Na Tatu Mohamed, Mwanza
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Stanislaus Nyongo ametoa wito kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya nchi.
Ameyasema hayo leo Aprili 16, 2025 wakati akifungua Mdahalo wa Kitaifa ulioandaliwa na Media Brains kwa kushirikiana na PPPC wenye Mada Kuu ya Ubia wa Sekta ya umma na Sekta Binafsi katika Muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika maeneo mbalimbali kama vile sekta ya usafirishaji ikiwemo bandari, sekta ya Nishati na usafiri wa umma pamoja na huduma za kijamii.
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia, Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira bora, wezeshi na shindani kwa sekta binafsi ili kufanya kazi kwa ufanisi.

“Na ili tufanikiwe katika jambo hili, lazima tujipange na kuandaa midahalo kama hii ili kubadilisha fikra zetu na kujipanga vizuri. Kwahiyo nitoe wito kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mikakati ya nchi,” amesema.

Amefafanua kuwa, katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta binafsi imepewa kipaumbele katika kuchangia kwenye Dira hiyo.
“Mdahalo huu umekuja wakati ambapo Taifa letu limeingia katika hatua muhimu ya kupanga mustakabali wa Maendeleo yake kwa miongo ijayo kupitia maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

“Tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kutumia wananchi kukusanya maoni ya Dira hii. Tunatambua kuwa safari ya Maendeleo ni endelevu kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 iko katika hatua za utekelezaji na serikali imeanza katika maandalizi ya Dira mpya,” amesema.
Amefafanua kuwa, inapojadiliwa nafasi ya PPP katika Muktadha wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu kujiuliza maswali ya msingi yatakayosaidia kuweka mikakati thabiti ya ushirikiano kati ya Sekta ya umma na Sekta binafsi.

“Kwahiyo ni matarajio kuwa mdahalo huu utaongeza maarifa, kuibua hoja zenye tija na kuchochea ushirikiano wa kweli ambao utachangia kujenga Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Dira hiyo ina malengo sita ikiwemo kufanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi mseto, Stahimilivu, Jumuishi na imara ifikapo 2050,” amesisisitiza.