KILA mwaka wa uchaguzi serikali ina kawaida ya kutoa bajeti inayogusa wananchi walio wengi, hasa wa kipato cha chini. Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, na ni kwa jinsi hiyo bajeti ya serikali ya mwaka 2025-2026 ina mwelekeo wa kugusa watu wa kipato cha chini zaidi.
Hatua hizi ni muhimu hasa zinapotazamwa kama mkakati halali wa serikali kusaidia wananchi kupunguza makali ya maisha. Ni halali pia kuunga mkono hatua hizi.
Kwa mfano miongoni mwa hatua ambazo serikali imetangaza katika bajeti inayokwenda kuanza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu ni marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147.
Akiwasilisha bajeti hiyo ya mwisho ya serikali iliyoingia madarakani mwaka 2020 na muda wake ukigota Oktoba mwaka huu, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchembe alitaja bidhaa zinazokwenda kunufaika na punguzo la ushuru ni pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks).
Mwigulu alisema kuwa serikali inakusudia kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) vinavyozalishwa ndani ya nchi kutoka Sh. 561 kwa kila lita hadi Sh. 134.2 kwa kila lita. Lengo la hatua hii ni kuweka unafuu kwa wazalishaji wa ndani, kuongeza ushindani na kuchochea uwekezaji.
Hapana shaka kwamba katika miaka ya hivi karibuni unywaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu umeongezeka sana nchini. Unywaji huu umeongezeka sana kwa kundi kubwa la vijana.
Duniani kote vinywaji vya kuongeza nguvu ni maarufu. Wanakunywa watu wa rika zote. Hata hivyo, hapa nchini vijana wenye afya njema, wanaotarajiwa wawe na nguvu za kawaida za mwili za kukabiliana na pilikapilika za maisha ndiyo wanywaji wakuu wa vinywaji hivi. Aghalab, unywaji wao umekuwa ni wa kupindukia.
Unywaji huu wa kupindukia umetajwa na wataalam wa afya kwamba ni wa hatari. Kwa mfano zipo tafiti nyingi zinazofungamanisha unywaji wa kupindukia wa energy drinks na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu ambayo ni kama mapigo ya moyo kwenda kasi; shinikizo la damu kuwa juu; mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida; uwezekano wa kupata mshituko wa moyo au moyo kusimama.
Madhara mengine yanayonasibishwa na unywaji wa energy drinks uliopitiliza ni pamoja na athari kwa mfumo wa mishipa ya fahamu kama vile wasiwasi, kutetemeka au mashambulizi ya hofu (panic attacks), kutopata usingizi au usingizi hafifu, kuumwa kichwa au kipandauso hata wakati mwingine kupata degedege (seizures).
Athari nyingine za kitafiti zinaonyesha kuwako kwa madhara ya kimetaboliki na viungo vya ndani. Hizi ni pamoja na kuongezeka kwa sukari kwenye damu (hatari ya kisukari aina ya pili), kuongeza uzito na unene kupita kiasi, madhara kwa figo, msongo kwa ini hasa kama inatumiwa pamoja na pombe au dawa.
Nimetafuta taarifa hizi kutoka vyanzo mbalimbali vya kitabibu kwa nia moja tu, kuweka wazi kwamba fasheni mpya hasa kwa kundi la vijana ambao kwa sasa ni kama damu yao imegeuka kuwa energy drinks, ni ya hatari sana. Wataalam wa moyo, kwa ujumla wao wanakubaliana kwamba matumizi yaliyopindukia ya energy drinks kama ambavyo yanashuhudiwa katika mitaa ya miji mingi ya nchini hapa ni wa hatari.
Nimeshuhudia kuwa kwa kiwango kikubwa sana nchini vijana wameingia katika uraibu wa energy drinks. Leo ukitembelea eneo lolote ambalo kuna kazi ya ujenzi ambayo inawakusanya vijana wengi kila uchao, utaokota makopo/chupa za energy drinks nyingi zilizotupwa baada ya vijana kujiburudisha na kinywaji hicho.
Kwa bahati mbaya sana, unywaji huu hauangalii muda. Kijana anafika kazini (site) asubuhi saa mbili, mkononi kashikilia chupa ya energy drink. Ikifika jioni anaweza kuwa amekunywa mpaka chupa kama tano hivi. Wapo wanaokunywa zaidi ya hapo. Ukiwauliza kwa nini wanakunywa vinywaji hivyo, jibu ni kwamba wanatafuta nguvu. Wanadai ‘kujiboost.’
Swali la kujiuliza, hivi kama asubuhi saa mbili mwili wa kijana hauna nguvu za kufanya kazi bila kusaidiwa na energy drink, ina maana uwezo wa mwili kujiendesha wenyewe bila msaada huo haupo. Huu ni ugonjwa, ni janga na ni hatari kwa kizazi hiki.
Wataalam wa afya wanasema kuwa kiasi cha mililita 400 cha energy drink ndicho kinaruhusiwa kutumika kwa siku kwa mtu mzima. Kwa bahati mbaya sana, vijana wengi, wakiwamo wabeba zege, waendesha bodaboda, wamachinga mitaani, vinyozi wa saluni, waendesha teksi, madereva wa daladala nk. wamegeuka kuwa mateja wa energy drinks. Hawawezi kufanya tena kazi bila msaada wa energy drinks.
Ni katika kutafakari ukweli huu mchungu, mtu anapaswa kujiuliza, hivi uamuzi huu wa kupunguza ushuru katika energy drinks, nia ni kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa hizi nchini ili kujenga taifa la namna gani? Hivi serikali haisikii kauli za ilani za mara kwa mara za wataalam wa afya juu ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza yakiwamo yanayochochewa na unywaji uliokubuhu wa energy drinks.
Kwa bahati mbaya sana, chupa moja ya energy drink yenye ujazo wa mililita kati ya 300 hadi 400 inauzwa kwa Sh. 500 tu. Jero! Hii ni pesa kidogo sana ambayo hata mtoto wa shule ya msingi anaweza kuipata akiamua kubana nauli yake ya kwenda shule. Urahisi wa vinywaji hivi na dhana potofu kwamba vinasaidia vijana kukabiliana na uchovu, kuongeza nguvu ya mwili kufanya kazi na pengine hata kwa dhana nyingine potofu za ‘kuwaboost’ kwenye mapenzi, zimechangia sana matumizi yake miongoni mwao.
Katika mazingira haya, uamuzi wa serikali wa kupunguza ushuru katika vinywaji hivi, kiuhalisia unakwenda kusaidia nini katika taifa letu. Inaweza kujengwa hoja kwamba vitajengwa viwanda vingi zaidi hivyo kukuza ajira; kuongeza mapato ya serikali na kila aina ya utetezi wa takwimu za kiuchumi. Utetezi wowote wa matumizi ya energy drinks wa kiwango kinachoshuhudiwa sasa nchini ni wa kuteketeza kizazi cha vijana. Ni janga linalokula taifa kidogokidogo, kama hatua muhimu hazitachukuliwa sasa ikiwa ni pamoja na kuongeza elimu juu ya madhara ya energy drinks, pamoja na kufanya upatikanaji wake uwe mgumu, tutakuja kukumbuka shuka alfajiri.