Na Esther Mnyika
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), limefuta matokeo ya watahiniwa 102 wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2023 kutokana na udanganyifu na waliondika lugha ya matusi kwenye karatasi za majibu.
Matokeo ya ya kitado cha nne yametangazwa leo Januari 25, 2024 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk.Said Mohamed.
Amesema kati hao waliofutiwa matokeo, watano waliondika matusi, wakati matokeo ya wanafunzi 376 yakizuiwa kutokana na kupata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani.
Dk.Mohamed amesema watahiniwa walioshindwa kufanya mtihani huo mwaka jana wamepewa fursa ya kufanya masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa kwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.
Dk. Mohammed amesema jumla ya watahiniwa 572,359 walisajiliwa kufanya mtihani huo Novemba mwaka jana ambapo 484,823 sawa na asilimia 87.65wamefaulu.
Amesema wasichana waliofaulu ni 257,892, wavulana wakiwa 226,931, huku masomo ya lugha ikiwamo kichina yakifanya vizuri zaidi.
Amesema wanafunzi waliofaulu masomo ya kiswahili asilimia 96.80 na kichina ni 91.36
“Kati ya watahiniwa 471,427 waliofaulu, wasichana ni 250,147 sawa na asilimia 88.11 na wavulana ni 221,280 sawa na asilimia 90.81. Hivyo, wavulana wamefaulu vizuri zaidi kuliko wasichana,” amesema.
Hata hivyo NECTA imezipongeza Kamati za Uendeshaji Mitihani za Mikoa na Halmashauri, Manispaa na Jiji, wakuu wa shule, wasimamizi na wasahihishaji wa mtihani huo kwa kazi nzuri ya kutekeleza jukumu la uendeshaji mtihani huo.