Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa rai kwa Majaji na Mahakimu nchini kuwa uhuru wa Mahakama usitumike kama sehemu ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki na kuwataka kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba pamoja na sheria za nchi
Amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa, imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo, wakati alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama, na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwa Kata zote nchini zisizo na Mahakama za Mwanzo.
Makamu wa Rais amesema Mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi mbalimbali kuheshimu tume iliyoundwa na Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuacha kuongelea masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, amesema mahakama itachukua hatua stahiki kuhakikisha inakuwa sehemu ya kupata haki mapema bila ucheleweshwaji, badala ya kuwa mahali pa kuegesha mashauri ya migogoro.
Amesema baadhi ya wadau si waaminifu, kwani wanashindwa kuwajibika kimikataba na kisheria katika mashauri ya madai, na kwamba mahakama itachukua hatua dhidi yao ili kuimarisha nidhamu na uwajibikaji wa mawakili na watendaji wa mahakama.
Aidha, Jaji Mkuu ameeleza kuwa Mahakama inaendelea na hatua ya kuiboresha Sheria ya Mawakili ili kulinda mamlaka na uhuru wake.


