Na Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA Mgombea wa Bavicha Taifa, Masoud Mambo amesema kuwa demokrasia ya kweli haijengwi kwa mashinikizo, vitisho au siasa za misimamo mikali, bali hujengwa kwa hoja, ushindani wa sera na heshima kwa katiba na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mambo amesema Tanzania ni nchi inayotawaliwa na sheria na kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria ni sawa mbele ya sheria bila ubaguzi wowote.
“Hivyo basi, jaribio lolote la kubeza, kudharau au kupuuza ushiriki wa vyama fulani vya siasa katika chaguzi, mijadala au majukwaa ya kitaifa kwa hoja kwamba chama au vyama vingine vimesusa, ni kinyume cha misingi ya demokrasia, haki na usawa.
“Kila chama cha siasa kina haki ya kushiriki au kutoshiriki katika mchakato wowote wa kisiasa, lakini haki hiyo haiwezi na haitakiwi kutumika kama chombo cha kulazimisha nchi kuyumba au kuvuruga utulivu wa Taifa,” amesema.

Amewataka Watanzania watambue kwamba lengo la vyama vya siasa si kusambaratisha nchi, bali ni kushika dola ili kutekeleza sera zao kwa maendeleo ya Nchi na wananchi wenyewe.
“Lengo hili haliwezi kufikiwa katika mazingira ya migawanyiko, machafuko, taharuki, chuki na uhasama wa kisiasa. Taifa lolote lisilo na amani, umoja na usalama, halina mustakabali wa maendeleo.
“Tunasisitiza kwa msisitizo mkubwa kwamba changamoto za kisiasa hazitatuliwi kwa maandamano na hamasa za uvunjifu wa amani, lugha za uchochezi, au kampeni za kuichafua nchi ndani na nje ya mipaka yake. Njia sahihi, ya kistaarabu na ya kizalendo ni kutumia meza ya mazungumzo na majadiliano ya wazi kwa hoja na ustahimilivu, mifumo ya kisheria iliyopo, na elimu ya uraia kwa wananchi kupitia kampeni zenye kujenga hoja ili wapime na kuamua kwa busara,” amesisitiza na kuongeza:

“Watanzania tukiruhusu siasa za kuvuruga amani zitawale, waathirika wa kwanza tutakuwa ni sisi wenyewe sio hao walio ughaibuni au wanasiasa wenye viza tayari kukimbilia ughaibuni. Maendeleo yatasimama, uchumi utadorora na ajira zitapotea hivyo gharama ya kuyajenga upya itabebwa na sisi wananchi wenyewe,”.
Amefafanua kuwa, kwa miongo mingi Tanzania imejenga heshima kubwa kimataifa kama nchi ya amani, umoja na utulivu wa kisiasa. Sifa hii haikuja kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya umadhubuti wa serikali zetu, busara za viongozi wetu na uzalendo wa sisi wananchi wake.
Amesema Tanzania imekuwa kimbilio la watu waliokimbia machafuko ya kisiasa katika mataifa yao. Tusikubali historia hii tukufu ibatilishwe kwa matakwa ya kisiasa ya muda mfupi.
“Tuwakatae wanaohamasisha au kuunga mkono mikakati inayolenga kuingiza nchi kwenye machafuko, vurugu au migawanyiko ya kisiasa kwani hao ni wanapinga maslahi ya Taifa na ustawi wa wananchi. Bila amani, hakuna haki; bila utulivu, hakuna maendeleo; bila umoja wa kitaifa, hakuna Tanzania imara,” amesema.
Aidha, amewakumbusha Watanzania wote waliopo nchini na diaspora kuwa mitandao ya kijamii si uwanja wa kuichafua nchi. Maneno, maandishi na kampeni za kuipaka nchi matope zina athari kubwa kiuchumi, kidiplomasia na kiusalama.
“Uzalendo wa kweli ni kukosoa kwa hoja, kutoa mapendekezo ya utatuzi kwa heshima na kwa nia ya kujenga si kubomoa,” ameeleza.


