Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MWAKILISHI Mkazi wa shirika lisilo la kiserikali la Konrad Adenauer Stiftung nchini, Peter Koch, amewapongeza waandishi wa habari kwa kujitolea kwao katika kukuza masuala ya demokrasia na utawala bora na kusisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika mfumo wa utawala wa kidemokrasia.
Akifunga mafunzo ya siku moja jijini Mwanza ambayo ni mfululizo wa mafunzo yanayotolewa na kampuni ya Media Brains kwa ufadhili wa KAS kwa ajili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuzifahamu sheria zinazohusu uchaguzi, Koch alisema ushiriki wa wao katika mafunzo hayo ni wa msingi ili kusaidia uchaguzi kuwa huru.
“Uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika unategemea uwepo wa vyombo vya habari vyenye taarifa sahihi na vinavyowajibika,” Koch alisema na kuongeza: “Tunaamini kazi yenu itasaidia kulinda uhalali wa taasisi za kidemokrasia nchini Tanzania.”

Mafunzo hayo yalitolewa kwa waandishi wa habari 31 kutoka mkoa wa Mwanza yalijikita katika
masuala ya kisheria za uchaguzi, maadili ya taaluma, usalama wa waandishi wa habari na usawa wa kijinsia katika uchaguzi ili kuhakikisha kuna uandishi wa haki, sahihi na unaoelimisha jamii wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Absalom Kibanda ambaye ni Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains, alizungumzia historia ya sheria za uchaguzi nchini, huku akiweka wazi mabadiliko kadhaa yaliyofanyika kwa kutungwa sheria mpya ambazo ni Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kibanda alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuzisoma na kuzielewa kwa undani sheria hizo akizitaja kuwa nyenzo muhimu za kuwawezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao ipasavyo ya kuuelimisha umma wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu.
“Kama waandishi wa habari, uwezo wenu wa kuelewa mchakato wa uchaguzi na kuuliza maswali sahihi unategemea uelewa wenu wa sheria,” Kibanda alisisitiza. “Huwezi kuripoti kwa ufanisi kama huelewi sheria zinazotawala uchaguzi unaouandikia.”

Aidha, alitoa mtazamo wa kina kuhusu mageuzi ya hivi karibuni, kama vile kubadilishwa kwa jina la NEC kuwa INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi) pamoja na kuanzishwa kwa mchakato shindani wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo, licha ya mabadiliko hayo kuonekana kutokodhi kiu tarajiwa kwa wadau hasa vyama vya siasa vya upinzani.
Kadhalika baadhi washiriki wa mafunzo walionyesha wasiwasi kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana haukuonesha tofauti kubwa, kwani bado maafisa walioteuliwa kisiasa ndio waliendesha shughuli za uchaguzi.
Katika majadiliano ya pamoja, washiriki walibaini kuedelea kuwepo kwa upungufu katika mfumo wa uchaguzi wa Tanzania ukilinganishwa na majirani kama Kenya na nchi nyingine barani Afrika.

Upungufu huo ni pamoja, matokeo ya uchaguzi wa urais kutopingwa mahakamani hata kama kuna malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu, marufuku dhidi ya wagombea binafsi katika nafasi zote, mvutano na ukosefu wa uwazi katika mipaka ya majukumu kati ya Tume ya Huru y a Taifa ya Uchaguzi (INEC) na madaraka makubwa mno kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, na ukosefu wa usawa wa kijinsia hasa wanawake kutopewa nafasi stahiki katika mifumo ya uchaguzi.
Washiriki walibainisha kuwa ingawa marekebisho ya sheria na kutungwa kwa sheria hizo mpya ni hatua muhimu katika maboresho ya uchaguzi, bado unahitajikwa utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa sheria hizo.

Kwa upande wake Jesse Kwayu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Media Brains, aliwasilisha mada kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu, alisisitiza umuhimu wa kuzingatiwa kwa maadili ya uandishi wa habari na kuripoti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
“Hatuwezi kuzungumzia demokrasia na kuwaacha wanawake nyuma,” alisema Kwayu na kuongeza: “Waandishi wa habari hawapaswi kuripoti tu ukweli, bali kuhakikisha kwamba sauti za wanawake, vijana na makundi mengine yaliyotengwa zinasikika kwa haki na usawa.”
Washiriki walijadili masuala ya kijinsia katika kampeni, wakichambua jinsi vyombo vya habari vinavyopaswa kuwapa nafasi wagombea wanawake kuripoti masuala ya sera, sifa za uongozi na vikwazo vya kimfumo vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi.
Kahalika katika mjadala huo, washiriki walizungumzia changamoto wanazokutana nazo, zikiwemo hofu ya usalama wao wakati wa uchaguzi, uelewa wa sheria na mashinikizo ya kitaaluma.