Watanzania wanazidi kunasa katika mzunguko wa umasikini unaosababishwa na kushamiri kwa bidhaa duni na bandia nchini, licha ya kuwapo kwa juhudi mbalimbali za vyombo vya usimamizi na udhibiti wake nchini.
Uwapo wa bidhaa duni au bandia mbali ya kuendelea kuzidisha mzunguko wa umasikini kwa wananchi, pia zinachangia matatizo mengine ya kiafya na hata vifo vya mapema kwa baadhi ya watumiaji wake.
Uchunguzi wa waandishi wa makala hii umebaini kuwa bidhaa hizo pia ni chanzo kikubwa cha ukosefu wa mapato kwa serikali kupitia kodi na ushuru.
Bidhaa hizo pia husababisha serikali kuingia gharama kubwa ili kuzibaini, kuzikusanya sokoni na kuziharibu.
Kwa upande wa afya, maisha ya watu wengi yameharibika na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na matumizi ya bidhaa dawa na vipodozi.
Kwenye kilimo wakulima nao wameripoti kupata hasara kubwa kutokana na kuuziwa pembejeo ambazo hazina ubora unaotakiwa.
Hasara kutokana na bidhaa bandia na zile zisizo na ubora haiendi kwa watu binafsi pekee, bali pia kampuni nyingi zinapata hasara na wakati mwingine kulazimika kufunga shughuli zake na kulazimika kutumia mabilioni ya fedha kukabiliana na madhara yanayotokana na bidhaa kuigwa na kutengenezwa chini ya ubora.
Ingawa hakuna takwimu za pamoja na za kina za siku za hivi karibuni kuhusiana na hasara ya kifedha inayotokana na kushamiri kwa bidhaa bandia na zile zisizo na ubora katika soko, lakini utafiti umebaini kuwa hasara inayosababishwa na bidhaa hizo ni kubwa.
Mathalani, katika eneo la dawa pekee, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa, Vipodozi na Vifaa Tiba (TMDA) inasema katika moja ya ripoti zake kuwa miaka miwili iliyopita, zaidi ya tani 435 za dawa za binadamu, dawa za mifugo na vifaa tiba visivyo na ubora na bandia vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30, zilikamatwa na kuteketezwa.
Aidha, utafiti uliofanywa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) miaka kadhaa iliyopita ulibaini kuwa wakati huo hasara inayotokana na bidhaa zisizo na ubora na bidhaa bandia inafikia asilimia 15 na 20 za pato la taifa kwa mwaka.
Nalo shirika la Viwango nchini (TBS) limesema kuwa Kwa mfano, mwaka wa fedha wa 2022/23 mpaka April 2024, Shirika lilifanikiwa kuondoa katika soko bidhaa mbalimbali ambazo zilibainika kuwa chini ya kiwango kiasi 10,139,189 Kg zenye thamani ya TZS 12,718,367,100.
Aidha, TBS wanasema kuwa wanakabiliwa na changamoto katika kudhibiti ubora wa bidhaa kutoka nje ya nchi kutokana na uwepo wa mipaka isiyo rasmi na uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaingiza bidhaa ambazo hazijakaguliwa na kupitisha katika mipaka isiyo rasmi au njia za panya na kuingiza katika soko.
Watu kadhaa waliozungumza na waandishi wa makala hii wamethibitisha kuwa tatizo la bidhaa bandia na zisizo na ubora ni kubwa nchini na linaathiri karibu kila aina ya bidhaa.
Awali, matatizo yalikuwa kwa bidhaa ambazo zinaagizwa kutoka nje, lakini katika miaka ya hivi karibuni tatizo hilo limekua baada ya wajanja wachache kuanza kuiga bidhaa halisi zilizopo sokoni na kuzalisha bidhaa bandia kwa jina lile lile la bidhaa halisi.
Kampuni moja ya utengenezaji wa mvinyo unaopendwa na watu wengi nchini hivi karibuni ililazimika kubadili vifungashio vya mvinyo wake (chupa) baada ya wajanja wachache kuanza kutengeneza mvinyo bandia kwa jina la mvinyo huo, wakiufungasha kwenye chupa zile zile za mvinyo halisi.
Bidhaa kutoka China

Sam Petro, mfanyabiashara wa vifaa vya kieletroniki anasema ubora wa bidhaa kutoka China unategemea uamuzi na uwezo wa mfuko wa mnunuzi.
Anasema mfanyabiashara anayekwenda kununua bidhaa China anaangalia kama ana uwezo wa kununua bidhaa za ubora gani, kama mtaji wake ni mkubwa anamudu bidhaa bora, ila kama ndiyo kwanza anajitafuta anaweza kununua chochote ilimradi anajua akishafikisha nchini atauza.
“Binafsi nilipata kukumbwa na balaa ya kuagiza TV. Zilipofika nchini hapa siyo kama nilivyotarajia. Ubora wake ulikuwa duni sana. Mteja niliyemwagizia mzigo alilalamika. Juhudi za kuibadilisha kwa kweli hazikuzaa matunda. Wauzaji kule China wanakuambia ubora wa bidhaa yako unategemea kiasi cha fedha ulizolipa,” anasema na kuongeza: “Kusema ukweli TV nyingi unazoziona madukani hapa Tanzania ni za ubora wa chini sana. Ukileta ile OG (original-halisi) sijui ni watu wangapi watanunua. Itakuwa ghali mno.”
Hata hivyo, anasema kwamba kuna wakati serikali ya China iliweka ukaguzi mkali sana kwenye simu za mkononi. Walifanya ukaguzi na kuzuia simu walizoona ni duni sana kutoka kwao kwenda nje.
Hata hivyo, haijulikani ukaguzi huo ulipunguza kwa kiasi gani bidhaa zenye ubora duni kutoka China kwa sababu chanzo kikuu cha kushamiri kwake nchini ni waagizaji wa Kitanzania wenyewe.
Sam anasema hajawahi kusumbuliwa na mamlaka za ukaguzi wa ubora wa bidhaa. Anaeleza kuwa hulipia mzigo wake kwa kampuni za kuchukua bidhaa bandarini pamoja na kodi ya serikali moja kwa moja, bila yeye kukutana na mamlaka hizo. “Mimi nikishalipa gharama zote (kwa wakala) ninasubiri tu kupewa taarifa ya kwenda kuchukuwa mzigo wangu,” anaeleza.
Kwa upande wake, mjasiriamali mwingine ambaye amejikita kuagiza bidhaa kutoka China, Elinaja Nko, amesema kuwa wazalishaji nchini China wanatengeneza ubora wa bidhaa kulingana na kiasi cha fedha mtu anacholipa.
“Uzuri ni kuwa wale Wachina hawakufichi kitu. Ukienda dukani kununua unaonyeshwa bidhaa tatu za aina hiyo hiyo, kila moja ikiwa na ubora wake. Ile yenye ubora mkubwa huuzwa kwa bei ya juu na yenye ubora wa chini huwa na bei ndogo.
“Tatizo letu sisi Watanzania ni kupenda vitu vya bei rahisi hivyo waagizaji wengi hununua zile za ubora wa chini. Lakini kwa sababu mwonekano wake ni ule ule wanunuzi hapa nchini wanakuwa hawana wasiwasi kwani wengi huangalia tu picha kwenye maboksi ya bidhaa bila kusoma kwa undani maelezo kuhusu ubora wa bidhaa husika,” anasema Nko.
Kuhusu ukaguzi wa bidhaa zinapoingizwa nchini Nko anasema hafahamu vizuri kwa sababu wafanyabiashara wengi hutumia kampuni za usafirishaji kuleta bidhaa zao.
“Mimi nikifunga mzigo wangu China nakwenda kwenye kampuni ya usafirishaji na nikishalipia nakutana na mzigo wangu godown (ghalani) umeshatolewa bandarini. Kwa hiyo hayo masuala ya ukaguzi wafanyabiashara wengi huwa hatukutani nayo, labda wale wanaoleta bidhaa wao wenyewe moja kwa moja,” anafafanua.
Kwa upande wake, mjasiriamali mwingine, Peter Keegan, hakutaka sana kuzilaumu mamlaka bali alishusha lawama kwa waagizaji wa bidhaa wenyewe kwani wao ndio wanachagua bidhaa hizo.
Anasema kama waagizaji hao wakitaka bidhaa zenye ubora basi zitakazoletwa nchini ni zile zenye ubora.
Anasema bidhaa bandia zinaletwa kwa sababu ndizo zinazoagizwa na wafanyabiashara.
Hata hivyo, Keegan alishangaa kwa nini bidhaa bandia zipo sokoni nchini kwani kila mwagizaji anapaswa kujaza nyaraka kadhaa anapoagiza bidhaa kutoka nje na moja kati ya nyaraka hizo ni zile zinazoonyesha bidhaa imetengezwa wapi na ubora wake ukoje.
“Ni kweli kuwa unapokwenda China unatengenezewa bidhaa yenye ubora kulingana na kiwango cha fedha ulizo nazo. Kuna bidhaa zinaitwa ‘master copy’, ukiiangalia kwa macho ni kama original (halisi), lakini ukweli ni kuwa ina ubora wa chini isipokuwa imeigizwa tu kutoka kwenye ile halisi,” anasema.
Mzunguko wa umasikini

Mahojiano na watu wengi yamebaini kuwa Watanzania wengi wamenaswa kwenye mzunguko wa umasikini kutokana na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora kwa kuvutiwa na unafuu wa bei.
Mathalani, wazazi wengi wamekiri kuwa huwa wanalazimika kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto wao mara kwa mara kutokana na ukweli kuwa vifaa wanavyonunua havina ubora.
“Lakini tunalazimika kuvinunua kwa kufuata unafuu wa bei. Mzazi unapoingia mitaani kutafuta mahitaji ya mtoto anapokaribia kurudi shuleni kinachoongoza fikra zao ni kupata vifaa vyote kwa bei ya chini, wachache sana ndio wanajali ubora.
“Matokeo yake, unaweza kununua viatu mwezi Disemba, lakini kabla ya likizo ya Pasaka mtoto akakutumia ujumbe kutoka shuleni kuwa anahitaji viatu vingine kwa sababu ulivyomnunulia awali vimeshaharibika,” anasema Musa Ngunichile, mkazi wa Tegeta.
Ngunichile anasema hayo yanatokea si tu kwa mzazi anayenunua mahitaji ya mtoto wake, bali kwa Watanzania wengi wanapotafuta mahitaji, hata ya vifaa vya nyumbani. “Kwa mfano hivi vifaa vya elektroniki, au hata haya matoi (wanasesere), unaweza kununua mjini, lakini toi likaharibika hata kabla hujafika nyumbani,” anasema.
Madhara

Kuna madhara ya aina nyingi kutokana na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora na bidha bandia.
Madhara makumbwa ambayo Watanzania wengi wanaweza kuwa bado na kumbukumbu nayo kutokana na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora ni tukio la zaidi ya watu 200 kuathirika kiafya baada ya kula mafuta yanayoaminika kuwa yalikuwa na sumu huko Yombo jijini Dar es Salaam.
Ingawa wafanyabiashara waliohusika kuuza na kasambaza mafuta hayo wamejulikana, lakini watu walioathirika hivi sasa wanalazimika kuingia mifukoni kutoa fedha kwa ajili ya kujitibia madhara ya kiafya waliyoyapata baada ya kutumia bidhaa hiyo yenye mushkeli, huku wafanyabiashara hao wakiwa nje kwa dhamana.
Mwaka jana yalikuwepo malalamiko kutoka kwa wakulima wa pamba katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa baada ya kuuziwa mbegu za pamba ambazo walipopanda hazikuota.
Sakata hilo lilisababisha mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kurushiana maneno na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ingawa malumbano hayo hayakutoa jibu la uhakika hasa kuhusiana na jinsi ambavyo wakulima waliopata hasara baada ya kuuziwa mbegu hizo watafidiwa vipi.
Pia, malalamiko ya wakulima kuuziwa viuatilifu ambavyo havifanyi kazi kama inavyotarajiwa au mbolea ambazo hazina ubora, yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara miongoni mwa wakulima katika maeneo kadhaa nchini.
Novemba mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, alilazimika kutoa siku saba kwa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), kukagua ubora wa mbegu ya zao hilo wilayani Kishapu, na kumpatia taarifa.
Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa maofisa ugani na baadhi ya viongozi, kwamba mbegu za pamba ambazo zilikuwa zinasambazwa wilayani humo kwa ajili ya msimu wa kilimo 2024/2025, zimeonekana kutokuwa na ubora.
“Mbengu zilizoletwa Kishapu kuna baadhi zimethibitika hazifai… Bodi ya Pamba mnapaswa kufanya ukaguzi wa mbegu zote za pamba ambazo zimeanza kusambazwa kwa wakulima wilayani Kishapu, mjihakikishie kama mbegu hizo zinafaa, kama hazifai mlete mbegu zingine zenye ubora, ili kazi hii ambayo nimetumwa na Rais ifanyike kwa ufanisi,” alisema.
Kabla ya hapo, msimu wa 2023/24 tatizo kama hilo lilijitokeza ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude, naye alipokea malalamiko kuhusu ubora duni wa mbegu hizo zilizosambazwa kwa wakulima.
Mkaguzi wa pamba wilayani huko kutoka Bodi ya Pamba (TCB), Thomas Tiluhongerwa, aliziangalia mbegu hizo na kuthibitisha kuwa si nzuri sababu zilikuwa na kiwango cha juu cha unyevunyevu.
Mei mwaka jana, familia moja huko Morogoro ilipata pigo baada ya watoto wao wawili kufariki baada ya nyumba yao kuungua moto.
Ofisa Habari Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Benjamin Bandula, alithibitisha kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo ulibainisha kuwa sababu kubwa ya kuungua kwa nyumba hiyo ni hitilafu ya umeme.
Watalaamu wa masuala ya umeme wanabainisha kuwa inapotokea hitilafu ya umeme, hali huwa mbaya zaidi iwapo nyaya au vifaa vilivyotumika kwenye mfumo wa umeme ni bandia au zisizo na ubora unaotakiwa.
Wapo watu wengi wameshawahi kulalamika kuharibikiwa na vifaa vya umeme au hata maeneo mengine nyumba kuungua kwa moto kutokana na hitilafu ya umeme. Ukaguzi unapofanyika inabainika kuwa moto huo ulisababishwa na matumizi ya nyaya au vifaa vya umeme ambavyo havijafikia viwango vinavyotakiwa.
Tatizo sugu

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CIT), tatizo la bidhaa bandia si geni hapa nchini.
Katika ripoti hiyo, CTI inaeleza mathalani kati ya mwaka 2010 na 2016, Tume ya Ushindani (FCC) ilikamata makontena 1,151 yaliyokuwa na bidhaa bandia.
Jumla ya watuhumiwa 1,711 waliohusishwa na bidhaa hizo walishughulikiwa huku thamani ya bidhaa hizo ikitajwa kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 2.89.
Hata hivyo, hakuna maelezo kuhusiana na jinsi waathirika wa bidhaa hizo walivyofidiwa.
Maeneo ambayo yalibainika katika utafiti huo kuwa sugu kwa bidhaa bandia ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya. Ilikadiriwa wakati huo kuwa kiwango cha bidhaa bandia zilizokamatwa ni takribani asilimia 10 ya bidhaa zote zilizokuwa sokoni.
Utafiti huo wa CTI ulibaini kuwa takribani asilimia 80 ya bidhaa bandia zote huingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam na pia bandari za Tanga na Zanzibar.
Hasara

Utafiti huo wa CTI ulibaini kuwa thamani ya jumla ya bidhaa bandia zote katika soko la Tanzania inakadiriwa kuwa dola za Marekani milioni 525 kwa mwaka.
Aidha, thamani ya bidhaa zilizoghushiwa katika soko la dunia, kwa mujibu wa internet Doug Palmer ya China, ilikadiriwa wakati huo kuwa ni Dola za Marekani 520 bilioni kwa mwaka.
CTI ilieleza katika utafiti wake huo kuwa hasara inayotokana na bidhaa bandia kuwa ni kati ya asilimia 15 na 25 ya mapato yote ya ndani kwa mwaka.
Hii inamaanisha kuwa kwa viwango vya bajeti ya mwaka huu (Sh49 trilioni), hasara hiyo ni sawa na kati ya Sh7.35 trilioni na Sh9.8 trilioni.
Hiki ni kiasi cha fedha kinachotosha kuendesha zaidi ya wizara tano kwa mwaka.
Hasara kutokana na bidhaa bandia inaziathiri pia kampuni zinazowekeza nchini. CTI inaeleza katika utafiti wake kuhusu kampuni moja inayojihusisha na biashara ya vilevi ambayo hadi wakati huo ilikuwa imefanya biashara nchini kwa zaidi ya miaka 23.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, katika kipindi cha miaka mitano ilipata hasara ya asilimia 20 katika soko kila mwaka kutokana na bidhaa zake kughushiwa, na kusababisha ipate hasara ya jumla ya Dola za Marekani milioni 10.
Hasara hiyo ikaisababishia serikali nayo kupoteza mapato ya takribani Dola za Marekani milioni nne.
CTI inasema kutokana na hali hiyo kampuni hiyo ilishindwa kupanua uwekezaji kwani ilipanga kujenga kiwanda cha kutengeneza vinywaji hivyo hapa nchini.
Kwa upande wa bidhaa za umeme, CTI inaitaja kampuni nyingine ambayo ilifanya biashara nchini kwa muda wa miaka 38, lakini katika miaka minne ya mwisho ikashuhudia hasara kubwa kutokana na wimbi la bidhaa bandia katika soko na kupata hasara ya kati ya Sh 38 bilioni na Sh40 bilioni.
“Kama kampuni hiyo isingepata hasara hiyo ingeweza kuwekeza zaidi kwa kujenga kiwanda cha vifaa vya umeme na kutoa ajira kwa Watanzania wengi,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Kinachosababisha

Ingawa serikali imekuwa ikijinasibu kuchukua hatua dhidi ya bidhaa bandia na zisizo na ubora, lakini tatizo hilo limeendelea kukua kila mwaka na kuathiri maisha ya watu na uchumi.
Inaelezwa kuwa uwezo mdogo wa serikali kudhibiti mipaka ni moja ya sababu kubwa ya bidhaa hizo kuendelea kutawala sokoni.
Hali kadhalika, inaelezwa kuwa bajeti finyu inayotengwa kwa ajili ya taasisi zinazohusiana na kudhibiti bidhaa bandia na zile zisizo na ubora kama vile TMDA na TBS au FCC inayoshughulikia ushindani kwenye biashara, ni sababu nyingine ya kushamiri kwa bidhaa hizo kwenye soko.
Pia inaelezwa kuwa rushwa miongoni mwa maofisa wanaopaswa kuongoza mapambano dhidi ya bidhaa hizo nayo inachangia kukua kwa tatizo hilo.
Kwa upande mwingine, kukosekana kwa mwamko miongoni mwa wananchi na pia umasikini kunasababisha kwa kiasi fulani watu kuendelea kuzinunua bidhaa hizo licha ya baadhi yao kujua madhara yake.
Kariakoo ni kawaida

Mjasiriamali wa vipodozi mwenye duka lake eneo la Goba jijini Dar es Salaam alimweleza mwandishi wetu kuwa suala la bidhaa bandia na zisizo na ubora ni jambo la kawaida kwa wafanyabiashara ambao wananunua bidhaa za jumla katika eneo la Kariakoo.
“Pale Kariakoo biashara hii ya bidhaa zisizo na ubora ni ya kawaida. Mtu ukienda unaonyeshwa aina mbili za bidhaa hiyo hiyo. Moja anaiita namba moja ambayo ndiyo ubora na namba mbili ambayo haina ubora halisi.
“Bei ya bidhaa hizo zinatofautiana, ile namba mbili ina bei ndogo. Hivyo ukikutana na mfanyabiashara ambaye lengo lake ni kubana matumizi anakimbilia ile bidhaa yenye ubora hafifu akifuata unafuu wa bei.
“Lakini kuna matukio mengine kwa wafanyabiashara wanaokwenda kununua bidhaa bila kujua. Hujikuta wakibambikiwa ile namba mbili bila wao wenyewe kujua na huko wanakoenda ndiko hugombana na wateja inapobainika kuwa bidhaa hiyo haina ubora,” anasema mfanyabiashara huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
(Katika toleo lijalo usikose kusoma kauli za mamlaka nyingine za udhibiti zinasema je.)