LIPO tumaini. Ndivyo inavyoweza kuelezwa kwamba hata katika kiza cha usiku kuna tumaini la kutokea mwanga patakapopambazuka. Hali hii inaweza kueleza yale yaliyojiri katika nchi mbili za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya. Maofisa kadhaa wa vyombo vyenye dhamana na ulinzi wa raia na mali zao, Majeshi ya Polisi, wamejikuta katika uwajibikaji mkubwa kutokana na matendo yao maovu dhidi ya raia waliopaswa kuwalinda.
Nchini Tanzania Jumatatu wiki hii Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, imewahukumu kunyongwa maofisa wawili wa Jeshi la Polisi waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mfanyabiashara Mussa Hamisi (25), ambaye walimuua kwa kumchoma sindano ya sumu.
Mfanyabiashara huyo aliuawa Januari 5 mwaka 2022, mkoani Mtwara, baada ya kunyang’anywa fedha na mali na maofisa hao. Akisoma hukumu ya kesi hiyo namba 15/2023, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Hamidu Mwanga alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka (Jamhuri) umethibitisha kuwa watuhumiwa, aliyekuwa Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango walikiuka kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha makosa ya jinai, namba 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Hakimu alisema kuwa watuhumiwa hao ambao walikuwa na dhamana kubwa ndani ya Jeshi la Polisi, Kalanje akiwa ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara na Onyango aliyekuwa mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, baada ya kumuua mfanyabiashara huyo Mussa Hamisi kwa kumchoma sindano yenye sumu, walijaribu kuharibu ushahidi. Mwili wa mfanyabiashara huyo ulitupwa porini. Bila shaka wahusika wakiwa ni polisi wenyewe ili kufisha uovu wao dhidi ya raia.
Mfanyabiashara huyo aliingia katika mzozo na polisi alipokuwa anafuatilia fedha zake takribani Sh. milioni 31 walizokuwa wamempora. Bila shaka ili kuzima kabisa kelele zake, waliamua kumuua kwa sumu. Tukio hili halikuwa la kwanza kwa Polisi kuua raia baada ya kuwapora fedha zao. Mwaka 2006 polisi jijini Dar es Salaam waliwaua wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge baada ya kuwapora kiasi kikubwa cha fedha. Wafanyabiashara hao walikuwa ni Sabinus Chigumbi, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu aliyekuwa dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam. Waliuawa baada ya kuporwa fedha na polisi eneo la Sinza.
Matumaini haya si haba. Yametokea Tanzania na hivyo kuzidi kufunua uovu unaofanywa na baadhi ya askari polisi dhidi ya raia. Nchini Kenya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha mwanablogu na mwalimu Albert Omondi Ojwang.
Miongoni mwa walioshtakiwa nchini Kenya ni maofisa watatu wa polisi, Ofisa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi (OCS) aliyesimamishwa kazi, Samson Kiprotich Talaam na Konstebo James Mukhwana. Wengine waliotajwa katika kesi hiyo ni John Ngige Gitau, Gin Ammitoa Abwao na Brian Mwaniki Njue.
Taarifa kutoka ofisi ya DPP ya Kenya, inaeleza kuwa mauaji hayo yalitokea kati ya usiku wa Juni 7 na 8, 2025, ndani ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi, saa chache baada ya Ojwang kukamatwa nyumbani kwao Homa Bay na kuhamishiwa Nairobi. Ripoti ya upasuaji ilionyesha kuwa alifariki kutokana na majeraha ya kichwa, shingo na michubuko mingi mwilini, yakionyesha kuwa alishambuliwa kwa ukatili mkubwa.
Washukiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Kibera chini ya Kifungu cha 204 cha Kanuni ya Adhabu, kinachoshughulikia mashtaka ya mauaji nchini Kenya.
Nchini Kenya mashitaka haya yanafunguliwa dhidi ya askari polisi baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (Independent Policing Oversight Authority -IPOA), ambayo iliwasilisha matokeo yake kwa DPP siku moja tu kabla ya kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao.
Kifo cha Ojwang kilizua ghadhabu na maandamano ya umma nchini Kenya, hali iliyoibua mamlaka mbalimbali nchini humo, likiwamo Bunge la Seneti kutaka uwajibikaji wa wahusika wote wa uovu huo unaofanywa nyuma ya kuta za mahabusu za polisi.
Kama ilivyokuwa kwa Tanzania ambako Jeshi la Polisi lilitaka kujichunguza lenyewe baada ya kuwapo kwa taarifa za mauaji ya Mfanyabiashara Mussa aliyeuawa Januari 5, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan aliingilia kati akieleza kuwa polisi ni watuhumiwa katika suala hilo, hivyo isingeliwezekana wakajichunguza wenyewe. Alimtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, kuchukuwa jukumu hilo. Nchini Kenya nako awali polisi walitoa taarifa ya uongo kwamba Ojwang alikuwa amekufa baada ya kujipiga ukutani akiwa mahabusu ya polisi.
Mfanano huu wa Polisi wa Tanzania na Kenya, ndiyo hatimaye uliibua IPOA ya Kenya na Tanzania kamati ya Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alikabidhi ripoti kwa Rais Samia Februari 26, 2022. Ripoti hiyo haikuwekwa hadharani, lakini baadaye maofisa kadhaa wa polisi wakiwamo hawa waliotiwa hatiani walifikishwa mahakamani. Kenya ingali inasubiri kesi hiyo isikilizwe ili ukweli zaidi uwekwe wazi.
Rais Samia alisikia kilio cha Watanzania Januari 2022 juu ya mauaji ya Mfanyabiashara Mussa kama vile Rais Jakaya Kikwete alivyosikia kilio cha mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge na dereva teksi aliyekuwa anawaendesha. Rais alichukuwa hatua ambazo leo tunaona matokeo yake. Haki imetendeka. Hata kama uhai wa Mfanyabiashara Mussa hautarejea, walau ndugu zake na hata Watanzania wapenda haki, watahesabu kwamba kuna jambo kubwa limetendeka la kujenga uwajibikaji.
Kwa matukio ya kupotea, kutekwa na kuuawa kwa watu nchini kwa sasa, tukio la Mtwara na jinsi ambavyo limehitimishwa, hakika ni kengele imepigwa. Kwamba kunahitajika hatua nyingine nyingi na kubwa zaidi za kumaliza udhia huu. Kutuhumu, kulia na kupiga kelele peke yake hakuwezi kuleta uwajibikaji. Hakuwezi kukomesha uovu huu unaotokea nchini kwa sasa. Bila shaka zinahitajika hatua kama zilizochukuliwa Mtwara. Hatua hizi zitasaidia kujenga imani na tumaini jipya ndani ya jamii juu ya malalamiko yote ya vitendo vya kutekwa, kupotea na kuuawa kwa watu kwa kisingizio eti ni watu wasiojulikana wanatenda maovu haya.
Mara nyingi tumesikia watu wakisema kwamba eti wanaotenda haya hawajulikani. Kwa bahati mbaya sana ni kama kuna juhudi kubwa ya kutaka kuaminisha umma kwamba wanaotenda maovu haya hawajulikani. Ieleweke tu kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina vyombo vingi vya usalama. Kuna Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lipo Jeshi la Polisi, ipo Idara ya Usalama wa Taifa, lipo Jeshi la Magereza, ipo Idara ya Uhamiaji, kadhalika kuna Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Hivi ni vyombo vya usalama. Vimejaa uwezo, nyenzo na maarifa. Vina askari wenye weledi. Vina askari waliofunzwa na kufuzu vizuri sana. Hazina hii kubwa namna hii, hakika haiwezi kuzidiwa maarifa na watu wachache wanaojiita ‘wasiojulikana’.
Ni shauku ya kila mpenda amani katika nchi hii na katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki kuona kwamba haya ambayo yametokea Jumatatu nchini Tanzania na Kenya, yanakuwa ndiyo njia ya kuendea ili kujenga uwajibikaji katika mataifa yetu. Ni wakati wa kuvunja ukimya sasa, hakuna linaloshindikana kukomeshwa katika kadhia hii ndani ya nchi.