakati wote kutambua kwamba yeye ni mwanadiplomasia namba moja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hana namna ya kukwepa wajibu huo, iwe ni kwa kukerwa au vinginevyo.

spot_img

Latest articles

Msimu wa pili mbio za Pande Marathon kuzinduliwa Feb 14 Siku ya Wapendanao

Na Mwandishi Wetu UZINDUZI wa mbio za Msakuzi Pande Game Reserve Marathon awamu ya...

Dk. Mwigulu ajadiliana na Kamati ya Maandalizi AFCON 2027

Na Mwandishi Wetu WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amekutana na  Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi...

Coastal Union yawatembezea kichapo maafande wa Magereza

Na Mwandishi Wetu TIMU ya Coastal Union imetembeza kichapo cha mabao 4-1 kwa maafande wa...

Simba yazitaka pointi tatu kwa KMC kesho

Na Winfrida Mtoi KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Steve Barker ameweka wazi kuwa hakuna...

More like this

Msimu wa pili mbio za Pande Marathon kuzinduliwa Feb 14 Siku ya Wapendanao

Na Mwandishi Wetu UZINDUZI wa mbio za Msakuzi Pande Game Reserve Marathon awamu ya...

Dk. Mwigulu ajadiliana na Kamati ya Maandalizi AFCON 2027

Na Mwandishi Wetu WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amekutana na  Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi...

Coastal Union yawatembezea kichapo maafande wa Magereza

Na Mwandishi Wetu TIMU ya Coastal Union imetembeza kichapo cha mabao 4-1 kwa maafande wa...