Jumatatu wiki hii Rais Samia Suluhu Hassan alifungua mkutano wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Tanzania, ambao ulikuwa mahususi kwa ajili ya watoaji wa haki hao kujijengea uwezo katika utendaji wao.
Katika mkutano huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji George Masaju, alitumia fursa ya kuwapo Rais katika mkutano huo, kueleza hali ilivyo katika muhimili wa mahakama katika kutekeleza wajibu wake. Kikubwa ambacho Jaji Masaju alisema ni kusukuma kutambua ukweli kwamba kazi ya mahakimu na majaji inapaswa kuwa ya uadilifu wa juu kabisa katika utumishi wa umma, kwa kuwa ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kikatiba ya kutoa haki kwa kila mmoja katika taifa.
Kabla ya kumkaribisha Rais Samia kufungua mkutano huo, Jaji Mkuu Masaju alisema kuwa kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘Jukumu la Mahakama Huru Katika Utoaji Haki’ akishikamanisha kauli hiyo na ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 107 A na 107 B. Ibara hizo zinaeleza kwa ujumla kwamba mamlaka na kauli ya mwisho ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama; aidha katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.
Katika hotuba yake, Jaji Mkuu alitaja vigezo kadhaa ambavyo kwa tathmini yake anaamini kuwa mahakama ya Tanzania imekuwa na hadhi ya kuaminika duniani. Alifanya rejea hiyo kwa kuwa Juni 2025 siku Rais Samia anamuapisha kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania alitamani mahakama ya Tanzania iwe na hadhi duniani; Jaji Masaju alianisha vigezo vinavyoipa mahakama hadhi ni pamoja na kuwa huru, kujiendesha bila woga, upendeleo wala kupokea shinikizo kutoka upande wowote; Usalama wa ajira wa mahakimu na majaji kama inavyoelezwa katika ibara ya 110 A (3) ambayo inaelekeza Rais kuunda Tume ya Majaji kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za mwenendo usiofaa wa jaji husika.
Aidha alisema kuwa hadhi ya mahakama inaaminika kama ni rahisi kufikika na wananchi katika kupata huduma za haki; ikijumuisha uwezo wa kukidhi gharama za kufungua mashauri, lugha inayotumika na upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi ambao uwezo wa kugharamia kesi haupo kama vile kulipa mawakili wa kuwawakilisha. Kadhalika alisema hadhi ya mahakama pia inapimwa kuangalia jinsi haki inavyopatikana kwa wakati bila kupoteza muda kwa kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa.
Mambo mengine ni uadilifu na uwazi wa mahakama, kutabirika na uthabiti wa maamuzi; maslahi stahiki ya kutosha za mahakimu na majaji ambazo zinalindwa kisheria; upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha na miundombinu ya kitekinolojia katika kufanikisha ufunguaji wa mashauri na uendeshaji wa mashauri, pamoja na mambo mengine. Kwa vigezo hivyo, Jaji Mkuu alisema kwamba mahakama ya Tanzania imepiga hatua na kufaulu vema katika vigezo hivyo. Hata hivyo, alisema bado zipo changamoto kadhaa, zikiwamo za rasilimali fedha, miundombinu ya makazi ya majaji, bima ya afya, vitendea kazi kama usafiri na maslahi na stahiki za mahakimu na majaji ambavyo aliomba virekebishwe ili kuongeza kasi na ufanisi wa mahakama nchini.
Ni dhahiri zipo hatua kadhaa zimepigwa katika kuboresha utendaji wa mahakama, hasa katika ujenzi wa miundombinu- majengo ya mahakama ya kisasa katika wilaya zote za Tanzania (kasoro tatu) na katika mikoa yote kuna majengo ya kisasa ya mahakama. Ni jambo la kheri na heshima kubwa kuona Taifa limepiga hatua katika upatikanaji wa miundombinu hii.
Hata hivyo, ni vema ikakumbukwa kwamba mkutano huu umefanyika katika kipindi ambacho taifa la Tanzania linapita katika kipindi chenye changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kisheria. Ni kipindi ambacho nchi yetu imeshuhudia wimbi kubwa la kufunguliwa kwa kesi nyingi zenye harufu ya kisiasa na kwa bahati mbaya, wapo majaji ambao ama kwa sababu ya woga, hofu au maslahi ya kufungamana na upande fulani katika kusikiliza mashauri wameshindwa kusimamia haki kupatikana mahakamani kwa wakati.
Inajulikana kwamba kazi ya mahakimu na majaji ni wajibu unaopaswa kufanywa na watu wenye uadilifu wa kiwango cha juu. Ni kazi ya ki-Mungu ya kutenda haki kwa wote bila upendeleo. Kama ambavyo nukuu mbalimbali kutoka kwa wanazuoni zinafundisha, kuwa na hakimu au jaji anayeegemea upande mmoja, ni vigumu haki kupatikana chini ya uangalizi wake, hali hii inadaiwa kuwa imeshamiri nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mfano, zipo kesi zinazofunguliwa na Jamhuri katika mahakama za Tanzania, sura, mwelekeo wake na hata msukumo wake ni kukanyaga haki za baadhi ya raia ambao wanaonekana kutokukubaliana na watawala. Kesi hizi, aghalabu hufunguliwa ili kuwazuia kupata haki zao, zinafunguliwa bila kuwa na ushahidi wowote wa maana, na kwa ujumla wake tathmini yoyote inaonyesha ni kesi za kimkakati za kudhibiti watu wa kundi au mwelekeo fulani katika jamii kupata haki zao.
Isivyo bahati, kesi hizi zinapofikishwa mahakamani, wapo baadhi ya majaji ama wanajifunga au kujikataza au kujiepusha na uamuzi ambao kwa tafsiri yao ni kupingana na wakuu walioko madarakani. Matokeo yake, wameacha kesi hizi kukaa mahakamani kwa muda mrefu kiasi cha kuangukia katika mtego wa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa (justice delayed is justice denied). Hizi zipo nyingi za kutoka katika zama hizi ambazo kumekuwa na madai kuwa kuna majaji wanajulikana wazi kwamba ni watetezi wa watawala na siyo wasimamizi wa haki katika mahakama za Tanzania kikatiba.
Katika mkutano huu ambao idadi ya mahakimu na majaji waliohudhuria ni 1,200 kati ya wanachama wake 1,700 wa Chama cha Mahahakimu na Majaji Tanzania, kuna kitu ninaona mahakama inakitafuta. Mahakama inatafuta uhuru wake. Mahakama inatafuta kuaminiwa kwake. Mahakama inatafuta kukubalika kwake ndani ya nchi na hata kimataifa. Na ndiyo maana katika mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kufanyika kwa marekebisho ya kuendesha sheria za ardhi kwa kuwandoa watendaji serikalini kama ilivyo kwa mabaraza ya ardhi na kuacha mashauri ya ardhi yasikilizwe na mahakama pekee. Aidha kuwaondoa watendaji wa serikali kuwa sehemu ya kusikiliza mashauri ya kinidhamu ya mahakimu na kuacha mfumo wa ndani ya mahakama kutenda kazi hiyo, hali ambayo itajenga uhuru wa mahakama.
Ukisikiliza kwa makini hotuba ya Jaji Mkuu Masaju, utaona kilio cha kutaka kuiweka mahakama mbali na kuingiliwa kiutendaji na mihimili mingine, iwe ni ya watawala (executive) au ya kisiasa. Utaona anavyosukuma mbele hoja ya uhuru wa mahakama kama ulivyofafanuliwa kikatiba. Pamoja na juhudi hizi, suala la kujiuliza anapatikanaje hakimu au jaji asiyejua kuwa kikatiba mahakama ni muhimili huru unaojitegemea katika kutenda kazi zake? Ni nini hasa kiini cha kuwapo kwa majaji wanaoshindwa kukalia viti vya kuhakikisha kuwa mahakama ni chombo huru kinachoendesha mambo yake kwa uhuru, bila woga wala shinikizo? Mkutano huu ukawaamshe mahakimu na majaji wote walioamua kufungamana na upande wowote katika kutenda kazi ili haki ikatamalaki nchini.


