Na Winfrida Mtoi
BONDIA wa kimataifa wa Tanzania, Hassan Mwakinyo, ameweka bayana kuwa pambano lake la kesho dhidi ya Mnaigeria, Stanley Eribo litakuwa la kisasi, huku Hamad Furahisha akitaka kuweka rekodi ya kumchapa Mmalawi Hanock Phiri.
Mabondia hao wanatarajia kupanda ulingoni kesho Desemba 26, kuzichapa katika pambano lililopewa jina la Boxing On Boxing Day kwenye Ukumbi wa Warehouse, jijjni Dar es Salaam.
Akizungumzia mchezo huo, Mwakinyo amesema kuwa hadi kufikia hatua ya kupima uzito na kila mtu afya yake ipo sawa, hakuna sababu ya kuzuia pambano hilo lisipigwe.

“Kutokana na afya za watu wote hapa ni nzuri, nafikiri hakuna sababu ya kufanya pambano lisipigwe. Mimi sina mengi ya kuongea kisasi kitafanywa,” ametamba Mwakinyo.
Naye Furahisha amesema mpinzani wake anatamba kwa kuwa amewapiga baadhi ya mabondia hapa nchini lakini ajue safari hii atakutana na kitu tofauti na kipigo kinamhusu.
Amesema amesindikizwa na watu wengi kwenda kupima uzito akiwamo diwani, wote wakiwa na imani naye, hivyo hatawaangusha watanzania.

Kwa upande wake Mratibu wa matukio wa Peak Time ambao ni waandaaji wa mapambano yako, Bakari Hatibu, amesema maandalizi yote yamekamilika na mabondia wote waliotakiwa wamefika.
Mapambano mengine Hassan Ndonga atazichapa na Ismail Boyka, Ally Ngwando vs Mussa Makuka
Issa Simba (Kahama) vs Wilson Phiri (Malawi), Debora Mwenda vs Mariam Dick (Malawi) na Leila Machi vs Hidaya Zahoro.


