Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameizawadia Klabu ya Yanga Sh 100 milioni kwa kutambua ushindi na mafanikio makubwa waliopata katika msimu wa mwaka 2024/2025.
Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 30, 2025 alipokutana na viongozi pamoja na wachezaji wa Yanga waliofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kumkabidhi makombe matano ya michuano mbalimbali waliyoyatwaa msimu huu.
Amepongeza mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana na klabu hiyo kongwe, akieleza kuwa yanajenga heshima na historia muhimu katika tasnia ya michezo nchini.

Aidha, ameishukuru klabu hiyo kwa kuendelea kuitangaza Zanzibar ndani na nje ya nchi kupitia kampeni ya Visit Zanzibar, huku akieleza kuwa hatua ya klabu hiyo kucheza baadhi ya michezo yake Zanzibar kunachangia kukuza uchumi na sekta ya utalii kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wageni na wananchi kunufaika na fursa mbalimbali.
Halikadhalika, Rais Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha viwanja vya michezo ili kuwezesha michuano mingi zaidi kufanyika Zanzibar.

Naye Rais wa Yanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vilabu vya Soka Barani Afrika, Hersi Said, amemkabidhi Rais Mwinyi medali maalum ya michuano ya CRDB pamoja na jezi ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kutoa pongezi na shukrani kwa Rais kutokana na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya michezo nchini na kuahidi kuwa klabu hiyo itaendelea kucheza mechi zake visiwani humo.



Katika msimu wa 2024/2025 Yanga imefanikiwa kutwaa makombe matano ambayo ni Ngao ya Jamii, Kombe la Michuano ya Toyota, Kombe la Muungano, Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho.
Kikosi cha Yanga kimewasili jijini Dar es Salaam, huku kikipokewa na mamia ya mashabiki wa timu hiyo, wakishudia makombe yote matano yakiwa kwenye gari maalum.