Viongozi wa dini wahimiza Watanzania kupiga kura, amani

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

VIONGOZI wa dini mbalimbali mkoani Mwanza, wametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kupiga kura kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, uliopangwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Kadhalika katika kongamano la Amani la Viongozi wa Dini lililofanyika jijini Mwanza, viongozi hao wametoa wito kwa wananchi kudumisha amani hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu wakisema ni tunu ambayo Tanzania imekuwa nayo kwa zaidi ya miaka 60 ya Uhuru.

Akisoma Tamko la Kamati ya Amani ya Viongozi wa dini wa mkoa wa Mwanza, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Askofu Dkt. Charles Sekelwa, amesema viongozi wa dini wataendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwa wingi na kwa utulivu ifikapo Oktoba 29, 2025.

“Tunawahimiza wananchi kutumia haki yao ya kupiga kura kwa upendo, usawa na uwazi, kisha warejee majumbani kwao kwa amani. Tutaendelea kuiombea nchi yetu Mungu aibariki Tanzania kwa hekima na utulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema Askofu Sekelwa katika kongamano hilo lililokuwa na kaulimbiu isemayo ‘Uchaguzi ni Muda wa Maamuzi, Tushiriki Sote. Tudumishe Amani na Mshikamano kwa Maendeleo ya Taifa.’

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke, amesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa haki na maendeleo.

“Wapo wanaodhani tunahubiri amani kuliko haki, lakini haki haiwezi kusimama bila amani. Tusijidanganye amani kwanza. Tukajitokeze kupiga kura; kuacha kupiga kura ni kujinyima haki,” amesema.

Akichangia kwenye kongamano hilo, Sheikh Amani Mussa Maumba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Wilaya ya Nyamagana, amesema mahali popote hata kukiwa na riziki haiwezi kulika kama hakuna amani.

“Kwahiyo sisi kama viongozi wa dini jukumu letu tuhubiri amani kufa na kupona, lakini tuwaambie watu wetu wasiache kwenda kupiga kura na baada ya kupiga kura warudi majumbani wawe tayari kupokea matokeo,” amesema.

Mwenyekiti wa CCT Mkoa wa Mwanza na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, Zefania Ntuza ametoa wito kwa viongozi wa dini wenzake pamoja na familia zao kujitokeza kupiga kura.

“Lakini na waumini wetu tuwaeleze jambo hili kwamba wasiache kwenda kupiga kura, na watambue kuwa suala la amani ni jambo la muhimu sana, ndugu zangu Watanzania tuilinde amani, ni Mungu tu ameijalia nchi ya Tanzania,” amesema.

Naye Mchungaji Upendo Isaya amesema: “Ili tufanye maamuzi ya busara tunahitaji amani, na amani inaanzia moyoni. Kwahiyo tunapoenda kwenye Uchaguzi tumesikia mengi lakini kikubwa tutafute amani na kumbuka hii ni haki yetu ya Kikatiba kwa kuchague yule ambaye atakwenda kutufanyia yale yanafaa kwa manufaa ya nchi yetu”.

Mwenyekiti kamati ya kinamama wakiislam Mkoa wa Mwanza, Amina Masenza amewaomba Watanzania wafuate maamuzi ya Kikatiba kwa kwenda kushiriki katika Uchaguzi Mkuu, kwani watakuwa wameipata haki yao na kulinda amani ya nchi.

Akihutubia kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewahakikishia wananchi kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na usalama.

“Ninawahakikishia kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa kwamba tuko salama. Serikali ya Mkoa na vyombo vyote vya ulinzi na usalama tumejipanga kuhakikisha uchaguzi unamalizika kwa amani. Rai yangu ni wananchi wote kujitokeza kupiga kura bila hofu, wakiamini serikali ipo kazini kutimiza wajibu wake,” amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa Mwanza, ikiwa ni mkoa mkubwa na wa kimkakati wenye zaidi ya wakazi milioni 3.6, imeweka mikakati madhubuti ya kulinda usalama wa raia na mali zao katika kipindi chote cha uchaguzi. 

Aidha, amewapongeza viongozi wa dini kwa kuandaa kongamano hilo na kuendelea kuwa nguzo ya amani, haki, upendo na mshikamano, huku akitaka umma kutokubali kuchokozeka na watu wenye nia ya kuchochea vurugu.

“Serikali ipo tayari kukosolewa, lakini tukosoane kwa hekima na ustaarabu; si kwa chuki, dini au jinsia. Tukasikilize sauti za wananchi ili kudumisha misingi ya nchi,” amesisitiza.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema amani ni tunu ya kipekee ambayo kila Mtanzania anapaswa kuilinda, hususan wakati wa uchaguzi.

“Tuwakumbushe vijana wetu na waumini kuwa hakuna tunu muhimu zaidi ya amani, upendo na mshikamano. Tunapopiga kura, tufanye hivyo kwa upendo na kuilinda amani yetu. Tanzania imebarikiwa kuwa nchi isiyo na udini; tuilinde baraka hii,” amesema.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali, vijana na wadau wa amani, ambao kwa pamoja wametoa wito uchaguzi mkuu uwe wa amani, haki na mshikamano ili kuendelea kujenga taifa imara linaloongozwa na Watanzania wenyewe.

spot_img

Latest articles

Chalamila amkabidhi mjane Alice Haule Hati ya Nyumba

Na Tatu Mohamed MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemkabidhi hati ya...

Rasmi Kocha Yanga afungashiwa virago usiku

Na Mwandishi Wetu Uongozi wa Klabu ya Yanga umevunja mkataba na Kocha Mkuu, Romain Folz. ...

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...

More like this

Chalamila amkabidhi mjane Alice Haule Hati ya Nyumba

Na Tatu Mohamed MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemkabidhi hati ya...

Rasmi Kocha Yanga afungashiwa virago usiku

Na Mwandishi Wetu Uongozi wa Klabu ya Yanga umevunja mkataba na Kocha Mkuu, Romain Folz. ...