Na Tatu Mohamed
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema serikali itaendelea kutekeleza kwa vitendo agenda ya maendeleo jumuishi kwa kuwawezesha makundi maalum yakiwemo wanawake, vijana, watoto, wazee na wafanyabiashara ndogondogo kwa mwaka wa fedha 2025/26 kupitia sera, programu na miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Gwajima, amesema hatua hizo zinafanyika chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na uchumi unaojitegemea.
Dkt. Gwajima amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta zinazotoa ajira kwa wananchi wengi zikiwemo kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, michezo, sanaa za ubunifu na madini, hatua inayolenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa makundi maalum na wananchi kwa ujumla.
“Katika kuhakikisha wananchi wanapata ujuzi wa kujiajiri na kuongeza kipato, Serikali imehamasisha matumizi ya vyuo vya maendeleo ya jamii vilivyopo nchini, sambamba na kuimarisha malezi na makuzi bora ya watoto kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali katika kutoa elimu ya malezi kwa wazazi na walezi,” amesema.

Akizungumzia masuala ya vijana balehe, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe nchini, inayohamasisha upatikanaji wa huduma bora za afya, ikiwemo upimaji wa Virusi vya UKIMWI na magonjwa ya zinaa, ili kujenga Taifa lenye nguvu kazi yenye afya na tija.
Katika eneo la uwezeshaji kiuchumi, Dkt. Gwajima amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya NMB imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo, ambapo jumla ya wafanyabiashara 4,870 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 9.9 yenye riba ya asilimia saba.
Amewahimiza wafanyabiashara hao kujisajili katika mfumo wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBN MIS) kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika halmashauri zao.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (Women Development Fund – WDF), ambapo katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2025 wanawake wajasiriamali 45 waliwezeshwa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 337.9.
Katika kulinda ustawi wa wazee, Dkt. Gwajima amesema zaidi ya wazee milioni 1.2 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu na bima ya afya bila malipo, huku makazi ya wazee yanayomilikiwa na Serikali na taasisi binafsi yakiendelea kutoa huduma muhimu kwa wazee nchini.
“Kupitia Sheria ya Manunuzi ya Umma, Serikali imeelekeza kila taasisi ya umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee,” amesema.
Vilevile Waziri Gwajima amesisitiza umuhimu wa amani kwa maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa kukosekana kwa amani huathiri zaidi makundi maalum.
Amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kutumia fursa za kiuchumi zilizopo na kuendelea kulinda amani, maadili na tunu za Taifa kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.


