Na Tatu Mohamed
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amewataka wahandisi vijana nchini kutumia ubunifu na maarifa yao kutafuta suluhisho za changamoto zinazolikabili taifa badala ya kusubiri kupatiwa majibu kutoka nje.
Akizungumza leo Septemba 24, 2025 wakati akifunga Kongamano la Pili la Vijana Wahandisi (YEF) lililoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB), Dkt. Msonde amesema uhandisi wa Tanzania uko mikononi mwa vijana na si wageni kutoka mataifa mengine.

“Suluhisho la kiuhandisi sio kwa kuiga au kuleta kutoka mataifa mengine pekee. Hatutoweza kutatua matatizo yetu kwa kufikiria namna ile ile na utaratibu ule ule. Elimu yenu ya kiuhandisi mliyoipata ikusaidieni kuleta vitu vipya vya kutatua changamoto zetu za ndani,” amesema.
Ameongeza kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kuonesha ubunifu wa vijana, akiwapongeza washiriki kwa bunifu walizozionesha.
“Mafanikio yanahitaji ujasiri, nidhamu na ushirikiano wa kimkakati. Msikate tamaa mnaposhindwa, kwani kushindwa huko ndiko ishara ya kuelekea kwenye mafanikio zaidi. Mbegu ili iote lazima ioze,” amesema Dkt. Msonde.

Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa ERB, Wakili Mercy Jilala, amesema jumla ya wahandisi vijana 145 wameshiriki katika kongamano hilo huku 84 wakihudhuria kwa njia ya mtandao.
“Bodi iliamua kuanzisha mafunzo haya kwa sababu tuliona vijana wanapohitimu vyuoni wanakosa fursa ya kutoa mawazo mapya na kufundishwa namna ya kujiajiri. Tunawaandaa ili wasibaki kusubiri ajira pekee,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Menye Manga, amesema ERB itaendelea kutoa mafunzo na makongamano ya aina hiyo kwa kuwa idadi ya wahitimu wa uhandisi inaongezeka huku changamoto za ajira zikibaki kubwa.

Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu: “Mustakabali wa Uhandisi: Mageuzi ya Kitaifa Yanaongozwa na Suluhisho za Ubunifu za Vijana”, liliwakutanisha wahandisi vijana na watoa mada mbalimbali kwa lengo la kujenga uwezo wa kitaaluma na kuhimiza ubunifu katika sekta ya uhandisi.


