Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini leo Februari 2, 2026 kwenda Dubai, Falme za Kiarabu, ambapo anatarajiwa kushiriki katika uzinduzi wa mpango wa Global Africa Investment Summit (GAIS) utakaofanyika kwa pamoja na mkutano wa Dunia wa Serikali (WGS 2026).
Mkutano wa WGS 2026, unaobeba kaulimbiu “kutengeneza serikali zijazo (Shaping Future Governments)”, ni jukwaa la kimataifa linalowakutanisha wakuu wa nchi na serikali, watunga sera, viongozi wa taasisi za kimataifa, sekta binafsi na wawekezaji wakubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ushiriki wa Rais Samia katika mkutano huo unaweka mkazo katika diplomasia ya uchumi, huku lengo kuu likiwa ni kuoanisha sera za maendeleo ya Tanzania na mwelekeo wa mitaji ya kimataifa na kuharakisha uwekezaji unaochochea ajira na ukuaji wa uchumi.
Sambamba na WGS, Rais Samia atashiriki uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa la kimkakati la uwekezaji lililoanzishwa na Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa.
Mpango wa GAIS ulianzishwa na Dk. Akinwumi Adesina, Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa, lengo kuu likiwa ni kuunganisha miradi yenye tija barani Afrika na wawekezaji wa kimataifa ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuongeza fursa za ajira.


