Na Mwandishi Wetu
Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali shauri la maombi ya kuidharau Mahakama hiyo lililokuwa linawakabili viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, Katibu Mkuu John Mnyika na wenzao.
Shauri hilo lilikuwa la madai ya kukiuka amri yake ya kukizuia chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama hicho hadi hapo kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali baina ya Chadema Bara na Chadema Zanzibar itakapoamuliwa.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni walalamikaji katika kesi ya msingi namba 8323 ya mwaka 2025.
Akisoma uamuzi wa Mahakama hiyo leo Novemba 28,2025, Jaji Awamu Mbagwa aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa kwa hati ya dharura amesema, Mahakama imekubaliana na pingamizi lililokuwa limewekwa na Wakili wa utetezi Hekima Mwasipu kuwa maombi hayo yameletwa Mahakamani hapo nje ya muda
Jaji Mbagwa amesema kesi ya msingi namba 8960/2025 iliyoko chini ya Jaji Hamidu Mwanga ndio iliyokuwa msingi wa kesi iliyokuwa mbele yake na kwamba amri ya Mahakama kuzuia shughuli za kisiasa za CHADEMA ilitolewa na Mahakama Juni 10.2025
Ameeleza kuwa kesi ya kudharau amri ya Mahakama ililetwa Mahakamani hapo Oktoba 03 mwaka huu takribani siku 106 jambo ambalo halikubaliki kisheria, amesema Sheria inataka maombi ya aina hiyo yaletwe ndani ya siku 60.
Mbali na Heche na Mnyika, wengine katika shauri hilo la madai ya kudharau amri ya mahakama hiyo ni Rose Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya Gervas Bernard Lyenda, wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu Chadema.
Hivyo waombaji walikuwa wanaiomba mahakama hiyo iamuru wafungwe kama wafungwa wa madai kwa kuidharau mahakama kwa madai hayo ya kukiuka amri yake hiyo.


