Na Winfrida Mtoi
BONDIA wa Kimataifa wa ngumi za kulipwa Tanzania, Hassan Mwakinyo anatarania kupanda ulingoni Desemba 26, 2025, jijini Mwanza, huku akitamani kupata vipaji vyenye ubora kama wake.
Akizungumza leo Agosti 15, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuelekea pambano hilo lililopewa jina la Boxing on Boxing Day, amesema anaamini kuna mabondia wenye uwezo wa kufanya vizuri kama yeye lakini wanahitaji kusaidiwa ili waonekane.
Mwakinyo amesema anatamani kuona mabondia bora wanatengenezwa nchini na kueleza kuwa hajaridhishwa na kile kinachoendelea katika mchezo huo kwani anafahamu kuna mabondia wanapewa ushindi usiostahili.

Amesema hakuna njia fupi ya kufikia malengo inabidi watu wapambane, wapigane kweli wakipata nafasi na si kusubiri kutengenezewa mazingira ya kushinda bila kutumia nguvu na kufanya maandalizi.
“Mimi ni mpiganaji na ninafuatilia wa ngumi, kwa hiyo naona vitu vingi ambayo vingine siwezi kuvisema hapa hadharani, ni kwamba tu tunahitaji kuapata mabondia wengi zaidi Tanzania na jitihada zilizopo ni ndogo sana. Hakuna bingwa wa kununua hata siku moja.
“Kuna wakati unapigana ulingoni, uwezo aliokufundisha mwalimu unaisha, nguvu uliyokuwa nayo inaisha, sapoti na kelele za za watu zilizokuwa nyuma huautazisikia tena lakini kitakachokufanya ushinde ni yale yaliyopo kwenye maisha yako na yanayopita katika moyo wako. Hivyo ukishakuwa na mabondia ambao lazima uwanunulie mechi ndiyo washinde unatangeneza watu ambao sio sahihi kuwepo walipo,” ameeleza Mwakinyo.

Ameeleza kufurahia kwake kwenda kicheza jijini Mwanza akiahidi kutoa burudani na ushirikiano na waandaji ambao ni Peaktime Promotion ili kuhakikisha wanaibua vipaji vya kulisaidia Taifa kufika mbali katika mchezo wa ngumi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kampuni ya PeakTime Promotion, Bakari Khatibu, amesema lengo ni kuinua vipaji vya mabondia wa Kanda ya Ziwa ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao wa kuendeleza vipaji vya mchezo wa ngumi nchini.
“Lengo la kufanya pambano hilo ni kuinua vipaji vya mabondia waliopo Kanda ya Ziwa pamoja na kuendelea kuutangaza mchezo wa ngumi katika mikoa mbalimbali nchini,” amesema Khatibu.
Aidha amesema mpinzani wa Mwakinyo atatangazwa hivi karibuni ili mashabiki na wadau wa ngumi waweze kumfahamu mapema.
Katika hatua nyingine amewakaribisha wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini pambano hilo, kwani litakuwa ni lenye mvuto wa aina yake kutokana na mabondia wanaopata ulingoni siku hiyo.